MKUTANO WA BUNGE LA KATIBA KUANZA KESHO
Katibu wa bunge doctor Thomas Kashililah
Bunge la Katiba litaanza mkutano wake kesho kwa uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu wake.
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashilila, alitangaza jana mjini Dodoma kuwa Mwenyekiti wa kudumu na Makamu wake watachaguliwa Februari 21 pamoja na Katibu na msaidizi wake. Katibu na msaidizi wake wataapishwa siku hiyo hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Dk. Kashilila ambaye alifuatana na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, Mwenyekiti na Makamu wake watakula kiapo Februari 22. Wajumbe wataapa kuanzia Februari 22 hadi 24, siku ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano atalizindua Bunge hilo.
Rasimu ya Katiba mpya itawasilishwa katika Bunge hilo Februari 25 na mjadala kuanza rasmi Februari 26.
“Baada ya uzinduzi huo kufanywa ndiyo Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwa mpangilio tuliouanisha katika ratiba ambayo tutakuwa tumewapa...kwa hiyo baada ya pale Rasimu ikiwasilishwa na kanuni zitakuwa zimeainisha ni kwa utaratibu gani Rasimu hiyo kabla ya kuwasilishwa itajadiliwa hatua kwa hatua mpaka mwisho, ambapo sasa itakuwa imepatikana Katiba inayopendekezwa ili iende kwa wananchi kwa ajili ya kupata ridhaa,” alisema Dk. Kashilila.
UKARABATI SH. BILIONI 8.2
Akizungumzia gharama za ukarabati wa Bunge zima alisema limetumia jumla ya Sh. bilioni 8.2, kati ya hizo usafirishaji wa viti hadi kufungwa zimetumika Dola za Marekani milioni moja.
“Haya yote mliyoyaona yamefanyika hapa ni mambo ya kawaida ambayo yalikuwa kwenye bajeti la Bunge la Muungano wa Tanzania...katika bajeti iliyopishwa mwaka jana Juni, si mambo mapya yalikuwa tu yapo kwenye mchakato, sasa yote yamefanyika kwa wakati mmoja.
POSHO SH. 300,000 KWA SIKU
Kuhusu posho za wajumbe wa Bunge hilo, alisema wajumbe wote wa Bunge hilo wanalipwa posho maalum Sh. 300,000 kila mmoja kwa siku na si 700,000 kama ilivyokuwa inadaiwa.
“Sisi tumesikia kuwa Wabunge wa Bunge la Katiba wanalipwa 700,000 na wala hatujui hili limetoka wapi, kwanza mamlaka ya kuidhibisha posho ni la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na hajaidhinisha Sh. 700,000.
“Kwa hiyo posho aliyoidhinisha ni posho inayolipwa sasa..kwa maana fedha ya kujikimu ni sawa sawa na viwango vingine, kwa maana posho ya kikao na posho ya usafiri imechanganywa kwa pamoja inalipwa kama ni posho ambayo ni ya kawaida ambayo ni Sh. 220,000.
“Jumla Mbunge wa Bunge Maalum akija Dodoma akiingia kwenye kikao atalipwa Sh. 300,000,” alisema
WAJUMBE BUNGE LA KATIBA
Wajumbe wa Bunge hilo jana walianza kuingia kwenye viwanja vya Bunge kwa ajili ya kufanyiwa usajili ikiwa ni pamoja na kupiga picha za vitambulisho.
Zoezi hilo lilianza jana asubuhi katika Ofisi ya Bunge na kuendeshwa na maofisa wa ofisi ya Bunge.
No comments:
Post a Comment