Tuesday, 11 February 2014

KARIAKOO: WAFANYABIASHARA WAGOMA TENA



 SAM_3723 (FILEminimizer)



Wafanyabishara ambao wanamiliki maduka maeneo yote ya kariakoo leo asubuhi wameweka mgomo wa pamoja wakutofungua maduka yao wakipinga uamuzi wa TRA kutaka kila duka kuwa na mashine. Mitaa yote ya Kariakoo, Msimbazi, Uhuru, Lumumba, Aggrey, Mchikichi, Narung'ombe, Tandamti, Congo, kote maduka yamefungwa baada ya kutangaziwa na umoja wa wafanyabiasha.

Wafanyabiashara hao wa Kariakoo jijini Dar es Salaam wamefunga maduka yao kuanzia jana na hata leo pia kupinga utaratibu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wa kutoza kodi kwa kutumia mashine za elektroniki (EFD). 


Wafanyabiashara walifanya mgomo huo ili kushinikiza kuonana na ama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa au Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.
Wanadai kuwa mashine hizo za EFD zinauzwa bei ghali ya kati ya Sh800,000 hadi Sh1.2 milioni, gharama ya kuzifanyia matengenezo zinapopata hitilafu ni kubwa na pia wanadai kuwa kuna harufu wa ufisadi kwenye suala hizo kwa kuwa ni kampuni chache zilizochaguliwa kuuza mashine hizo.
Maduka karibu yote hayakufunguliwa tangu alfajiri tofauti na ilivyozoeleka na hata wafanyabiashara wachache waliojaribu kufanya hivyo walilazimika kuyafunga kwa hofu ya kufanyiwa vurugu na wenzao.
Baadhi ya maduka ya vifaa vya umeme, magodoro na friji yaliyopo Mtaa wa Uhuru yalikuwa wazi lakini baada ya muda mfupi yalifungwa.
Hata hivyo, maduka yaliyoko kwenye Soko Kuu la Kariakoo yalikuwa wazi muda wote.
Mgomo huo ulianza baada ya wafanyabiashara hao kupeana taarifa wakihamasishana kutokufungua maduka yao kushinikiza kusikitishwa kwa matumizi ya mashine hizo za kukokotoa kodi.
Msimamo wa Serikali kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara:
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo hauwezi kubadili msimamo wa Serikali wa kukusanya kodi kwa kutumia mashine za EFD. Alisema suala la bei haliwezi kuwa kigezo cha kugoma kwa kuwa baada ya kununua fedha zao zitarejeshwa kidogokidogo kwenye marejesho ya kodi.
“Changamoto iliyopo ni kwamba wafanyabiashara wengi hawajui kama fedha hizo wanazonunulia mashine watarejeshewa kwenye makato ya kodi. Hatuwezi kuzibadilisha mashine hizo kwa kuwa siyo kama simu za mkononi, zimetengenezwa kwa mfumo maalumu wa TRA,” alisema.
Aliitaka TRA kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu manufaa ya kutumia mashine hizo.

No comments:

Post a Comment