PROF LIPUMBA ASEMA:"POSHO IMESHUSHA HADHI YA WABUNGE"
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema suala
la madai ya nyongeza ya posho ya Sh. 300,000 wanayolipwa wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kwa siku, limepewa taswira mbaya na wananchi na
kushusha hadhi ya Bunge kutokana na kukuzwa na vyombo vya habari.
Alisema jambo la kanuni za Bunge Maalumu ndilo lililokuwa la msingi, lakini ghafla likazuka hilo la posho likapewa uzito mkubwa na vyombo vya habari, ambao haukustahili, kwa kuwa halikuwa ajenda ya Bunge.
Alisema kwanza malalamiko ya kudai nyongeza ya posho hayakutolewa na mjumbe yeyote kati ya wale 201 walioteuliwa na Rais.
Alisema hawakulalamika kwa kuwa anaamini kuwa Sh. 300,000 wanazolipwa ni fedha, ambayo inatosha kumwezesha mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu la Katiba kuishi mjini Dodoma na kufanya kazi za Bunge na siyo fedha za kuanzia mtaji wa maisha.
“Hivyo, suala la posho limepunguza hadhi ya Bunge, kwa sababu limepewa uzito na vyombo vya habari tofauti na lilivyowasilishwa,” alisema Profesa Lipumba.
Kadhalika, alisema moja ya matatizo yanayowakabili wajumbe wa Bunge hilo ni kutokuwa na mafunzo kuhusu wajibu na kazi za Bunge.
Alisema Bunge lilitakiwa kuandaa mapema kanuni kwa kuwa jambo hilo ni la msingi kwa sababu kanuni ndiyo mwongozo wa namna ya kuendesha Bunge.
“Pamoja na kutupa rasimu ya katiba, wangetupa pia na rasimu ya kanuni za Bunge iliyoandaliwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Lakini ikachelewa,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “Kanuni ni suala la msingi. Tumechelewa (kuanza kuijadili rasimu ya katiba) kwa sababu hatujakamilisha (kuipitisha rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu). Hilo halikutazamwa vizuri namna ya kuandaa mapema.”
No comments:
Post a Comment