Thursday, 20 February 2014

 WAJUMBE 20 KUANDAA KANUNI ZA BUNGE LA KATIBA

 http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2013/07/mr-pandu-ameir-kificho.jpg

Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, Ameir Pandu Kificho,ameunda kamati ya wajumbe  20, watakaokuwa na jukumu la kumsaidia kutengeneza kanuni na kumshauri.

Akizungumza wakati wa kuahirisha semina kwa wajumbe hao juu ya rasimu ya kanuni za Bunge Maalum, Kificho alisema kamati hiyo itakuwa na jukumu la kumshauri na kuandika nukuu mbalimbali za majadiliano ya wajumbe na kutoa ufafanuzi wa vifungu mbalimbali.

Wajumbe walioteuliwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, Tundu Lissu,Abubakari Khamis Bakari (Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar), Othman Masod Othuman, Mgeni Hassani Juma, Ussi Jecha Simae, Ismail Jusa, Dk. Tulia Akison.

Wengine ni Prof. Abdul Sheriff, Magdalena Rwebangira, Evold Mmanda, Amon Mpanjo, Prof. Costa Mahalu, Honoratha Chitanda, Nakazaeli Tenga, Elizabeth Minde, George Simbachawene, Adila Hilary Vuai na Peter Kuga Mziray.

RASIMU YA KANUNI KUWASILISHWA LEO
Wakati huo huo, Kanuni za Bunge na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vinatarajiwa kuwasilishwa mbele ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba leo.

Kificho aliwaeleza wajumbe hao jana kuwa zoezi la kuwasilisha rasimu na sheria hiyo lilitakiwa kufanyika jana, lakini kutokana na muda kuwa mfupi litafanyika kesho.

Alisema pamoja na kuwasilisha, elimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba itatolewa kwa wajumbe hao na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Zoezi la kugawa rasimu hizo lilichukua muda mrefu kutokana na baadhi ya wajumbe kudaiwa kuchukua nakala zaidi ya moja na wengine kukosa.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alisema nakala 600 zilitengenezwa na wajumbe waliopo ndani ya ukumbi huo hawafiki idadi hiyo, jambo linaloonyesha wapo waliochukua zaidi ya moja.

Kupunguza kwa nakala hizo kulizua mjadala kukiwa na mapendekezo tofauti kwa baadhi ya wajumbe wakitaka mjadala uendelee huku nakala nyingi zikitengenezwa na wengine walikataa.

Mjumbe Moses Machali, alisema si busara kwa sheria ya mabadiliko ya Katiba iliyotungwa na Bunge kuwasilishwa kwenye Bunge hilo ambalo halina mamlaka kisherai kuongeza au kupunguza.

Mjumbe John Mnyika, alisema kwa kuwa Katiba inayotungwa ni kwa ajili ya Watanzania, hivyo ni vyema kanuni hizo zikafikishwa kwa wadau ili wazijadili na kutoa mapendekezo, hoja iliyopigwa na wajumbe hao.

Alisema ni muda wa kujadili rasimu hiyo uwe wa siku tatu ili kutoa nafasi wajumbe kupitia kifungu hadi kifungu na kumaliza vifungu 113 vilivyopo.

Aidha, kwa muda wa zaidi ya nusu saa ndani ya ukumbi huo kuligubikwa na kelele za kila mmoja kutaka kuongea na kushindwa kumsikiliza mwenyekiti.

Kadhalika, palizuka mvutano wa siku za kupitia na kusoma rasimu na sheria hiyo kwa wajumbe, huku  Mjumbe Tundu Lissu akitaka zitolewe siku tano za kusoma na tatu za kujadili.

Naye Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahaya Khamis Hamad, alisimama na kusema kuwa baadhi ya wajumbe walizungumza na kukubaliana kabla ya kuingia kwenye kikao hicho na kukubaliana siku za majadiliano na kusoma.

Wakati akieleza hivyo, baadhi ya wajumbe walilipuka kwa kelele wakisema ‘Katibu unaleta siasa’ hali iliyomfanya Dk. Kashillilah kunyamaza.

Kificho alitangaza utaratibu kuwa rasimu na sheria hiyo zitawasilishwa na kutoa nafasi kwa wajumbe kusoma na kujadili hadi Jumatatu itakapoanza kujadiliwa.

Alisema leo ratiba ya semina hizo zitatolewa kwa wajumbe na kwamba siku za majadiliano zitajulikana kwa kadri kazi itakapoanza na kujua siku ya Rais atazindua Bunge hilo.

Mwenyekiti huyo alisema Ofisi ya Bunge imezingatia mahitaji ya makundi yote ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa maandishi ya vinundu kwa watu wenye ulemavu wa kuona.
 

No comments:

Post a Comment