JAJI WARIOBA ASISITIZA UMUHIMU WA MUUNGANO
Pia amesema kupendekezwa kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika haina maana ya kuunda nchi mpya, bali kinachopendekezwa ni kutenganisha mamlaka ya mambo ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano.
Warioba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Kitaifa la maridhiano, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kushirikisha viongozi mbalimbali na serikali na vyama vya siasa.
Alisema Tanganyika na Zanzibar hazina hadhi ya Jamhuri, na Kwamba taswira ya Muungano wa serikali tatu unaopendekezwa katika rasimu ya Katiba imejengwa katika ibara ya 1 inayoeleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi, na ni shirikisho lenye mamlaka kamili.
Alisema Muungano wa Serikali Tatu unaopendekezwa umezingatia mamlaka tatu zilizomo ndani ya Jamhuri ya Muungano hivi sasa, yaani Mamlaka ya Mambo ya Muungano yanayosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Nyingine ni Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar yanayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kadhalika, Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika ambayo kwa sasa yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano.
Akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, alisema huenda mjadala wa Muundo wa Muungano katika Bunge maalum la Katiba ukawa mkali kwa kuchangiwa na wanasiasa ambao mara nyingi wamekuwa si wakweli kuhusu umuhimu wa kulinda muungano.
Pia alisema ni vema bunge hilo likazingatia na kutafakari mambo mengi ambayo yamefanyika katika Muungano na kuyazungumza kwa uwazi ikiwezekana kufikiria kuongeza masuala hayo badala ya kuyapunguza.
No comments:
Post a Comment