MEMBE AIPONGEZA CCM
Siku mbili baada ya makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupewa
adhabu ya onyo na kuzuiwa kugombea nafasi za uongozi kwa mwaka mmoja,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
amefunguka na kupongeza uamuzi huo uliofanywa na Kamati Kuu (CCM) ya
chama hicho.
Membe ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu yaTaifa (Nec) ya CCM, ni miongoni mwa makada hao walioadhibiwa kwa tuhuma za kuanza kampeni za kutaka wateuliwe na chama chao kugombea urais wa mwaka 2015 pamoja na kukiuka taratibu na kanuni za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Membe aliupongeza uamuzi huo na kueleza kuwa ni wa lazima kwa kuwa unajenga nidhamu ndani ya Chama.
Makada wengine waliothibikika kukiuka kanuni na taratibu hizo ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Membe alisema adhabu iliyotolewa na CCM ni taratibu za kawaida na za lazima ambazo zinapaswa kuigwa na vyama vingine.
Alisema dunia imekuwa ikiiga matendo na kanuni za maisha ya waumini wa Kanisa Katoliki, lakini wameshindwa kuiga namna wanavyofanya uchaguzi wa kumteua mkuu wa kanisa hilo Baba Mtakatifu, kwa utulivu na amani, hivyo kubaki kufanya chaguzi za fujo na vurugu.
“Hakuna yeyote duniani aliyeiga kanuni na taratibu za Waroma wanavyompata Papa wa kuliongoza kanisa, hivyo kila chama kina wajibu wa kuweka taratibu na kanuni kwa wagombea wake ili nidhamu iwepo ndani ya Chama, ili taratibu na kanuni zisipofuatwa hatua zichukuliwe,” alisema Membe.
Alisema kuwa msimamo wa CCM wa kuwadhibiti kutokana na kuona kuwa taratibu na kanuni zilizowekwa na chama hicho zinakiukwa ni mzuri, na kwamba kama kuna chama hakifanyi hivyo, hakuna faida ya kuendelea kuwapo.
“Utaratibu huu ni mzuri na wa kawaida na ni wa lazima, hauwezi kukwepwa kwa waliooteshwa na wasiyooteshwa kuwa viongozi,” alisema Membe.
CCM kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Jumanne wiki hii, alitangamza msimamo wa CCM wa kuwapa onyo kali makada hao kwa kosa la kubainika kufanya kampeni kabla ya wakati na kuvunja kanuni na taratibu za chama hicho.
Nape alisema msimamo huo ulifuatia vikao vyake kuanzia Februari 13 hadi
18, mwaka huu mjini Dodoma, kujadili masuala mbalimbali likiwamo la
makada hao ambao wote walihojiwa na Kamati ya Maadili kabla ya kupatiwa
adhabu hiyo.
“Makada hawa watakuwa na wakati mgumu kwani hawataruhusiwa kujihusisha
na aina yeyote ya siasa, hivyo kama watajihusisha kanuni na taratibu
hazitamruhusu kugombea nafasi yeyote ya uongozi ndani ya Chama, kwa hiyo
tunaweza kusema wako kwenye ‘Danger Zone,’ alisema Nape.
Alisema pia chama hicho kimetangaza kuwaita na kuwahoji wapambe na mawakala wote wanaoshirikiana na makada waliopewa onyo na wengine ambao hawajabainika kufanya kampeni za chini chini ili kuwachukulia hatua stahiki.
Nape alisema Kamati ya Maadili inaendelea kuwachunguza na kuwafuatilia
kwa makini na baadaye watawaita ili kuwapatia adhabu kutokana na utovu
huo wa nidhamu unaokichafua Chama na jamii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment