Thursday, 20 February 2014

BUNGE LA KATIBA WAJUMBE WADAI POSHO NI NDOGO


 Majina ya Bunge la Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania latangazwa

Sakata la posho na fedha za kujikimu kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, limezua kizaa zaa ndani na nje ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya baadhi ya  wajumbe wa Tanzania Bara kulalamikia posho ya Sh. 300,000 kuwa ni ndogo.

 

Kizaazaa hicho kiliibuka baada ya wajumbe wa Tanzania Bara kupata taarifa kuwa wenzao wa Baraza la Wawakilishi, wanalipwa kiasi sha Sh.
420,000 kwa siku.

Walidai kuwa baada ya kufika Dodoma, wawakilishi walilalamika kwa Spika wao na kuwasiliana na Serikali ya Zanzinar na kukubali kuwaongezea malipo.

Mvutano huo uliibukia ndani ya ukumbi wa Bunge wakati wajumbe wakikabidhiwa nakala za Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum, chini ya Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho.

 

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge jana, Mjumbe Richard Ndassa, ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo ndani ya ukumbi wa bunge kabla waandishi wa habari kuruhusiwa kuingia ndani, alilalamikia tofauti ya malipo ya posho kati ya wajumbe kutoka Bara na Visiwani.
 

Mapema asubuhi, waandishi wa habari hawakuruhisiwa kuingia ukumbini baada ya askari waliokuwa kwenye lango C linalotumiwa pia na waandishi wa habari kuingia ndani, walisema walipewa maelekezo kuwa waandishi hawakuruhusiwa kuingia kwa wakati huo.Hata waandishi waliowahi kuingia ndani, walitolewa nje.
 

Hata hivyo, baada ya kuwa nje kwa zaidi ya saa moja hivi, waandishi wa habari waliruhusiwa kuingia ndani na kukuta mjadala huo ukiwa unamalizika.
 

Akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa Bunge, Ndassa, alisema: “Inashangaza kuwa Bunge ni moja, lakini malipo ni tofauti, jambo ambalo limezua malalamiko. Sisi wabunge hatuna shida, tuna mishahara na maisha ya Dodoma tumeyazoea, ila tumesikia wenzetu 201 wanalalamikia posho ndogo, fedha wanayolipwa haiendani na gharama za maisha kwa sasa, kwani kuitaja inaonekana nyingi, lakini kwa matumzi si nyingi.”
 

Alisema iwapo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano watamuomba Spika waongezewe posho, wajumbe 201 watakosa mtetezi, jambo ambalo limemsukuma kuzungumzia suala hilo.
 

Alisema Bunge Maalum la Katiba ni muhimu na linatengeneza hatima ya maisha ya Watanzania kwa miaka 50 hadi 100 ijayo, na kwamba kumlipa mjumbe kiasi cha Sh. 220,000 baada ya kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge na Sh 80,000 ya malazi kwa siku ni fedha isiyotosheleza mahitaji kulingana na hadhi ya wajumbe.
“Kwa hadhi yetu unatakiwa kuishi kwenye nyumba ya Sh. 70,000 hadi Sh. 100,000, hujamlipa dereva, mafuta,  msaidizi, bado sijafanya shughuli za mahusiano, ukiangalia fedha yote inaisha, wajumbe hawa hawana kiinua mgongo baada ya kazi hii kwisha hakuna malipo mengine,” alisema.

 

Aidha, alisema malipo ya Sh. 220,000 kwa siku za mapumziko ya mwishoni mwa wiki na sikukuu hayatolewi na mjumbe anapougua na kulazwa hospitalini hulipwa Sh. 40,000.
 

Alisema taarifa alizonazo ni kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walilipwa Sh. 500,000 kwa siku huku madereva wao wakilipwa Sh. 220,000 kila mmoja na kwamba mjumbe wa Bunge Maalumu analipwa posho sawa na dereva wa Tume.
 

Alisema ili wajumbe watulie na kufanya kazi nzuri wanatakiwa kulipwa vizuri na kuwezesha akili zao kutulia na kwamba miongoni mwa wajumbe hao wamo wafanyabiashara na wasomi ambao kwa siku wanaweza kupata fedha zaidi ya hizo.
Ndassa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), alisema hofu kubwa ni kuwa kadri siku zinavyokwenda wajumbe hao watapungua kwa kuwa wengi watashindwa gharama za maisha na kuamua kutafuta fedha kwenye maeneo wanayotoka.

 

Mjumbe Selemani Nchambi, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa kazi ya kutunga Katiba ni ngumu kuliko ya Rasimu ya Katiba, hivyo wajumbe wa Bunge hilo wanastahili kulipwa fedha za kutosha ili watekeleze majukumu yao kikamilifu.
Alisema miongoni mwa wajumbe wapo maprofesa na madaktari ambao wanapokwenda kuwasilisha taarifa mbalimbali za kitaaluma hulipwa Dola 500 kwa saa kadhaa, hivyo ni vigumu kukaa kwa siku zote kwa malipo hayo.

 

Alisema iwapo serikali itashikilia msimamo wake ipo hatari ya kusikia mjumbe amepata matatizo ikiwamo kuvamiwa na kukatwa na panga na kusingiziwa sababu za kisiasa, lakini chanzo kikubwa kitakuwa ni malipo duni yanayomlazimisha kuishi katika hoteli ya malipo madogo.Alisema ni vema wananchi wakatambua kuwa kinachotengenezwa ni moyo wa Tanzania kwa miaka mingi ijayo.
 

Mjumbe Joshua Nassari, alisema wajumbe hao wana haki ya kudai nyongeza hiyo kutokana na hali ya maisha ilivyo na kwa malipo hayo ipo hatari ya wajumbe wengine kuondoka kabla ya kumalizika kwa kazi muhimu.
 

“Siku za mapumziko hawatalipwa posho ya Sh. 220,000, watalipwa fedha ya malazi ambayo ni Sh 80,000, ni ndogo sana, serikali iangalie mtu asije kutunga sheria akiwa na mawazo,” alisema Nassari ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema).
 

Mjumbe Sadif Juma Khamisi, alisema fedha hiyo ni ndogo hasa ikizingatiwa kuwa wajumbe wengi wanatoka kwenye maeneo yao wameacha
kazi zao na hawana mshahara.

 

Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge (CCM), alisema iwapo maofisa wa Bunge walioandaa kanuni walitumia miezi nane na walilipwa fedha ya kutosha iweje wajumbe ambao wana kazi kubwa walipwe fedha kidogo isiyotosheleza mahitaji.
 

Kufuatia malalamiko hayo, Kificho alisema suala hilo litapelekwa ngazi husika na kuangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na serikali.
 

Naye Mjumbe, Anna Abdalah, aliwaomba wajumbe hao kuwa makini na kufanya kikao kwa utulivu ili kuepusha kikao hicho kugeuka kuwa mkutano wa hadhara.
 

Anna ambaye pia ni Mbunge (Viti Maalum- CCM), alisema ni vyema wakaishuruku Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi ngumu kwa kuwa wajumbe hao wasingeweza kuikamilisha kwa muda waliopangiwa.
 

Wakati mjumbe huyo akizungumza, baadhi ya wajumbe walikuwa wanawasha vipaza sauti na kuzungumza pasipo utaratibu wakisikika wakisema ‘taarifa mwenyekiti', ‘kuna jambo la dharura’, ‘hoja mwenyekiti’ hali iliyosababisha ukumbi huo kugeuka kuwa gulio.

 

Kuhusu madai ya wawakilishi kulipwa Sh. 420,00, Kaimu  Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florence Turuka, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa posho inayotolewa na serikali kwa wajumbe wote ni Sh. 300,000 kwa siku na siyo Sh. 420,000.
 

Katika hatua nyingine, Dk. Turuka pia alitoa ufafanuzi kuhusiana na malalamiko ya Baraza la Maaskofu la Pentekoste Tanzania (TPC) kwamba wamebaguliwa kutokana na majina ya wawakilishi wao kutoteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba.
 

Alisema kuwa wamefuatilia katika mfumo wa takwimu na kubaini kuwa TPC haikupeleka majina kwa ajili ya uteuzi.
 

Kadhalika, alisema kuwa serikali imebaini kwamba jina la mjumbe mmoja kati ya mawili yaliyokuwa yanafanana lilikwenda kimakosa na kubakiza aliyestahili na imeshatoa taarifa kwa Ofisi ya Bunge Maalum la Katiba.

No comments:

Post a Comment