ULAYA YASEMA " WANAOZUA VURUGU UKRAIN WATABANWA"
Umoja wa Ulaya umekubali kuwawekea vikwazo watu waliohusika katika kuzua vurugu zinazoikabili Ukraine kwa sasa.
Uamuzi huo uliofanyika mjini Brussels, umejiri
baada ya makumi kadhaa ya watu kuuwawa mjini Kiev, katika siku ambayo
ilishuhudia umwagikaji mkubwa zaidi wa damu nchini Ukraine tangu uhuru
zaidi ya miaka ishirini iliyopita.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni
wa Italia, Emma Bonino, amesema vikwazo hivyo vinavyojumuisha vikwazo
vya usafiri na kupiga tanji mali za wahusika, vitawalenga wale
waliohusika na mauaji ya waandamanaji.
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kiev unajaribu
kuwapatanisha viongozi wa upinzani na rais Victor Yanukovych ili kuleta
amani na pia kushawishi taifa hilo kuandaa mapema uchaguzi uliopangiwa
kufanyika mwaka ujao.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa , Ban Ki-moon amesema hali nchini Ukraine ni ya kutamausha.
" Nasikitishwa sana na jinsi mambo yalivyogeuka
na kuwa mkasa nchini Ukraine hususan hapo jana ambapo zaidi ya watu mia
moja waliuwawa na vurugu hizi zilizozuka upya," amesema bwana Ban.
Bwana Ban ametowa wito kwa pande zote kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
"Naendelea kutoa wito kwa wato wanaohusika
kukomesha vurugu na kwa mamlaka za ukraine kujiepusha na matumizi ya
nguvu kupita kiasi. Nimetamaushwa sana na visa vya matumizi ya silaha
miongoni mwa polisi na waandamanaji. Natoa wito kwa pande zote mbili
kurejea mara moja katika mazungumzo ya dhati, hii ndio njia ya pekee ya
kukomesha umwagikaji wa damu na kufikia suluhu juu ya mzozo wa kiasi,
kiusalama na kiuchumi unaozidi kukithiri."
Wito huo umetolewa vile vile na waziri wa
mashauri ya nchi za kigeni wa marekani John Kerry ambaye ametaka vurugu
kusitishwa nchini Ukraine kukomeshwa akisema kuwa watu wa taifa hilo
wanastahili kuwa na hali bora kuliko kile alichokitaja kuwa maafa na
mateso yasiyofaa ambayo yameshuhudiwa katika barabara za mji mkuu mkuu
wa Kiev.
Haijabainika ni watu wangapi waliouwawa katika
vurugu za Alhamisi lakini wizara ya Afya inasema tangu Jumanne, watu
sabini wamuewawa na zaidi ya 570 wamejeruhiwa.
No comments:
Post a Comment