Friday 28 February 2014

BENKI YA DUNIA YABANA MSAADA KWA UGANDA

 

Benki ya dunia imebana msaada wa dola milioni 90 kwa Uganda , siku chache tu baada ya Rais Yoweri Museveni kutoidhinisha sheria mpya dhidi ya mapenzi ya jinsia moja.

Benki hiyo imesema kuwa inataka kufanya tathmini yake kuhakikisha kuwa malengo yake ya maendeleo nchini Uganda katika sekta ya afya, ambayo msaada huo ulikuwa unanuiwa, hayataathirika .

Sheria iliyoidhinishwa na Rais Yoweri Museveni, ilitiwa saini Jumatatu na inatoa adhabu kali kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Wafadhili wengine tayari wameanza kusitisha misaada Uganda. Wahisani kama Denmark na Norway wamesema kuwa wataanza kufadhili mashirika moja kwa moja badala ya serikali.

Aslimia 20% ya bajeti ya Uganda inategemea michango ya wafadhili.
Mpaka sasa nchi tatu za Ulaya zimeamua kukata misaada yao kwa mamilioni ya dola.

Wizara ya fedha ya Uganda imesema inasubiri mawasiliano rasmi ya nchi husika, na iko tayari kukabiliana na athari za hatua hiyo.

Hadi kufikia sasa Waziri wa Fedha Wa Sweden, akiwa mjini Kampala, alisema waekezaji kutoka nchi yake watakuwa na wakati mgumu kuweka pesa zao nchini Uganda kwa sababu watakuwa na hofu kuwa sheria yo yote inaweza kupitishwa kuwadhulumu watu.

Jana serikali ya Uholanzi ilisema itazuia kwa muda misaada kwa Serikali ya Uganda. Norway na Denmark pia zimetangaza kupunguza au kusimamisha kwa muda misaada yake kwa Uganda.

KURA YA SIRI YAWAGAWANYA WABUNGE BUNGE LA KATIBA


 

Mjadala  mkali wa ama kuwa na utaratibu wa kupiga kura ya siri au ya wazi, umezuka na kuwagawa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, katika semina ya wajumbe hao kujadili Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.
Kama ilivyokuwa juzi usiku, jana pia baadhi ya wajumbe wakiwamo wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliendelea kuweka msimamo wa kuwa na utaratibu wa kura ya wazi badala ya kura ya siri wakitaka kifungu cha 38 (1) hadi (6) cha Rasimu za Kanuni la Bunge Maalum kuhusu kura ya siri kifutwe na kuwe na utaratibu wa kura za wazi.

 
BULAYA
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM), ndiye alikuwa wa kwanza kuweka bayana msimamo wake akipingana na wengi kutoka CCM wanaotaka kura za wazi.

Alisema: “Napendekeza utaratibu wa kura za siri ndio utaratibu niliouzoea…nitasema kweli na fitina kwangu ni mwiko, nitapiga hapa kura za siri, kwanini unataka nipige kura ya wazi unataka kujua nini toka kwangu.”

“Tusitengeneze mazingira ya kuvurunga utaratibu wa kupiga kura na sasa tupige kuwa za wazi, hilo hapana,” aliongeza.

Alisema tangu zamani ndani ya CCM kuna utaratibu wa kupiga kura za siri, na hata katika chaguzi mbalimbali utaratibu wa kura za siri ndio unaotumika.Alisema kwenda kinyume cha utaratibu huo ni kukiuka sheria za nchi zinazotaka kura zipigwe kwa siri.

 
KAPUYA
Naye Profesa Juma Kapuya (Urambo Magharibi CCM), alisema iwapo watapiga kura za siri watatoka bungeni humo wakiwa wameimarika.

Alisema kinachotakiwa wakati huu wa mchakato wa kujadili Rasimu ya Katiba mpya ni kuifanya katiba hiyo kuwa mali ya Watanzania wote.

“Tunachotakiwa hapa ni ‘ownership’ (umiliki) wa hiyo katiba, isije ikawa tunatoka hapa tukiwa na katiba yenye umiliki wa watu wachache au kikundi kimoja tu cha watu,” alisema.

 
KILANGO
Anne Kilango Malecela (Same Mashariki-CCM), alishauri kuwa kabla ya kufikia uamuzi wa kupiga kura wa ama ziwe za wazi au za siri ni vema wajumbe wakapiga kura kwanza kufikia uamuzi huo.

“Kila tunaloamua tuamue kwa umakini mkubwa sana. Waliozungumzia kuhusu utaratibu wa kura za siri wamenishawishi na wale waliozungumza kuhusu kura za wazi nao pia wametoa ushawishi…Hakuna kitu kizuri kama kuwapa watu walio wengi,” alisema.

 
SHEIKH KUNDECHA
 Mjumbe kutoka Kundi la Dini, Sheikh Mussa Kundecha, alisema kura za siri ni muhimu sana na litawaacha wajumbe katika hali ya amani na alitaka dhana ya uwazi ibaki katika kuhesabu kura na siyo wakati wa kupiga kura.

 
MTIKILA
Mchungaji Christopher Mtikila, alikataa utaratibu wa kuwa na vikundi vilivyojitokeza bungeni kurubuni baadhi ya wajumbe ili wafuate misimamo ya vyama fulani au watu wachache.

“Kama kuna mtu yeyote hapa na tunasikia anafanya vikao vya kurubuni wajumbe na aache kabisa. Wapo wajumbe hapa wanadai kuwa utaratibu wa kura za wazi utawafanya kuwa majasiri…sijaona mtu hapa mwenye ujasiri kuliko mimi,” alisema.

Alisema ni aibu kwa wajumbe kuzungumzia utaratibu wa kuwa na kura za wazi kwani kwa kufanya hivyo wanapoka haki za msingi za binadamu.

“Haki ya msingi katika ustaarabu wa kidemokrasia ni kupiga kura za siri,” alisema na kuongeza: “Hata wewe mwenyekiti wa muda (Pandu Ameir Kificho) umechaguliwa kwa kura za siri.”

 
GAMA
Hata hivyo, Dk. Zainab Gama, alitaka wajumbe lazima wawaonyeshe watu wanaowawakilisha nini wameamua na wanaweza kufanya hivyo kwa kupiga kura za wazi.

“Ukitaka siri kuna watu wamekuleta hapa na sasa unaogopa tena watu waliokuleta…tuache woga tuwe wajasiri kwa kupiga kura za wazi,” alisema.

 
THABIT
Mjumbe kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mahmood Kombo Thabit, alitaka kifungu chote cha 38 cha Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum kinachozungumzia kura za siri kifutwe.

Alisema wakati Zanzibar wakibadilisha katiba yao walifanya kura za wazi hivyo akataka hata katika bunge hilo utaratibu wa kura za wazi utumike.

 
NDESAMBURO
Philemon Ndesamburo (Mbunge wa Moshi Mjini-Chadema), alipinga utaratibu wa kura za wazi akiwataka wajumbe waache ushabiki katika jambo hilo muhimu.

“Tunapiga kura za siri ili kuamua nini Watanzania wanataka…mwisho wake mtasema hapa hiyo Rasimu mnataka kuibadilisha. Hiyo siyo haki ya msingi. Tuache mitizamo ya vyama vyetu kule nje na siyo humu ndani,” alisema.

 
MAZIKU
Dk. Masele Maziku alisema anashangaa kuona wajumbe wanataka kura za wazi, lakini katika vikao vya kamati za Bunge hilo wameamua kuwapiga marufuku waandishi wa habari kuripoti habari zake.

 
GEKUL
Pauline Gekul (Viti Maalum Chadema), alisema: “Utaratibu wa kura za siri hauna mjadala.”

Alitaka wajumbe kutoshawishiwa na baadhi ya misimamo ya makundi au vyama huku akisema wapo wanaotaka muundo wa serikali mbili na wale wanaotaka serikali tatu.

Alisema ni kujidanganya kudai utaratibu wa kura za wazi kwani hata wakiamua wawapigie kura kwa kusimama nyuma ya wajumbe wanaotajwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo, Andrew Chenge na Samuel Sitta, kila mmoja atakimbia humo bungeni.

“Wapo wapi, watakimbia humu ndani tukisema tusimame nyuma ya wagombea hao,” alisema.

 
DUNI
Naye Juma Duni Haji (Baraza la Wawakilishi-CUF), alisema kura ya siri ni lazima.

“Kura ya siri ndiyo iliyonipa mimi hifadhi ya kutotiwa adabu…tumekuja hapa kwa makundi na kundi moja limeanza nje kueleza misimamo yao,” alisema.

Alisema utaratibu wa kutumia kura za wazi wakati wa Bunge Maalum la Katiba siyo wa kwa Tanzania tu, kwani hata nchi za Ulaya zilitumia utaratibu.
“Kama tunataka kutoka humu ndani kwa umoja lazima utaratibu wa kura za siri utumike,” alisema na kuongeza kuwa mawazo kinzani lazima yatakuwapo ndani.

 
MIPASHO YAIBUKA
Mchango wa Duni hasa baada ya kuzitaja baadhi ya nchi za Ulaya kuwa zimetumia utaratibu wa kura za siri,  Asha Bakari Makame (CCM), alianza vijembe kwa kudai kuwa nchi zote zilizotajwa na mjumbe aliyepita ni za mashoga.

 
SAFARI ATAHADHARISHA
Hatua hiyo ilimfanya mjumbe Profesa Abdallah Safari (Chadema) kuomba utaratibu kwa mwenyekiti akitaka mjumbe aliyesema nchi hizo ni za kishoga athibitishe au la afute kauli yake kwani inaweza kusababisha mahusiano mabaya ya kibalozi na nchi hizo.

Mwenyekiti Kificho aliwakumbusha wajumbe kazi iliyowaleta bungeni hapo na kwamba maneno yaliyotamkwa na Asha siyo yaliyowaleta bungeni humo.

“Hatujakaribisha jambo hilo, sitaki tuliendeleze,” alisema.

 
RUNGWE
Hashimu Rungwe, aliwashangaa wanaotaka utaratibu wa kura za wazi huku akimnukuu Rais Jakaya Kikwete kuwa alishawaambia wajiandae kisaikolojia.

“Tuache kufikiri kwa kutumia matumbo, tunavyo vichwa vyenye betri zinazochaji…upigaji wa kura uwe wa siri, Bunge hili tunataka kukiuka sheria yetu wenyewe, hao wachache wenye kutisha wenzao hapa waache.

“Tuwe makini, wachache wasivuruge mahusiano yetu mataifa mengine,” alisema.

Alisema hata hao wanaodai kuwa na ujasiri wa kupiga kura za wazi hawawezi kusimama mbele ya Edward Lowassa na wengine wanaotaja kuwania urais na kupiga kura za wazi, watakimbia

TFF YAVUNJA MKATABA NA KOCHA WAKE


Hatimaye Shirikisho la Kabumbu nchini Tanzania TFF limetangaza kuvunja mkataba wake na Kocha mkuu wa Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars Kim Poulsen kwa kile kilichoelezwa maafikiano ya pamoja baina ya kocha huyo,TFF, na Serikali.

Jamal Malinzi ambaye ni Rais wa Shirikisho la soka Tanzania amesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida hasa baada ya wadau mbali mbali kuona kuwa huu ni wakati wa kufanya mabadiliko ya lazima katika benchi la ufundi la Taifa Stars ambayo inajiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Fainali za kombe la mataifa Afrika hapo mwakani zitakazofanyika nchini Morocco.

Kuhusu gharama za kuvunja mkataba na Kocha huyo Bwana Malinzi amesema serikali haitagharamia uvunjaji huo wa mkataba na kocha huyo na badala yake wapo wadau waliojitokeza kugharamia kutokana na kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko katika kipindi hiki kwa faida ya soka la Tanzania.

Kwa Upande wake Kocha Kim Poulsen amesema na rekodi yake inaonyesha kuimarika kwa soka la Tanzania katika kipindi cha takriban miaka miwili aliyokuwa akikinoa kikosi cha Taifa Stars lakini kusitishwa mkataba ni jambo la kawaida kwa kocha yeyote baada ya kipindi fulani kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine na ndiyo sehemu ya maisha.

“Kama kocha unapoona ndiyo umefanya kazi yako,unapaswa kuangalia mbele zaidi baada ya kufanya kazi yako si lazima uendelee kuwa hapo, mnakaa na kujadiliana na kuachana kwa amani kisha unapaswa kusonga mbele,ninaondoka nikiwa najivunia kipindi nilichofundisha soka hapa,na ninawatakia kila la kheri Tanzania na Taifa Stars kwa ujumla.”alisema Poulsen.

Kuhusu Kocha mpya wa Taifa Stars Jamal Malinzi ambaye ni Rais wa TFF amesema hadi sasa wapo makocha watatu raia wa Uholanzi ni wawili na Mjerumani mmoja wanaosailiwa kwa ajili ya kumrithi Kim Poulsen,lakini moja ya vigezo Malinzi amesema kuwa ni lazima kocha huyo awe amewahi kuipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika moja ya nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara.

Katika hatua nyingine kocha Salum Madadi ameteuliwa kukaimu nafasi iliyoachwa wazi na Kim Poulsen ambapo kocha huyo akisaidiwa na Hafidh Badru kutoka Zanzibar watasimamia Taifa Stars kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia iliyoko kwenye kalenda ya FIFA baadaye mwezi ujao.

SHAMBULIZI SOMALIA


Mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejilipua ndani ya gari na kuwauwa watu 12 na kujeruhi wengine wanane mjini Mogadishu Somalia.

Mlipuko huo umetokea nje ya makao makuu ya maafisa wa usalama .
Mwandishi wa BBC anasema kuwa waliofariki ni maafisa usalama na wengine raia wa kawaida waliokuwa katika mkahawa karibu na hapo.

Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi huku vikosi vya nchi hiyo vikipambana na wanamgambo wa al shaabab.
Kundi la wanamgambo la Al Shabaab limekiri kufanya shambulizi hilo ambalo limetokea chini ya wiki mbili baada ya kundi hilo kushambulia ikulu ya Rais mjini Mogadishu.

Msemaji wa kijeshi wa kundi hilo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa huu ndio mwanzo tu wa kundi hilo kushambulia Mogadishu na kwamba operesheni yao itaendelea.

Alisema kuwa shambulio hilo lililenga maafisa wa usalama waliokuwa wameketi katika mkahawa mmoja na kuwaua watu 11 huku 15 wakijeruhiwa.
Polisi walisema kuwa takriban watu 10 walifariki katika mkahawa huo ambao unapendwa sana na maafisa wa usalama.

Ingawa kundi la Al Shabaab liliondolewa kutoka mjini Mogadishu na miji mingine, lingali linadhibiti sehemu kubwa za nchi hiyo.
Pia limekuwa likifanya mashambuzli makali dhidi ya serikali na kutatiza juhudi zake za kutaka kudhibiti baadhi ya sehemu za nchi hiyo

Thursday 27 February 2014

WARAKA CCM WAZUA BALAA


Waraka unaodaiwa kuandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kutoa maelekezo juu ya katiba mpya kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba umezidi kuibua mapya baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuja juu na kutaka mwenyekiti wa chama tawala ambaye ni Rais Jakaya Kikwete atoe msimamo wake kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ni kinyume cha makubaliano baina yake na viongozi wa vyama vya siasa.


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ndiye aliyeibua suala hilo jana wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kalenga, kwenye Kijiji cha Tanangozi katika kampeni zinazoendelea za uchaguzi mdogo wa ubunge ambako chama hicho kimemsimamisha Grace Tendega. 


Uchaguzi huo unafanyika kuziba nafasi ya Dk. William Mgimwa aliyefariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kloof Med-Clinic Pretoria Afrika Kusini, Januari mosi mwaka huu.

Slaa alisema kuwa Rais Kikwete akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa Februari 6, mwaka huu kabla ya kutangaza wajumbe 201 wa Bunge la Katiba, alisisitiza umuhimu wa kila mjumbe kutanguliza maslahi ya taifa wakati wa mjadala wao kuhusu katiba mpya badala ya kujali vyama vyao, makundi wanayotoka na utashi binafsi.


Slaa alisema kuwa hata hivyo, inashangaza kuona kuwa hivi sasa, CCM inayoongozwa na Rais Kikwete inatenda kinyume cha maelekezo hayo kwa kutanguliza maslahi ya chama chao badala ya taifa, tena kwa kuibua mipango hiyo katika vikao vyao.

Slaa alitoa mfano kuwa hivi karibuni, CCM iliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba wanaoiunga mkono CCM kuhakikisha kuwa wanatetea msimamo wa chama chao katika muundo wa serikali ya muungano ambao ni wa kuwa na serikali mbili na siyo tatu kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya pili ya katiba hiyo. 


Aidha, alizungumzia pia waraka aliodai kuwa ni wa siri wa CCM unaoelekeza namna katiba mpya inavyopaswa kuwa na kisha kutaka kuusambaza (waraka huo) kwa wajumbe wanaoiunga mkono CCM; mambo ambayo amedai hayaashirii hata kidogo utekelezaji wa kile alichokiasa Rais Kikwete hadharani wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa.

Slaa alisema Chadema imeuona waraka wa siri ambao ulipelekwa kwa Kamati Kuu (CC) kupata baraka ili utumike kama mwongozo katika kubadili baadhi ya mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya na tena ulipangwa kusambazwa kwa wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba wanaoiunga mkono CCM.


"Tunataka ufafanuzi kuhusiana na waraka huo ambao ulipelekwa kwenye kamati Kuu (ya CCM) iliyokaa siku chache zilizopita. Chadema hatukubaliani na hili la kuipinga rasimu ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba kwa kuwa yaliyomo katika rasimu hiyo ni mawazo ya Watanzania," alisema Dk. Slaa.


Alisema asilimia 60 ya Watanzania wameridhia mambo yaliyomo katika rasimu ya pili ya katiba na kwamba kuyachakachua kutokana na hila za kisiasa ni kufifisha fikra na mitazamo ya Watanzania kuhusu wanachokitaka katika miaka 50 ijayo.

Alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu, alisema kuwa hayo ni masuala ya CCM na hivyo ofisi yake haiwezi kuyatolea maelezo. 
 

“Suala la waraka unaodaiwa kuwa wa CCM waulize CCM wenyewe...siyo Ikulu,” alisema.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa juzi akiukana waraka huo wenye kurasa 22 unaodaiwa kutoa maelekezo juu ya namna wajumbe wanaoiunga mkono CCM wanavyopaswa kutoa mapendekezo yao katika maeneo muhimu yanayogusa ustawi wake kwenye kila ibara, ikiwamo inayozungumzia muundo wa Muungano.

ASASI DRC ZATAKA AL BASHIRI AKAMATWE

 
 

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, yamesema kuwa Serikali ya nchi hiyo itachukuliwa kuwa dhaifu iwapo hawamkamati Rais wa Sudan, Omar el Bashir.

Mashirika yapatayo 90 yalitoa wito Serikali ya DRC imkamate el Bashir ambaye alikuwa mjini Kinshasa kushiriki katika vikao vya muungano wa COMESA.

Mmoja wa waandalizi wa maandamano ya kushinikiza Serikali imkamate kiongozi huyo wa Khartoum, Bwana Andre Kito Masimango, amesema:
"kuna barua ambayo inasema kuwa mahali po pote ambapo El Bashiri anapatikana anapaswa kukamatwa na kupelekwa kwenye mahakama ya kimataifa."

Mkerektwa huyo wa haki za kibinadamu anasema kuwa Rais El Bashir anapaswa kukamatwa kwa heshina ya waathirika wa dhuluma inayodaiwa kufanywa nchini Sudan na hata DRC yenyewe.

Watu kadhaa ambao wametoa maoni kwenye mtandao wa BBC wamesema kuwa lilikuwa kosa kwa Serikali ya DRC kumkaribisha Rais El Bashar kwa mkutano wa COMESA huku ikijua kuwa anatafutwa.

Hata hivyo kuna wale wanaosema kuwa msimamo wa Umoja wa Afrika (AU) ambao unasema kiongozi anayetawala hapaswi kukamatwa unapaswa kuzingatiwa ili El Bashir asikamatwe ugenini DRC.

MAREKANI YAIONYA URUSI KUHUSU UKRAINE


Hatua hii inawadia siku moja tu baada ya Urusi kuamuru kufanyika kwa mazoezi ya kijeshi yanayoshirikisha askari wapiganaji laki moja na nusu kwenye mpaka wake na Ukraine .

Kujitokeza kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine kumeimarisha uhasama ulioko kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry amesema kuwa Urusi inapaswa kukubali ushauri ya kwamba mataifa ya kigeni yasiingile mambo ya ndani ya Ukraine.
Alisema kuwa kujiingiza kijeshi katika hali ilivyo nchini Ukraine kwa hivi sasa ni kosa kubwa.

Mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya muungano wa NATO wametoa taarifa ambapo wamesema kuwa wanachama wake wataendelea kuunga mkono uhuru na hadhi ya taifa la Ukraine.

Serikali ya Marekani imesema kuwa imetenga mbinu mbalimbali inazotazamia kutumia kuimarisha Ukraine kiuchumi, huku kukiendelea kuwa na hofu kuwa huenda taifa hilo likashindwa kuendelea kulipa madeni yake.

Kwa wakati huu msaada wa kijeshi pekee kwa Ukraine hautoshi kwani taifa linalotaka kusaidia lazima kwanza liimarishe hali ya kukubaliwa kwake katika taifa hili ambalo limegawanyika kwa imani yake kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.

Wabunge kadhaa wa Marekani wameonya kuwa Jumuiya ya Ulaya na Marekani wasipotoa msaada wa pesa taslimu Urusi huenda ikafanya hivyo.

 BAADA YA MAMBO KUMWENDEA VIBAYA CHENGE NGUVU YAHAMIA KWA MIGIRO


Kampeni  za makundi ya vigogo wanaopigana vikumbo kugombea uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba zimechukua sura mpya, baada ya kundi lililokuwa likimuunga mkono Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kudaiwa kubadili ghafla mwelekeo wa kampeni zake.


 Habari za kuaminika zilizopatikana mjini hapa jana zilieleza kuwa kundi hilo lililokuwa likimtaka Chenge, sasa linataka nafasi hiyo iwaniwe na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro au Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.

 Hatua hiyo inadaiwa kuchukuliwa na kundi hilo baada ya kubaini kuongezeka kila uchao kwa nguvu za Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye tayari ameshatangaza kuwania nafasi hiyo, huku zile walizozitarajia kutoka kwa Chenge zikizidi kushuka.


 Habari hizo zinaeleza kuwa uthibitisho wa hilo, ni ujasiri ulioonyeshwa na Sitta aliyeamua kutangaza hadharani azma yake ya kuwania nafasi hiyo, huku Chenge akishindwa kuthibitisha kuwa atagombea ama la.


Uchaguzi wa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba unatarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii baada ya Bunge hilo kupitisha azimio la kuipitisha rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu kesho.


Awali, Chenge aliiambia NIPASHE kuwa hayuko tayari kutangaza kama atagombea nafasi hiyo au la kwa kuwa kanuni za Bunge hilo bado hazijatungwa.


Kauli kama hiyo iliwahi pia kutolewa na Waziri Sitta katika siku hiyo hiyo, ambayo Chenge aliashiria kusubiri kanuni.


Hata hivyo, siku chache baadaye, hata kabla ya rasimu ya kanuni hizo haijapitishwa na Bunge, Waziri Sitta alitangaza azma yake ya kugombea nafasi hiyo kwa maelezo kwamba, anataka kutimiza ndoto ya Rais Jakaya Kikwete ya kupata katiba bora.


Jumatatu wiki hii, Chenge alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana kinyang'anyiro hicho, alikataa kuzungumza na badala yake akamtaka mwandishi aendelee na shughuli zake.


Waziri Chikawe alipotafutwa na NIPASHE jana kuzungumza kama ana nia ya kugombea nafasi hiyo au la, alimtaka mwandishi kuvuta subira kwa kuwa wakati huo hakuwa na nafasi ya kuzungumza.


Dk. Migiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN) hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Jitihada za kuwatafuta viongozi hao wanaotajwa kuwania nafasi hiyo zinaendelea.

Wednesday 26 February 2014

POSHO BUNGE LA KATIBA KUSHUSHA HADHI YA WABUNGE

 PROF LIPUMBA ASEMA:"POSHO IMESHUSHA HADHI YA WABUNGE"


 Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema suala la madai ya nyongeza ya posho ya Sh. 300,000 wanayolipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa siku, limepewa taswira mbaya na wananchi na kushusha hadhi ya Bunge kutokana na kukuzwa na vyombo vya habari.


 Alisema jambo la kanuni za Bunge Maalumu ndilo lililokuwa la msingi, lakini ghafla likazuka hilo la posho likapewa uzito mkubwa na vyombo vya habari, ambao haukustahili, kwa kuwa halikuwa ajenda ya Bunge.

Alisema kwanza malalamiko ya kudai nyongeza ya posho hayakutolewa na mjumbe yeyote kati ya wale 201 walioteuliwa na Rais.


Alisema hawakulalamika kwa kuwa anaamini kuwa Sh. 300,000 wanazolipwa ni fedha, ambayo inatosha kumwezesha mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu la Katiba kuishi mjini Dodoma na kufanya kazi za Bunge na siyo fedha za kuanzia mtaji wa maisha.

“Hivyo, suala la posho limepunguza hadhi ya Bunge, kwa sababu limepewa uzito na vyombo vya habari tofauti na lilivyowasilishwa,” alisema Profesa Lipumba.


Kadhalika, alisema  moja ya matatizo yanayowakabili wajumbe wa Bunge hilo ni kutokuwa na mafunzo kuhusu wajibu na kazi za Bunge.


 Alisema Bunge lilitakiwa kuandaa mapema kanuni kwa kuwa jambo hilo ni la msingi kwa sababu kanuni ndiyo mwongozo wa namna ya kuendesha Bunge.


“Pamoja na kutupa rasimu ya katiba, wangetupa pia na rasimu ya kanuni za Bunge iliyoandaliwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Lakini ikachelewa,” alisema Profesa Lipumba.


Aliongeza: “Kanuni ni suala la msingi. Tumechelewa (kuanza kuijadili rasimu ya katiba) kwa sababu hatujakamilisha (kuipitisha rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu). Hilo halikutazamwa vizuri namna ya kuandaa mapema.”

KENYA YAPELEKA WANAJESHI SUDANI KUSINI


Kamati Kuu ya Usalama Nchini Kenya imependekeza kwa bunge liidhinishe nyongeza ya idadi ya wanajeshi wake wa kudumisha amani walioko nchini Sudan Kusini, chini ya kivuli cha Umoja wa Mataifa, kwa majeshi 310.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Rais Uhuru Kenyatta imesema imechukua hatua hiyo kufuatia ombi la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lililofanywa Desemba 24, mwaka jana.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa ikulu ya Nairobi usiku wa kuamkia leo, kamati hiyo ambayo imekutana kwa mara ya kwanza tangu Rais Uhuru Kenyatta kuanza utawala wake mwaka mmoja uliopita ilisema kuwa Kenya itawatoa wanajeshi wengine ili kufanya idadi ya wanajeshi wake walioko Sudan Kusini kufikia 1,000.
Taarifa hiyo ilieleza wazi kuwa wanajeshi wa Kenya wanaingia huko chini ya Umoja wa Kimataifa na wala sio kama taifa huru.

Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kuanza kati ya jeshi la Sudan Kusini linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanajeshi waasi wanaomuunga mkono makamu wa rais wa zamani Daktari Riek Machar, Uganda iliwatuma wanajeshi nchini humo kuunga mkono Rais Salva Kiir.
Katika taarifa hiyo kamati ya usalama nchini Kenya ilisema kuwa hali ya usalama nchini Sudan Kusini imeathiri Kenya.

Wakimbizi wengi wametorokea Kenya, taifa ambalo kwa hivi sasa linakabiliwa na matatizo yake mengi ya kiuslama kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wa Somalia .
Miongoni mwa matatizo ya kiusalama yaliyotajwa katika taarifa hiyo ni mapigano kati ya makabila mbalimbali nchini Kenya na pia hatari ya mashambulizi ya kigaidi katika uwanja wake wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Mkutano huo wa usalama ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ulisema usalama katika uwanja huo utaimarishwa kwa kuimarisha mitambo ya kuwapekua wasafiri wa kimataifa.
Nairobi ni kitovu kikubwa cha usafiri kwa watalii na wafanyabiashara katika eneo zima la ukanda wa mashariki na upembe wa Afrika.

Rais Uhuru Kenyatta hii leo atasafiri hadi mji Mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kama hatua mojawapo ya viongozi wa eneo la Afrika Mashariki la kutafuta suluhu la mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.

 CHADEMA YATAKA POSHO ZA WABUNGE ZIKATWE KODI


 Mkurugenzi wa bunge na halmashauri John Mrema

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshangazwa na uamuzi wa serikali wa kuwalipa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba posho ya Sh. milioni tisa kwa mwezi, huku ikiacha kuwatoza Kodi ya Mapato (Paye) kutoka katika fedha hizo, kinyume cha sheria za nchi.

 Pia kimewashangaa wajumbe hao, ambao ni watunga sheria mama ya nchi (katiba) kuwa wavunjifu wa sheria ya kodi kwa kutolipa kodi.

 Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chama hicho, John Mrema, alisema:

“Haiwezekani (wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba) walipwe milioni tisa kwa mwezi bila kukatwa kodi wakati mwalimu analipwa 298,000 kwa mwezi na anakatwa kodi.”

Alisema daima katiba ya nchi hutakiwa kutungwa na wazalendo na kwamba, kipimo kimojawapo cha uzalendo ni pamoja na kulipa kodi ili kutekeleza sheria za nchi bila shuruti na kuwataka wajumbe wote wa Bunge hilo kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria.

 
Pia aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi ya mapato kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Haiwezekani watunga sheria mama wawe wavunjifu wa sheria ya kodi. Hiyo katiba wanamtungia nani akaitekeleze kama wao wenyewe siyo watiifu wa sheria za nchi?” alihoji Mrema.

Aliongeza: “Ni wakati sasa wa TRA kuonyesha kwa vitendo na siyo kuwaumiza wafanyabiashara wadogo na wafanyakazi kwa mashine zao za EFD, huku wanasiasa wakiachwa bila kodi.”
 

Tuesday 25 February 2014

KUTOKA UKRAINE

BUNGE LA UKRAINE KUJADILI SERIKALI MPYA

  


Maelfu ya waandamanaji wameendelea na maandamano katikati ya mji wa Kiev wakati Wabunge wakikutana kujadili kuhusu uundwaji wa Serikali mpya nchini Ukraine.

Hali katika viwanja vya uhuru imetulia, ikiwa ni siku moja baada ya Bunge kupiga kura kumuondoa Rais wa nchi hiyo, Viktor Yanukovych,hatua ambayo amedai kuwa ni mapinduzi huku mpaka sasa akiwa hajulikani alipo.

Mpinzani wake mkuu, Waziri mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko, pia aliachiwa huru toka kifungoni , hatua hii imekuja baada ya maandamano dhidi ya Serikali ya nchi hiyo yaliyodumu kwa miezi kadhaa.

Yulia tymoshenko alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela akishutumiwa kutumia vibaya madaraka yake, na kuachiwa kwake yalikua madai ya msingi ya waandamanaji nchini humo.

Wabunge wa upinzani wameiambia Televisheni ya taifa kuwa Bunge litajadili kuhusu uundwaji wa Baraza jipya la mawaziri na uteuzi wa Waziri mkuu.

 FAIDA ZA UYOGA MWILINI


 

Uyoga una vitamini na aina nyingi za madini. Virutubisho vilivyothibitishwa kuwemo kwenye uyoga ni pamoja na Vitamin B2, B3, B5, B6, B Complex pamoja na madini ya Potasiamu na ‘phosphorus’. Virutubisho hivyo ni muhimu kwenye mwili wa binadamu katika kutoa na kuimarisha kinga ya kupambana na ‘wavamizi’ maradhi.
 
Aidha, inaelezwa kuwa uyoga ni chanzo kingine kizuri sana cha madini ya chuma (iron) na kopa ambayo yanahusika kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wa usambaza wa hewa ya oksijeni mwilini. Kupatikana kwa madini ya chuma na kopa kwenye uyago ni jambo la kipekee ambalo linafanya mmea huo kuwa tofauti na muhimu.
 
Zikifafanuliwa nguvu za uyoga (Mashrooms) kwa mapana, inaelezwa kuwa Vitamin B2 inayopatikana kwenye uyoga, ni tiba tosha kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kichwa unaojulikana kama ‘kipanda uso’. Kiasi kidogo cha uyoga utakachokula kitapunguza kasi ya kuumwa kichwa hicho.
 
Vilevile Vitamin B inasifika kwa uwezo wake wa kuzuia uchovu wa mwili (fatique) na akili hasa wakati wa kazi nyingi. Vitamin B3 husaidia kupunguza kiwango cha mafuta mabaya ya Kolestrol mwilini, wakati Vitamin B6 yenyewe huondoa hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au moyo kusimama ghafla (Heart Attack).
 
Kama faida zote za kiafya zilizo orodheshwa hapo juu zinazopatikana kwenye uyoga hazikutosha, basi kuna faida nyingine ambayo inatokana na madini aina ya Zinc yanayopatikana kwa wingi kwenye mboga hii. Zinc ina faida nyingi sana mwilini na miongoni mwa faida hizo ni uimarishaji wa kinga ya mwili (Immune System).
 
Zinc si muhimu tu kwa uimarishaji wa kinga mwilini, bali pia kwa uponyaji wa haraka wa vidonda mwilini. Vilevile mboga hii inasaidia sana ukuaji mzuri wa seli za mwili, huimarisha kiwango cha sukari mwilini na kukufanya kusikia ladha na harufu ya vyakula na vitu vingine ipasavyo.
 
Kwa ujumla uyoga ni mboga muhimu na inapaswa kuliwa na kila mtu anayejali afya yake kutokana na faida zinazopatikana humo. Kuanzia leo, jaribu kuweka uyoga katika orodha ya mboga unazonunua kila wiki kwa ajili ya familia yako.
 
Bila shaka kwa wakazi wa miji midogo na vijijini, mboga hii hupatikana kwa wingi wakati wa mvua na kwa miji mikubwa kama Dar es Salaam, uyoga unaweza kupatikana kwenye masoko maalum kama, Kariakoo, Kisutu na ‘super market’ mbalimbali.

BUNGE LA KATIBA:WABUNGE WACHUKUA TSH MILIONI 129 KWENYE KIKAO

 

Wakati Bunge Maalum la Katiba likikutana kwa takribani nusu saa tu jana huku wajumbe wakiendelea kulipwa mamilioni ya fedha za kodi za wananchi, baadhi ya wajumbe wa wamelalamika na kupinga hali ya kuendelea kuahirisha vikao kwa kuwa hatua hiyo inasababisha matumizi makubwa ya fedha za umma na muda.

Bunge hilo limekuwa likiahirishwa tangu kuanza Jumanne iliyopita kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wajumbe kuzisoma kanuni pamoja na Kamati ya Kanuni kukamilisha kazi ya kuzichambua na kuwasilisha mbele ya wajumbe hao kwa ajili ya kuzijadili na kuzipitisha, kabla ya kuanza kujadili Rasimu ya Katiba.

Wajumbe hao walitoa madai hayo jana baada ya kikao hicho kufanyika kwa nusu saa na kuhairishwa wakidai kuwa huko ni kupoteza muda na rasilimali za Watanzania  bila sababu ya msingi.

Jana wajumbe takribani 629 waliokwisharipoti waliingia katika kikao kilichodumu kwa nusu saa kuanzia saa 3:00 asuhuhi hadi saa 3:30 na kuahirishwa. Kutokana na kila mjumbe kulipwa posho ya kikao ya Sh. 220,000 kwa siku, jana kwa dakika 30 zilitumika takribani Sh. 128,920,000 zilitumika kuwalipa wajumbe hao.

Baada ya Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Ameir Pandu Kificho, kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Ezekia Oluoch kutoka Vyama vya Wafanyakazi, alishauri siku mbili ambazo kamati itakuwa inaendelea na
kazi ya kuchambua kanuni, wajumbe waendelee na kazi ya kuijadili Rasimu ya Kanuni na maoni yapelekwe kwenye Kamati.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi bunge, Oluoch alisema
anashangazwa na uamuzi huo kwa kuwa unapoteza rasilimali na muda kwa kuwa tangu bunge hilo lianze Februari 18 mwaka huu hakuna jambo la msingi lililofanyika.

“Tungeambiwa hivi wala tusingewahi asubuhi, sasa tunaambiwa hadi Jumatano, siku zote hizi mbili tunafanya nini hapa Dodoma, ni matumizi
mabaya ya muda na rasilimali za Watanzania ambao ndiyo wanatulipa tunavyokuwa hapa,” alisisitiza.

Profesa Sospeter Muhongo alisema anashangaa kazi hiyo kushindwa kukamilika kwa siku hizo wakati walikuwa na mwongozo wa Rasimu ya Kanuni.

“Tusipokuwa waangalifu kuzingatia muda hii kazi haitaisha, kwa hiyo tukubaliane kwamba muda uliopangwa ukimalizika hakuna muda wa nyongeza kwa maelezo kwamba hawajamaliza, wananchi wanavyotuona tunaweza kujifurahisa tunafanya vitu vya maana sana, lakini watu wanatushangaa, kama kamati haiwezi unaitoa tunaendelea mbele,” alisema Profesa Muhongo ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Waziri wa Nishati na Madini.

Mjumbe mwingine, James Mbatia, alisema kanuni hizo ni ngumu na zimetengenezwa kama kanuni za kudumu za Bunge, jambo ambalo litawafanya wajumbe wengine washindwe kuzitumia.

“Fikiria mvuvi wa Muleba au Mwanza au mkulima ambaye hana uzoefu na mambo ya kibunge, hizi kanuni zinavyotengenezwa ni ngumu inaonyesha zinanakiliwa na kubandikwa wakifuata zile Kanuni za Kudumu za Bunge,” alisema na kuongeza:“Huu ni mkutano wa siku 70 na si bunge la kudumu. Zingepaswa ziwe kwenye karatasi mbili au tatu kwa kuwa tupo hapa kwa tendo la Katiba ambalo ni maridhiano.”

Alisema wabunge waliozizoea kanuni na ukumbi huo bado zinawasumbua, kwa mtu ambaye amekuja mara ya kwanza anawekewa masharti ya uvaaji ikiwamo kuvaa suti na kwamba tatizo kubwa lipo kwenye muundo wa Bunge lenyewe kwa kuwa wengi wa wajumbe wanatokana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Alisema Katiba si kwa ajili ya kizazi hiki bali vizazi vya miaka 100 ijayo, na kwamba mambo yanakuwa magumu kwa kuwa yanazungumzwa masuala ya nchi mbili kwa wakati moja.

Alisema mkutano huo ni wa siku 70 na ni sawa na mkutano wa kawaida, hivyo huwezi kutengeneza kanuni kama kanuni za kudumu kama mtu anayeandaa kanuni zitakazotumika kwa miaka 20 ijayo.

“Ni kanuni ngumu sana na zinachanganya, wanasahau kuwa Katiba ni suala la maridhiano, Bunge la Nepal lilitumia siku 90 kutengeneza Kanuni. Ukishakosea kwenye kanuni ndiyo basi, hizi zilitengenezwa na sekretarieti ambazo siyo wajumbe wa Bunge, zinapaswa kutokana nawajumbe wenyewe iwe ya kurasa mbili au tatu,” alisema.

Alisema kwa mwendo huo haoni dalili za Bunge hilo kuanza wiki hii wala ijayo na kwamba Watanzania wasikubali kuondoshwa kwenye hoja ya msingi na kupelekwa kwenye suala la posho.

Aidha, alikosoa kanuni hizo na kudai kuwa zimetengenezwa kwa hofu ya watawala na kwamba kuweka kanuni ya kumtoa nje mjumbe kwa siku kumi kwa Bunge la siku 70 ni ajenda isiyo na lengo jema.

Ally Kessy, ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), alisema kuahirishwa kwa vikao vya bunge tangu wiki iliyopita kwa madai kwamba wajumbe wanahitaji muda wa kutosha kusoma Rasimu hiyo ni kupoteza bure fedha za wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema haoni sababu ya bunge hilo kuahirisha vikao kwa hoja ya kutoa muda wa kutosha kwa wabunge kusoma vya Rasimu ya Kanuni.

“Haina sababu, busara inakosekana, Mwenyekiti wa Muda alikwishaunda kamati ya wajumbe 20 ya kumshauri, kwa nini sasa hali hii inaendelea kuwa hivi?” alihoji.

Alisema kwa upande wake ameisoma Rasimu hiyo kwa siku mbili tu na kuielewa, hivyo haoni kwa nini wajumbe wahitaji siku nyingi kuisoma na kuielewa.

Naye Mjumbe kutoka kundi la Vyama vya Wavuvi Zanzibar, Issa Ameir Suleiman, alisema: “Sisi tunaona hawatundei haki, lengo letu lilikuwa kuja na kufanya kazi moja kwa moja, lakini sasa tunaingia wiki ya pili bado hatujaanza kujadili Rasimu ya Katiba.”

Halima Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema maadalizi mabovu ya bunge hilo ndicho kilichosababisha mambo mengi kwenda kinyume cha matarajio yao.

Alisema kutokana na kazi kubwa na umuhimu wa kupitia kanuni na kuzichambua kwa kina kukosa maandalizi ndiyo sababu ya bunge hilo kushindwa kufanya kazi yake kwa wakati.

“Maandalizi ya kuchambua Rasimu ya Kanuni ni kazi kubwa na ilitakiwa kanuni zipitiwe mapema na kuchambuliwa kwa kina, lakini kutokana na kutokuwapo kwa maandalizi ya kutosha ndiko kunakozalisha ucheleweshwaji na utendaji kazi wa ovyo.

“Mimi siitetei kamati ambayo ilitakiwa kupitia kanuni, lakini kimsingi kanuni ni muhimu sana kuingia katika mjadala wa Katiba na kama kanuni itakuwa mbovu, ni wazi kuwa katiba nayo itakuwa mbovu na kanuni ikiwa nzuri ni wazi kuwa Katiba itakuwa nzuri kwa maana kanuni ndizo zinatoa mwongozo wa mjadala wa Katiba,” alisema.

  “Nina shaka kama kweli makundi ambayo yamekuja katika bunge yamekuja kwa ajili ya kuboresha Rasimu ya pili ya Katiba au wamekuja kwa ajili ya kupinga maoni ya Watanzania zaidi ya milioni 45 ambao walitoa maoni yao,” alisema na kuongeza:

 “Kanuni zimekuja na vipengele mbalimbali ambavyo vinatoa nguvu nyingi kwa Bunge kuliko Sheria kwa maana ya kutaka kuondoa maneno au mapendekezo ya Rasimu ya pili na kuweka mapendekezo mapya, jambo ambalo litakuwa ni kutowatendea haki Watanzania.