Thursday, 27 February 2014

WARAKA CCM WAZUA BALAA


Waraka unaodaiwa kuandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kutoa maelekezo juu ya katiba mpya kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba umezidi kuibua mapya baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuja juu na kutaka mwenyekiti wa chama tawala ambaye ni Rais Jakaya Kikwete atoe msimamo wake kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ni kinyume cha makubaliano baina yake na viongozi wa vyama vya siasa.


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ndiye aliyeibua suala hilo jana wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kalenga, kwenye Kijiji cha Tanangozi katika kampeni zinazoendelea za uchaguzi mdogo wa ubunge ambako chama hicho kimemsimamisha Grace Tendega. 


Uchaguzi huo unafanyika kuziba nafasi ya Dk. William Mgimwa aliyefariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kloof Med-Clinic Pretoria Afrika Kusini, Januari mosi mwaka huu.

Slaa alisema kuwa Rais Kikwete akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa Februari 6, mwaka huu kabla ya kutangaza wajumbe 201 wa Bunge la Katiba, alisisitiza umuhimu wa kila mjumbe kutanguliza maslahi ya taifa wakati wa mjadala wao kuhusu katiba mpya badala ya kujali vyama vyao, makundi wanayotoka na utashi binafsi.


Slaa alisema kuwa hata hivyo, inashangaza kuona kuwa hivi sasa, CCM inayoongozwa na Rais Kikwete inatenda kinyume cha maelekezo hayo kwa kutanguliza maslahi ya chama chao badala ya taifa, tena kwa kuibua mipango hiyo katika vikao vyao.

Slaa alitoa mfano kuwa hivi karibuni, CCM iliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba wanaoiunga mkono CCM kuhakikisha kuwa wanatetea msimamo wa chama chao katika muundo wa serikali ya muungano ambao ni wa kuwa na serikali mbili na siyo tatu kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya pili ya katiba hiyo. 


Aidha, alizungumzia pia waraka aliodai kuwa ni wa siri wa CCM unaoelekeza namna katiba mpya inavyopaswa kuwa na kisha kutaka kuusambaza (waraka huo) kwa wajumbe wanaoiunga mkono CCM; mambo ambayo amedai hayaashirii hata kidogo utekelezaji wa kile alichokiasa Rais Kikwete hadharani wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa.

Slaa alisema Chadema imeuona waraka wa siri ambao ulipelekwa kwa Kamati Kuu (CC) kupata baraka ili utumike kama mwongozo katika kubadili baadhi ya mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya na tena ulipangwa kusambazwa kwa wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba wanaoiunga mkono CCM.


"Tunataka ufafanuzi kuhusiana na waraka huo ambao ulipelekwa kwenye kamati Kuu (ya CCM) iliyokaa siku chache zilizopita. Chadema hatukubaliani na hili la kuipinga rasimu ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba kwa kuwa yaliyomo katika rasimu hiyo ni mawazo ya Watanzania," alisema Dk. Slaa.


Alisema asilimia 60 ya Watanzania wameridhia mambo yaliyomo katika rasimu ya pili ya katiba na kwamba kuyachakachua kutokana na hila za kisiasa ni kufifisha fikra na mitazamo ya Watanzania kuhusu wanachokitaka katika miaka 50 ijayo.

Alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu, alisema kuwa hayo ni masuala ya CCM na hivyo ofisi yake haiwezi kuyatolea maelezo. 
 

“Suala la waraka unaodaiwa kuwa wa CCM waulize CCM wenyewe...siyo Ikulu,” alisema.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa juzi akiukana waraka huo wenye kurasa 22 unaodaiwa kutoa maelekezo juu ya namna wajumbe wanaoiunga mkono CCM wanavyopaswa kutoa mapendekezo yao katika maeneo muhimu yanayogusa ustawi wake kwenye kila ibara, ikiwamo inayozungumzia muundo wa Muungano.

No comments:

Post a Comment