WADAU WAPINGA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE
Wadau wa elimu wameishushua serikali kuwa inawaongopea wananchi kwa
kutangaza kuwa viwango vya ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne
vimepanda.
Wakitoa maoni walisema ufaulu uliotajwa kuongezeka ni maelezo ya
kisiasa na kueleza kuwa serikali ilichofanya ni kuongeza madaraja ambayo
hayaijengi sekta hiyo.
Walikuwa wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti baada ya
serikali kutangaza kuwa kati ya wanafunzi 404, 083 waliofanya mtihani
mwaka jana 235, 227 wamefaulu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 58.25,
ikilinganishwa na 185,940 sawa na asilimia 43.08 waliofaulu 2012.
Washirika hao waliitaka serikali kuboresha mazingira ya walimu ya
kufundishia pamoja na nyumba za walimu , kuweka vifaa vya kujifunzia
wanafunzi mashuleni badala ya kufanya siasa kwenye eneo hilo.
WALIOPATA SIFURI WAMEPANDA NGAZI KIJANJA
Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo
(Chadema), alisema kilichofanywa na serikali ni kuongeza ufaulu wa
madaraja ambapo mwanafunzi aliyepata sifuri amepandishwa ngazi kijanja.
Alieleza kuwa kilichofanyika ni siasa; “wameona tumebakiza mwaka
kuingia kwenye uchaguzi mkuu wameamua kuwapooza wazazi kupitia matokeo
yaliyoongezwa madaraja, tusishabikie hili hata kidogo,” alisema na
kuongeza:
“Maslahi ya walimu hayajaboreshwa, mazingira magumu ya kujifunzia
na kufundishia leo tunaambiwa wanafunzi wamefanya vizuri haiingii
akilini hata kidogo,” alisema.
Alikumbusha kuwa watu wamekuwa wakipiga kelele kuhusu elimu na
kwamba matokeo haya yanadhihirisha kuwa ufaulu wanaoambiwa umeongezeka
umetokana na kuongeza madaraja ya ufaulu, lakini ujinga bado upo.
Akizungumzia shule za umma kuboronga, alizitaka shule za serikali
kujifunza kutoka kwa shule binafsi ambazo mara kwa mara zimekuwa
zikifanya vizuri kwa sababu wamekuwa wakichuja wanafunzi kupitia
mitihani.
MFUMO WA ELIMU UANGALIWE UPYA
Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa, Ruth
Meena, akitoa maoni yake alisema kuna haja ya kutazama upya mfumo wa
elimu kwa sababu uliopo unamtayarisha mwanafunzi kupata cheti na sio
kujifunza na kuelewa masomo anayofundishwa darasani.
“Ule uwelewa na utayari wa mwanafunzi kupokea kile anachofundishwa
haupo, naona wanafunzi wengi wapo mashuleni kwa ajili wanajua mwisho wa
siku watapata cheti, hawapo kwa ajili ya kuelimika,” alisema.
Kuhusu kufanya vibaya kwa shule za serikali, Profesa Meena alisema
uwekezaji uliopo kwenye shule hizo ni kwenye majengo lakini vifaa,
walimu havipo vya kutosha.
“Ni kweli zipo shule nyingi za kata zilizojengwa lakini hatujawekeza kwenye vifaa na walimu,” alisema.
Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla, yeye anasema matokeo hayo
ni ya kawaida kwani siyo mazuri na wala mabaya na kwamba katika shule
kumi bora hakuna hata moja ya serikali.
Dk. Kigwagwalla alisema ili kunusuru elimu serikali inatakiwa
kuongeza motisha kwa walimu, kupunguza kero zao na walimu wenyewe
wafundishe kwa bidii na kujitolea.
Pia alisema mabadiliko ya mitaala yaliyofanyika yaongezewe kasi na
serikali itekeleza ahadi yake ya kuimarisha miundombinu ya kufundisha
mashuleni.
TAHADHARI YA MNYIKA
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema ongezeko la ufaulu
la asilimia 15.17 unadhihirisha tahadhari aliyotoa Oktoba 30 mwaka jana
kuhusu mabadiliko ya viwango vya ufaulu yaliyotangazwa na serikali.
Alisema katika tahadhari hiyo alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
kuweka wazi kwa umma ripoti za uchunguzi zilizoundwa iwapo kupanda huko
kwa ufaulu ni matokeo ya kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza
au ni mabadiliko ya alama na madaraja.
HAKUNA KILICHOBORESHWA MASHULENI
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT), wilayani Chamwino mkoani
Dodoma, Amani Msanga, alisema kuwa serikali haina sababu ya kuwadanganya
wananchi kuwa kiwango cha ufaulu kimepanda.
“Hakuna kilichoboreshwa mashuleni, huku ni kuwadanganya Watanzania
kwa kusema matokeo yamepanda lakini sifuri bado zinatawala” alisema
Msanga.
Msanga alisema pamoja na kuwepo kwa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) lakini serikali haijatatua changamoto zilizopo kwenye shule zake.
Mratibu wa Shirika la Marafiki wa Elimu mkoani Dodoma (MED), David Makundi, alisema haoni kilichobadilika.
Makundi alisema kuwa madaliko ambayo yapo ni katika daraja la tatu
na la nne ambayo hayana tija kama daraja la kwanza na la pili.
Alisema mpango wa BRN bado haujatekelezwa kwa vitendo hivyo haoni ufaulu unaoelezwa kuwa umepanda.
No comments:
Post a Comment