Friday, 14 February 2014

LOWASSA, SUMAYE NA NGELEJA kuhojiwa kuhusu kuivuruga CCM 

 
 
 
 
 Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndugu Phillip Mangula jana imewahoji watu watatu ambao wawili walishawahi kuwa Mawaziri Wakuu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
 
 Mawaziri hao waliohojiwa walifika mbele ya Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM kutoa maelezo juu ya tuhuma za kufanya kampeni za urais kabla ya wakati ni Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa,Waziri Mkuu wa Zamani Ndugu Fredrick Sumaye na Mbunge wa Sengerema Ndugu William Ngeleja ambaye pia alishawahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa White House pia kamati hiyo bado ina kazi ya kuwahoji viongozi wengine watatu ambao walishindwa kufika baada ya kuomba hudhuru kwani walikuwa na majukumu mengine ya kiserikali.
 
Ambao hawakufika jana kwa mahojiano hayo ni Waziri wa Mambo ya Nje Ndugu Bernard Membe ambaye yupo safarini nje ya nchi ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Ndugu Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Ndugu Januari Makamba. 
 
Akiwa amevalia mavazi rasmi ya CCM, Lowassa alihojiwa kwa takriban saa moja na nusu kwani aliingia katika kikao hicho saa 4:56 asubuhi na kutoka saa 6:40 mchana akiwa ametumia takriban saa moja na nusu na alitoka akiwa mwenye furaha.

Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo Lowassa: “Mazungumzo yalikwenda vizuri. Yalikuwa na lengo la kujenga chama kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Lowassa huku akitabasamu.

Muda mfupi baada ya Lowassa kutoka, Sumaye aliingia kuanzia saa 6:46 na kutoka saa 8:05.

Baada ya kutoka, Sumaye pia hakuwa tayari kuzungumzia kuhusu mahojiano hayo... “Tunawasubiri wakubwa watakavyotoa jawabu.” Alipoulizwa sababu za kutumia muda mwingi katika kikao hicho alisema: “Tulikuwa tunakunywa chai.”

Kwa upande wake, Ngeleja ndiye aliyetumia muda mfupi zaidi kwani aliingia katika ukumbi wa mahojiano saa 8:10 na kutoka 8:50.

Aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa nje ya ukumbi huo kuwa mazungumzo hayo yalikuwa ni ya kichama na kikazi zaidi na kwamba hizo ni taratibu za CCM kuwaita wanachama wake kwa ajili ya kutoa maelekezo.

Kuhusu kutangaza nia ya kugombea urais kabla ya muda uliopangwa na chama, Ngeleja alisema wanaongozwa na kanuni na taratibu na kwamba wakati wa kutangaza kugombea urais haujafika.

Alisema hakuitwa kuhojiwa kwa kutangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda... “Sijatangaza, sijasema, sina ugomvi huo.”
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa mahojiano ya makada hao watatu jana, Kinana alisema shughuli ya kuwahoji wengine itaendelea leo.
 

No comments:

Post a Comment