TFF YAVUNJA MKATABA NA KOCHA WAKE
Hatimaye Shirikisho la Kabumbu nchini Tanzania TFF
limetangaza kuvunja mkataba wake na Kocha mkuu wa Timu ya taifa ya soka
ya Tanzania Taifa Stars Kim Poulsen kwa kile kilichoelezwa maafikiano ya
pamoja baina ya kocha huyo,TFF, na Serikali.
Jamal Malinzi ambaye ni Rais wa Shirikisho la
soka Tanzania amesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida hasa baada ya
wadau mbali mbali kuona kuwa huu ni wakati wa kufanya mabadiliko ya
lazima katika benchi la ufundi la Taifa Stars ambayo inajiandaa kwa
mechi za kufuzu kwa Fainali za kombe la mataifa Afrika hapo mwakani
zitakazofanyika nchini Morocco.
Kuhusu gharama za kuvunja mkataba na
Kocha huyo Bwana Malinzi amesema serikali haitagharamia uvunjaji huo wa
mkataba na kocha huyo na badala yake wapo wadau waliojitokeza
kugharamia kutokana na kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko katika
kipindi hiki kwa faida ya soka la Tanzania.
Kwa Upande wake Kocha Kim Poulsen amesema na
rekodi yake inaonyesha kuimarika kwa soka la Tanzania katika kipindi cha
takriban miaka miwili aliyokuwa akikinoa kikosi cha Taifa Stars lakini
kusitishwa mkataba ni jambo la kawaida kwa kocha yeyote baada ya kipindi
fulani kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine na ndiyo sehemu ya
maisha.
“Kama kocha unapoona ndiyo umefanya kazi
yako,unapaswa kuangalia mbele zaidi baada ya kufanya kazi yako si lazima
uendelee kuwa hapo, mnakaa na kujadiliana na kuachana kwa amani kisha
unapaswa kusonga mbele,ninaondoka nikiwa najivunia kipindi
nilichofundisha soka hapa,na ninawatakia kila la kheri Tanzania na Taifa
Stars kwa ujumla.”alisema Poulsen.
Kuhusu Kocha mpya wa Taifa Stars Jamal Malinzi
ambaye ni Rais wa TFF amesema hadi sasa wapo makocha watatu raia wa
Uholanzi ni wawili na Mjerumani mmoja wanaosailiwa kwa ajili ya kumrithi
Kim Poulsen,lakini moja ya vigezo Malinzi amesema kuwa ni lazima kocha
huyo awe amewahi kuipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
moja ya nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara.
Katika hatua nyingine kocha Salum Madadi
ameteuliwa kukaimu nafasi iliyoachwa wazi na Kim Poulsen ambapo kocha
huyo akisaidiwa na Hafidh Badru kutoka Zanzibar watasimamia Taifa Stars
kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia iliyoko kwenye kalenda ya FIFA
baadaye mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment