Saturday, 22 February 2014

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE

 1
Idadi ya ufaulu mtihani kidato cha nne mwaka jana  imeongezeka kutoka 185,940  hadi kufikia 235, 225, ikilinganishwa na mwaka 2012.
Vile vile watahiniwa 151,187 kati ya 404,083 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamepata ‘divisheni’ ziro.


Hata hivyo,  idadi ya waliopata daraja sifuri imepungua ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo wanafunzi 240,903 kati ya 397,132 waliambulia daraja hilo na kusababisha hamaki iliyoshinikiza viongozi wa sekta ya elimu kuwajibishwa.

Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar- es- Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la  Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, aliyeongeza kuwa idadi ya ufaulu kwa mwaka jana ilipanda ikilinganishwa na mwaka 2012.

Ongezeko hilo la watahiniwa 49,285 waliofaulu zaidi mwaka huo, limefanya kiwango cha ufaulu kupanda kwa asilimia 58.25 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa  mwaka 2012.

“Jumla ya watahiniwa  404,083 sawa na asilimia 94. 48 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 151,187 ambao ni  asilimia 42.91 walishindwa mtihani.” Alisema Dk. Msonde na kuongeza kuwa wasichana waliofaulu ni 106,792 sawa na asilimia 56.73,  wavulana ni 128,435 sawa na asilimia 59.58.

Watahiniwa  waliofaulu  moja kwa moja kutoka shuleni ni 201,152 sawa na asilimia 57.09, wasichana wakiwa 90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.

Alisema idadi ya wanafunzi  wa kujitegemea ilikuwa   34,075 sawa na asilimia 66.23 ikilinganishwa na  ya mwaka 2012 ambao idadi yao ilikuwa 2,619.

Watahiniwa wa mtihani wa Maarifa(QT), waliofaulu ni 6,529 sawa na asilimia ikilinganisha na watahiniwa 5,984  wa  mwaka 2012.

Akitangaza matokeo hayo mbele ya wanahabari alisema watahiniwa  walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana walikuwa 427,679, kati yao wasichana ni  199,123 sawa na asilimia 46.56.


Wavulana walikuwa ni 228,556 sawa na asilimia 53.44, huku watahiniwa wa shule wakiwa 367,163 na watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 60,516.

Alisema kati ya watahiniwa 427,679 waliosajiliwa kufanya mtihani huo, 404,083 sawa na asilimia 94.48 walifanya mtihani huo na watahiniwa 23,596 sawa na asilimia 5.52 hawakufanya mtihani huo.




Kwa watahiniwa wa shule 367,163 waliosajiliwa , 352,614 sawa na asilimia 96.04 walifanya mtihani, wasichana wakiwa 162,412 sawa na asilimia 96.07 na wavulana ni 190,202 sawa na asilimia 96.0.



Pia alisema watahiniwa 14,549 sawa na asilimia 3.96 hawakufanya mtihani.

Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea 60,516 waliosajiliwa  kufanya mtihani huo, 51,469 sawa na asilimia 85.05 walifanya mtihani huo, na watahiniwa  9,047 sawa na asilimia 14.95 hawakufanya mtihani.

Alisema  kwa  watahiniwa  18,217 wa mtihani wa maarifa (QT),  waliosajiliwa, 15,061 sawa na asilimia 82.68 walifanya mtihani huo na 3,156 sawa na asilimia 17.32 hawakufanya mtihani.



Kwa upande wa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja , alisema kwa watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 74,324 sawa na asilimia 21.09 wamefaulu katika daraja la I hadi la III wakiwamo wasichana 27,223 sawa na asilimia 16.77 na wavulana 47.101 sawa na asilimia 24.

Dk. Msonde alisema takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 0.61 na 16.72 ikilinganishwa na mwaka 2012.

 



Alisema watahiniwa wamefaulu zaidi masomo ya Kiswahili kwa asilimia 67.77 na somo ambalo wamefaulu kwa kiwango cha chini ni Hesabu kwa asilimia 17.78.
Kwa mujibu wa Necta wanafunzi waliong’ara ni Robina Nicholaus, Sarafina Mariki, Abby Sembuche   na  Janeth Urassa  wa Sekondari ya Wasichana ya Marian.

 

Wengine ni  Magreth Kakoko na Angel Ngulumbi wa   St. Francis, Joyceline Marealle wa Sekondari ya  Canossa,   Sunday Mrutu  wa Sekondari ya Anne Marie,  Nelson Rugola na Emmanuel Mihuba Sekondari ya  Kaizirege .


 

Kadhalika, shule zilizofanya vizuri zaidi  na kuingia katika kumi bora  katika kundi la shule zenye watahiniwa 40 ni  shule ya wasichana ya St. Francis, Shule ya wavulana na Marian, shule ya wasichana ya Fedha, shule ya Precious Blood, Canossa, Shule ya wasichana ya Marian, shule ya wasichana ya Anwarite, Abbey, Rosminini na Shule ya Seminari ya Don Bosco.

No comments:

Post a Comment