Friday 28 March 2014

NI SERIKALI MBILI AU TATU WAAMUE WABUNGE

 KIKWETE ASEMA TUWAACHE WABUNGE WAAMUE SERIKALI MBILI AU TATU

 

Rais Jakaya Kikwete amesema amemaliza  kazi ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba na sasa anawaachia wabunge wa bunge hilo kujadili na kuamua muundo wa Muungano unaofaa kama serikali mbili au tatu kwenye mapendekezo ya  Rasimu ya Katiba Mpya.


Rais Kikwete alielezea msimamo huo juzi wakati akizungumza na wazee  katika Ikulu ndogo ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara yake ya siku moja wilayani hapa, alitoa msimamo wake baada ya wazee hao kumweleza kwenye risala yao kuwa wao wanataka serikali mbili. Risala hiyo ilisomwa na   Mwenyekiti wa Wazee wa Wilaya ya Muheza, Hamisi Mzee.

Rais Kikwete alisema kwa sasa amewaachia wabunge kuamua muundo wa Muungano unaotakiwa na baadaye wananchi wataamua kama wanataka serikali tatu ama mbili wakati wa kupitisha Katiba.

Alisema kama watapendekeza serikali tatu ruksa kwani ndiyo mapendekezo yao, hivyo hayawezi kupingika kwa namna yoyote.

Hata hivyo, Rais Kikwetee alisisitiza kuwa lakini waelewe kuwa serikali tatu zina changamoto zake

 POLISI WAUA DEREVA WA BAJAJI KWA KIPIGO

 

Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni limeingia katika kashfa baada ya askari wake wa Kituo cha Stendi Kikuu ya Mabasi Ubungo (UBT), kutuhumiwa kumpiga, kumjeruhi na kusababisha kifo cha dereva wa bajaji, Salehe Said (19), maarufu kama ‘Kibange Moto’, mkazi wa Kigogo, jijini Dar es Salaam.
Dereva huyo alikutwa na mkasa huo, Machi 24, mwaka huu, saa 7:00 usiku, huku kukiwa na utata wa eneo alilokutwa na mauti.

Utata huo unafuatia polisi kudai kuwa dereva huyo alifariki wakati akiendelea na matibabu, huku kikundi cha madereva wa bajaji cha Jitume cha Ubungo kikidai kuwa alifia mikononi mwa polisi.

 Baadhi ya madereva wa bajaj walidai chanzo cha tukio hilo ni ugomvi kati ya marehemu na dereva teksi bubu uliotokana na kugombea abiria aliyefika katika eneo hilo kutafuta usafiri nje ya UBT.

Walidai kutokana na vuta nikuvute hiyo, wote wawili walikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi.

Kwa mujibu wa madereva hao, Saleh aligoma kuingia mahabusu ya kituo hicho akitaka kwanza aambiwe kosa lake.

Walidai jambo hilo lilisababisha askari huyo (jina linahifadhiwa) kuanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili na kuwa baada ya kipigo hicho, baadhi ya madereva wenzake walianza kumtetea, lakini nao walikamatwa na kuwekwa ndani.

Walidai baada ya muda mfupi, mwenzao aliyepigwa alianza kuvimba na polisi aliyempiga aliamua kumpeleka katika Hospitali ya Sinza Palestina, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.

“Wakati askari huyo amempiga dereva mwenzetu, walikamatwa wengine watano wakawekwa ndani, lakini hali ya mwenzetu ilipokuwa mbaya, askari walimchukua na kumpeleka katika Hospitali ya Palestina Sinza, lakini walipomrudisha kituoni, alizidiwa. Wakamrudisha tena hospitali usiku huo huo,” alisema mmoja wa madereva hao.

Aliongeza: “Mara ya kwanza walivyompeleka hospitali, walitumia bajaj ya mwenzetu, ambaye naye alikuwa amewekwa ndani, lakini mara ya pili hali ilipozidi kuwa mbaya, walimrudisha hospitali na hawakumrudisha tena kituoni.”

 Kijana huyo alisema Jumanne asubuhi baada ya kwenda kituo cha polisi cha UBT walikokuwa wameshikiliwa wenzao, waliambiwa kuwa walikuwa wamehamishiwa kituo cha Magomeni Usalama.

Alisema baada ya kwenda kituo cha Usalama, waliwakuta wenzao wanne, ambao waliwaeleza kwamba, mwenzao aliyekuwa amepigwa alipelekwa hospitali usiku na hakurudishwa tena kituoni.

 Alisema walipowauliza polisi mwenzao aliko, hawakutoa jibu lolote na ndipo waliamua kufuatilia katika hospitali waliyokuwa wamempeleka, lakini hawakumuona na hivyo kuanza kumtafuta katika hospitali nyingine.

“Tulipokosa jibu la wapi alipo mwenzetu kutoka kwa askari, tuliamua kutembelea kila hospitali. Tulipofika Mwananyamala kwenye wodi, napo tulimkosa. Tukaamua kwenda mortuary (chumba cha kuhifadhi maiti). Tukakagua daftari na ndipo tukaona jina lake,”  alisema.

Aliongeza: “Kwa kweli ilituuma sana. Tena kibaya zaidi, maelezo yalikuwa yameandikwa kuwa kifo chake kimesababishwa na kupigwa.
Tunaomba sheria ichukue mkondo wake huyo askari achukuliwe hatua kali. Na pia tunataka wenzetu waliokamatwa bila hatia, waachiwe kwa sababu polisi wamewabambikia kesi ya wizi wakati siyo kweli.Pia faili lake limeandikwa kwamba alipigwa na wananchi wenye hasira kali, tumechoka kuonewa.”
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema hana taarifa zozote juu ya tukio hilo.Hata hivyo, jana alipoulizwa tena alisema: “Kifo cha dereva huyo hakikusababishwa na askari.”

Wambura alisema dereva huyo alikamatwa na kufikishwa kituoni kwa tuhuma za kumvamia afisa wa Benki ya ABC na kumpora na kuwa baada ya kukamatwa, alijaribu kutoroka, lakini alikamatwa tena na polisi kwa kushirikiana na watu wengine na kurudishwa kituoni.

“Kwanza naomba unielewe kwamba kifo cha dereva huyo, ambaye pia inasemekana ni ‘deiwaka’ wa bodaboda hakikusababishwa na polisi.
Bali alitaka kuwatoroka polisi baada ya kukamatwa kutokana na kosa la kumvamia afisa wa ABC katika lango la kutokea stendi ya mkoa (UBT) na kikundi cha madereva wanaopaki katika eneo hilo. Na kati ya waliohusika na tukio hilo, ni pamoja na huyo marehemu,” alisema Wambura.
Alisema afisa huyo aliegesha gari lake akisubiri mgeni wake, lakini kikundi hicho kilimzongazonga na kuanza kumshambulia kisha kumpora Sh. 40,000, simu mbili na kadi za benki na kumchania nguo zake.

Wambura alisema afisa huyo aliripoti kituo cha polisi na baadaye askari walikwenda kuwakamata madereva hao.

Alisema majira ya saa 4:30 usiku, marehemu alizidiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Palestina Sinza.

Kwa mujibu wa Wambura, marehemu alirudishwa kituoni, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya, hivyo kulazimika kurudishwa tena hospitalini hapo na baadaye Hospitali ya Mwananyamala na kwamba, ilipofika saa 7:00 usiku alifariki.

Wambura alisema kutokana na madai mbalimbali, wanafanya uchunguzi kujua chanzo hasa cha kifo hicho.

TALIBAN YAISHAMBULIA KABUL

 

Wanamgambo nchini Afghanitan wameshambulia jumba moja la kukodi lililo karibu na majengo ya bunge kwenye mji mkuu Kabul .
Mwandishi wa BBC mjini Kabul anasema kuwa baada ya mlipuko mkubwa kusika mapigano yalifuata.

Jumba hilo lilitumiwa na wageni kutoka mataifa ya kigeni lakini mkuu wa polisi alisema kuwa hakukuwa na wageni wakati wa tukio hilo.

Kundi la Taliban limesema ndilo lilioendesha shambulizi hilo llikiwa moja ya mashambulizi kadha ambayo yameshuhudiwa wiki hii.

Kundi la Taliban limeapa kuwa litavuruga uchaguzi wa urais ambao utaandaliwa mwezi ujao nchini Afghanistan.

Thursday 27 March 2014

RAISI OBAMA KUKUTANA NA PAPA ROMA

 

Rais Barrack Obama wa Marekani anatarajiwa kukutana na kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, katika makao yake makuu huko Vatican.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Obama kukutana na papa Francis.

Wawili hao wanatarajiwa kujadili namna ya kupunguza tofauti iliyopo kati yao katika maswala mengi mbali na kujaribu kuinua maisha ya watu maskini duniani baada ya takwimu kuonyesha kuwa tofauti ya mapato kati ya matajiri na Masiki inaendelea kupanuka .

Aidha viongozi hao wawili wanatazamiwa kujadili hali ilivyo Nchini Ukraine, na swala la upatikanaji wa amani mashariki ya kati.

Mwafaka baina ya mitazamo tata kuhusiana na maswala ya uavyaji mimba, matumizi ya dawa za kupanga uzazi na ndoa ya jinsia moja pia inatarajiwa kuwa kati ya mada itakayojadiliwa .

UN YAILAANI MISRI KUHUSU HUKUMU YA KIFO

 

Umoja wa Mataifa umelaani kitendo cha Misri kuwahukumu kifo zaidi ya watu miatano ikisema kuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Umoja huo umesema kuwa idadi ya watu waliohukumiwa Jumatatu, ndio idadi kubwa ya watu kuwahi kuhukumiwa kifo kwa wakati mmoja katika miaka ya hivi karibuni.

Mawakili wa utetezi wamesusia kesi ya pili ya watu wengine karibu miasaba wafuasi wa Morsi wanaokabiliwa na tuhuma sawa na zile zilizowakabili watuhumiwa wa kwanza.
Wamlalamikia kile wanachosema ni mahakama kukosa kufuata utaratibu unaofaa.

Kesi ya wafuasi wengine 682 waliosalia ilianza kusikilizwa mapema leo lakini ikaahirishwa baada ya muda mfupi huku jaji akisema kuwa hukumu itatolewa mwezi ujao.

MKUU WA JESHI KUGOMBEA URAISI MISRI



Mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi Misri, Abdul Fattah al-Sisi, ametangaza kujiuzulu jeshini ili kugombea katika uchaguzi wa urais mwezi ujao.
Wagombea wote wanapaswa kuwa raia.
Akizungumza Kwenye hotuba ya Televisheni huku akiwa amevalia sare ya kijeshi Abdel Fattah El Sissi amesema yeye sio mwanajeshi tena baada ya miaka 44 na kwamba amechukua hatua hiyo ili aweze kutimiza jukumu lingine muhimu.

Ni Bayana kwana Sisi hatakua na kibarua kigumu kujipatia ushindi katika uchaguzi wa Urais. Anaungwa mkono na idadi kubwa ya raia wa Misri na hadi sasa hana wapinzani wowote.
Baadhi ya waliotaka kugombea urais wamejiondoa wakidai kwamba hawataweza kuendesha kampeni zao kwa njia huru.

Wafuasi wake Sisi wanamuona kama kiongozi imara ambaye anaweza kurejesha amani na udhabiti nchini Misri baada ya miaka mingi ya machafuko.
Wakosoaji wake wanasema ana msimamo mkali na amechangia pakubwa katika kusambaratisha na kuhujumu upinzani nchini Misri.

Mkuu huyo wa jeshi atakabiliwa na majukumu mazito ya kufufua uchumi uliofifia , kupambana na uasi na kuileta pamoja nchi iliyogawanyika. Ameahidi kutekeleza mabadiliko makubwa lakini akaonya kuwa hawezi kufanya miujiza.

Tuesday 25 March 2014

 MGOMO WA DALADALA MOSHI


 

Vurugu  kubwa zimezuka katika kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi na kusababisha gari lililowabeba askari kanzu wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro kupopolewa kwa mawe na kisha kuvunjwa vioo na watu wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi yanayotoa huduma  hiyo katika miji ya Arusha na Moshi.


Vurugu hizo zilitokana na wamiliki wa mabasi pamoja na madereva kugoma kutoa huduma kuanzia asubuhi saa 11 hadi saa 10:30 jioni wakilalamika kuwa wanalazimishwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani kutoa rushwa ili kuficha makosa baada ya kuwadai stakabadhi ya uthibitisho wa malipo wanayotoa kwa askari hao.


Gari la Polisi lilipopolewa kwa mawe na kuvunjwa vioo likiwa na askari kadhaa ni lenye namba za usajili T 743 ADC Toyota Land Cruiser, lilikumbana na dhoruba hiyo baada ya askari kujaribu kumkamata mmoja wa madereva wa mabasi hayo ambaye hakufahamika jina mara moja anayefanya safari kati ya Moshi Mjini na Holili mpakani mwa Tanzania na Kenya.


Kufuatia mgomo huo, abiria wanaosafiri katika miji ya Arusha, Moshi na wilaya sita za mkoa wa Kilimanjaro walikwama kwa kutwa nzima jana.


 Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mabasi Kanda ya Kaskazini (Akiboa), Hussein Mrindoko, wamesema kua wameamua kugoma kutokana na baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani kugeuza stakabadhi za malipo yanayotokana na faini kuwa mtaji wa kibiashara kwa kuwa wanatoza gari moja faini ya Sh. 30,000 hadi mara tatu kwa siku.


 “Tunakuomba Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (Leonidas Gama) uchukue hatua za kimaadili dhidi ya maofisa watatu wa Jeshi la Polisi ambao wamekuwa wakifanya maamuzi ya kibabe na kusababisha uzaliwe mgogoro huu. Huyo ofisa anayekojoa nyuma ya magari halafu amelewa ni fedheha kwa jeshi na serikali kwa ujumla,” alisema Mrindoko katika kikao alichoitisha mkuu huyo wa mkoa.


Wakiwa katika mkutano huo wa usuluhishi, baadhi ya madereva hao na wamiliki wa mabasi walimweleza Gama kwamba Mkuu wa kikosi hicho, Mkuu wa kituo kidogo cha Polisi cha Stendi Kuu ya Mkoa na Mkaguzi wa Polisi kituo cha Himo wamekuwa na desturi ya kufanya kazi kwa ubabe ikiwamo kuwapiga makonde na kuwabambikizia makosa baada ya kuhoji uhalali wake, hivyo kusababisha uhasama mkubwa.


 Akijitetea, Mkuu  wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO), Joseph Mwakabonga, alikiri kumpiga makonde mmoja wa wamiliki wa mabasi wa wilaya ya Hai,  Abdulrazack Mtoro, akidai sheria inamruhusu kufanya hivyo pale kunapokuwa na vurugu.


Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Stendi Kuu (OSC), Hendry Nguvumali, alisema madereva na wamiliki wa mabasi hayo wanashuhudia uongo kwa kumdanganya mkuu wa mkoa kwamba yeye ni mlevi wa kupindukia na amekuwa akikojoa nyuma ya mabasi ya abiria, jambo ambalo haliwezi kumzuia kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.


Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, akizungumzia malalamiko yanayotokana na kupotoka kwa maadili ya askari, alisema ofisi yake itachukua hatua za kimaadili haraka iwezekanavyo, ingawa wananachi pamoja na madereva wa mabasi hayo wanatakiwa pia kutii sheria za usalama barabarani bila kushuruti.


 “Nitachukua hatua mara moja kuhusu maadili, hili la ulevi wa kupindukia kwa kweli limelidhalilisha Jeshi la Polisi, lakini pia suala la kupiga watu makonde siyo utaratibu kwa sababu ofisa anatakiwa kufuata sheria na kwa kuwa amekiri mwenyewe (RTO) nitalitazama kwa kufanya uchunguzi,” alisema Boaz.


Gama alisema iwapo mgomo huo wa mabasi utaachwa uendelee kwa siku ya pili, unaweza ukasababisha kuporomoka kwa uchumi wa mkoa huo.  Gama aliamuru Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kupeleka ofisini kwake ratiba inayoonyesha namna anavyokutana na wadau wa usafirishaji pamoja na kushughulikia kero zinazotokana na askari wa usalama barabarani.


 “Nyie Polisi, Sumatra na wasafirishaji mnafanya kazi zenu kwa kuviziana na kutengenezeana uhasama ili kuonyeshana ubabe. Muda mfupi baada ya kukaa na kamati yangu ya ulinzi na usalama, nitatoa taarifa kwa umma kuhusiana na hatua za kinidhamu nilizochukuliwa kama serikali kwa niaba ya Waziri Mkuu,” alisema Gama na kuongeza:


 “Sumatra nataka mnieleze kwa nini agizo langu hamjatekeleza hadi sasa na mmezalisha mgogoro huu?”
Mgomo huo ulisababisha wananchi kutumia usafiri wa bodaboda, bajaj na magari madogo ya kukodi. Hawa Hussein, mkazi wa Rombo alisema mgomo huo uliathiri shughuli zake nyingi za kiuchumi.


Francis Meena, mkazi wa Sanya Juu alisema mgomo huo ulisababisha adha kubwa ikiwamo kutembea kwa miguu umbali mrefu huku wengine wakilazimika kuingia gharama za kukodi bodaboda kwa gharama ya Sh. 5,000.
Mkaguzi mmoja aliliambia gazeti hili kuwa magari hayo yanastahili kukamatwa na trafiki kwa kuwa mengi ni mabovu na yanakiuka sheria za barabarani.


Alizitaja kuwa ni kupakia abiria katika maeneo yasiyo rasmi, hayafanyiwi usafi na kutokidhi viwango vya magari ya abiria.
Alisema wamiliki wake wanalalamikia, magari yao kukamatwa, lakini wana makosa mengi ya kiusalama.


 “Ninakuambia katika magari 300 ni magari 20 yatakidhi vigezo vya kubeba abiria kama yakikaguliwa sawasawa,” alisema mkazi mmoja wa mjini Moshi aliyejitambulisha kama msafiri wa kila siku ndani ya mkoa wa Kilimanjaro.

URUSI YATENGWA NA G7

 


Viongozi wa kundi la mataifa saba tajiri zaidi duniani, G-7, wanafanya mazungumzo kwa siku ya pili mfululizo hivi leo mjini Hague, Uholanzi ajenda kuu ikiwa ni hatua ya Urusi kunyakua jimbo la Crimea kutoka Urusi.

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, Moscow imenyimwa kiti katika kongamano hilo. Mkutano wa dharura wa G-7 uikubaliana kufutilia mbali kundi la G-8, kundi la mataifa manane tajiri zaidi duniani, ambalo linaishirikisha Urusi.

Viongozi wa mataifa ya kundi hilo wameonya kuwa vikwazo zaidi vitatolewa iwapo Urusi itaingia maeneo ya mashariki au Kusini mwa Ukraine ikiwepo kulenga sekta ya kawi nchini Urusi. Lakini Marekani kadhalika imesisitiza kuwa fursa ya kusuluhisha mzozo huo wa njia ya kidiplomasia ingalipo.

 SHUGHULI YA KUITAFUTA MH370 IMESITISHWA


 

Mamlaka ya usalama wa safari za baharini nchini Australia imesema kuwa operesheni ya kuitafuta ndege ya shirika la Malaysia iliyotoweka imesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa na mawimbi makali baharini.

Taarifa zinasema kuwa upepo mkali pamoja na mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo ina maana kuwa ndege hazitoweza kupaa kwa usalama. Mawimbi makali yameilazimisha meli ya jeshi la wanamaji wa Australia kuondoka katika eneo ambalo mabaki yanayodhaniwa kuwa ya ndege hiyo yalionekana hapo jana Jumatatu.

Dr Erik van Sebille, ambaye ni mtaalam wa maswala ya Baharini katika chuo kikuu cha New South Wales mjini Sydney, amefanya utafiti katika eneo hilo la kusini mwa Bahari Hindi kutambua ni wapi na vipi vifusi vinasafirishwa na mawimbi ya bahari. Anasema itakuwa vigumu sana kupata mabaki ya ndege hiyo.

" Ni eneo lisiloweza kukalika duniani, acha niseme. Upepo unaovuma ni mkali sana, mawimbi ni makubwa, ni mojawepo wa mawimbi makubwa zaidi baharini. Unapofika katika eneo hili la kusini, unaanza kuhisi athari za eneo la Antactica kwenye bahari.

Hapa tunazungumzia dhoruba kali kali sana hususan wakati huu tunapoingia majira ya kupukutika," anasema Dr. Erik van Sebille.Kadhalika amesema kuwa vifusi vilivyoenekana hapo jana tayari vimekwishaondolewa katika eneo hilo na mawimbi makali.

"Haitakuwa rahisi kabisa kupata kijisanduku cha kunasa habari. Mawimbi ya eneo hili ni makali na kwa hiyo vifusi ambavyo wametambua kwa sasa huenda vimehamishwa katika kipindi cha majuma mawili au matatu tangu ndege hiyo ianguka-na huenda vimesafiri kilomita alfu moja tayari. Na hii inaifanya vigumu kurejelea utafutaji kwa sababu bahari inabadilika sana hapa-ina vurugu ukipenda."

Hapo awali naibu waziri wa mashauri ya nchi za Kigeni wa China Xie Hangsheng, aliitaka serikali ya Malaysia kutoka ushahidi unaoelezea kuwa ndege hiyo ilianguka katika eneo la Kusini mwa bahari Hindi. Ndege hiyo ilitoweka kwenye mtambo wa Radar zaidi ya majuma mawili yaliyopita.

MPASUKO BUNGENI

MPASUKO BUNGENI


Wakati kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba za kupitia Rasimu ya Katiba zikitarajiwa kujulikana leo, hali ya mpasuko katika Bunge hilo imezidi kuwa dhahiri ikichochewa zaidi na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Ijumaa iliyopita.Mpasuko huo unajidhihirisha dhahiri baada ya sasa kuibuka makundi kinzani ndani ya Bunge Maalum la Katiba.


Wakati kundi la wabunge wanalounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) likijitokeza juzi na jana kuelezea kutoridhishwa kwao na hotuba hiyo kiasi cha wengine kujuta kushiriki katika maridhiano, kundi jipya la Tanzania Kwanza limeanzishwa.


TANZANIA KWANZA
Umoja wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaojiita ‘Tanzania Kwanza‘ wameeleza kusikitishwa na kauli za baadhi ya wajumbe wenzao zenye muelekeo wa kuhujumu mchakato wa kupata Katiba mpya ambazo wamekuwa wakizitoa baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge hilo Maalum.


Umoja huo ambao unaundwa na wajumbe kutoka chama tawala-CCM unadai kuwa na wajumbe 400, umedai kuwa viongozi waliotoa kauli hizo walionekana awali wakishangilia hotuba ya Rais pale aliposema yale waliyokuwa wanakubaliana nayo, lakini sasa watishia vurugu na kususia baadhi ya mambo wasiokubaliana nayo.


MKUMBA

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja huo, Said Mkumba, alisema wameshangazwa na wajumbe hao waliotoa kauli nzito na kuacha kuweka utaifa mbele kwa kushawishiana hoja kuliko kulazimisha kutunga Katiba itakayoimarisha Taifa.


Alisema kuwa wajumbe walionekana kukerwa na baadhi ya maneno yaliyotamkwa na Rais Jakaya Kiwete ya kuwa na ustahimilivu wa kidemokrasia, ustaarabu na hekima ya uongozi na utu uzima.


Mkumba alisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete imeweka wazi faida na hasara za mifumo yote ya Muungano wa nchi kwa hoja ili Watanzania wawe na fursa pana zaidi ya kutafakari na mwisho kuamua, hivyo wanashangazwa na baadhi ya wajumbe wenzao kutoa matamko hayo.


Naye Dk. Emanuel Nchimbi ambaye ni Mjumbe wa Umoja huo, aliwataka Wajumbe wa Bunge Maalum wasivumilie wala kuendekeza vitendo vya vurugu za makusudi vitakavyozuia au kuruhusu watu wachache waliweka rehani Bunge kwa kutengeneza mtaji wa kisiasa.

 
MBATIA AJUTA
Hali ilizidi kudhihirisha mgawanyiko mkubwa ndani Bunge hilo, Mjumbe wa Bunge hilo, James Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, ameowaomba radhi Watanzania kwa kushiriki kikao cha Kamati ya Maridhiano, ambacho kiliridhia kuvunjwa kwa kanuni ya 7 (1) ya Bunge hilo.

Kanuni hiyo inataka Rais azindue Bunge Maalum kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba haijawasilisha Rasimu ya Katiba.

Akizungumza na wandishi wa habari mjini Dodoma, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema anajutia uamuzi wake wa kushiriki kwenye maridhiano hayo.

Thursday 20 March 2014

 HOTUBA MAALUM YA UFUNGUZI WA BUNGE LA KATIBA

 

Siku  tatu baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, kutikisa Bunge Maalum la Katiba kwa hoja nzito juu ya rasimu ya katiba, kesho mji wa Dodoma utarindima tena kwa kufunikwa na viongozi wakuu wote wa kitaifa waliopo madarakani na waliostaafu.


Ugeni huo umealikwa bungeni kushuhudia hotuba ya ufunguzi wa bunge hilo la kihistoria itakayotolewa na Rais Jakaya Kikwete kesho kama sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012.
Tukio hilo litahudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Wengine walioalikwa ni wajane wa waasisi, Mama Maria Nyerere na Fatma Karume.
 Akizungumza na waandishi wa Habari jana, Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, alisema kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, amewaalika wageni mbalimbali ili kushuhudia tukio hilo muhimu la kitaifa.

Khamis aliwataja wageni wengine walioalikwa kuwa ni pamoja na marais wastaafu kutoka pande zote za Muungano. Marais wastaafu waliopo ni Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour Juma na Amani Abeid Karume.

 Wengine ni maspika wastaafu, Waziri Kiongozi mstaafu ambaye hakutajwa jina. Hata hivyo, mawaziri kiongozi wastaafu waliopo ni Shamsi Vuai Nahodha ambaye ni Mjumbe wa bunge hilo, Ramadhan Haji Faki na Maalim Seif. Spika Mstaafu ni Pius Msekwa.

 Waalikwa wengine ni watendaji wakuu kutoka pande zote za Muungano, mabalozi wa nchi mbalimbali waliopo nchini, wawakilishi wa taasisi za kimataifa pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za ndani ya nchi.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni taasisi za kidini, wawakilishi wa tasnia ya habari, vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi zisizo za kiserikali, vyama vya watu wenye ulemavu, taasisi ya elimu, vyama vya Wafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya wavuvi, vyama vya wakulima na wawakilishi toka sekta binafsi.

Akizungumzia mpangilio wa shughuli hiyo, Khamis alisema kuwa Bunge litaanza kikao chake majira ya saa 9:10 jioni na baadaye kikao kitaahirishwa saa 9:20 kwa ajili ya kumpokea Rais.
Khamis aliwataka wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba pamoja na waalikwa wote kuwahi kuingia ndani ya ukumbi kabla Rais hajawasili kwenye viwanja vya Bunge.
Alisema baada ya Rais kuwasili katika viwanja vya Bunge, atapokewa na Mwenyekiti wa Bunge, Makamu wake, Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba.
Alisema baada ya mapokezi, Rais ataelekea kwenye Jukwaa maalum kwa ajili ya kupokea salamu ya heshma na kukagua gwaride Maalum ambalo limeandaliwa na Jeshi la Polisi.
Khamisi alisema kuwa tukio la kukagua gwaride hilo litakapokamilika, viongozi wataingia bungeni kwa maandamano maalum kwa ajili ya kwenda kusikiliza hotuba ya Rais ya kuzindua Bunge hilo.

Alisema viongozi watakaoshiriki maandamano hayo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atafuatana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum.

Alisema Rais atakapomaliza kuhutubia, Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba watapata fursa ya kupiga picha ya pamoja na Rais.
Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia Bunge saa 10:00 jioni kwa mujibu wa kanuni ya 75 (1) ya Bunge Maalum la Katiba.
Ingawa maudhui ya hotuba ya Rais Kikwete hayajajulikana, hotuba ya Jaji Warioba bungeni juzi, imekuwa ni jambo zito ambalo yamkini yatagusiwa kwa mapana yake.

Miongoni mwa mambo nyeti na  yamekuwa na ubishani mkubwa ambayo yameibuliwa na Tume na kuwekwa kwenye Rasimu ya Katiba ni pamoja na muundo wa Muungano wa serikali mbili, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakipinga kwa nguvu zote.

Mambo mengine ni kupunguzwa kwa kiwango kikubwa kwa madaraka ya rais; kujenga uwajibikaji kwa kuweka maadili ya viongozi ndani ya katiba; kuimarishwa kwa haki za raia na kuwandoa mawaziri kuwa wabunge.

Hofu iliyokuwa imetanda mjini Dodoma ambayo ilisababisha hata Jaji Warioba kushindwa kuwasilisha hotuba yake Jumatatu, ni suala linaloonekana kama kuviziana na kukosekana kuaminiana baina ya wabunge wanaotokana na CCM na wale wa upinzani wakishirikiana na wa kundi la kuteuliwa lenye wajumbe 201.

MSUKOSUKO WA AMANI SUDANI YA KUSINI




Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa naibu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar yanatarajiwa kuanza tena leo mjini Addis Ababa Ethiopia. Mazungumzo hayo yaliahirishwa mapema mwezi huu baada ya mazungumzo ya hapo awali kukwama.
Aidha, pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini mwezi Januari. Mnamo siku ya Jumatano, mataifa ya magharbi yanayohusika na mgogoro huu wa Sudan Kusini katika kuutafutia suluhu la kudumu, walitishia kuwawekea vikwazo wahusika wakuu kwenye mgogoro huo ikiwa hawatausuluhisha.

Mazungumzo ya kuzipatanisha pande hizo hayajapiga hatua kwa wiki mbili zilizopita huku wahusika wakilaumiana. Serikali na waasi wanalaumiana kwa kuyumbisha mazungumzo ya amani. Nao mkataba wa amani uliotiwa saini kusitisha vita pia haujafanikiwa katika kumaliza mgogoro huo.

Baadhi ya wanadiplomasia kutoka nchi za magharibi, wamehoji ikiwa viongozi wamejitolea kikweli kutafuta muafaka huku kila mhusika akimlaumu mwenzake kwa kizungumkuti kilichoko.

Mazungumzo hayo yanaanza tena baada ya wiki mbili ya kusitishwa kwake, ingawa wajumbe wamesema haijulikani ikiwa pande hizo mbili zitakuwepo. Maswala makuu yanayoyumbisha mazungumzo hayo, ni matakwa ya waasi wa Sudan Kusni kwamba wafungwa wanne wa kisiasa ambao bado wanazuiliwa, sharti waachiwe huru.

Wanne hao walilaumiwa kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir wakiongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar.

VIFUSI VYA NDEGE VYAONEKANA AUSTRALIA


 

John Young meneja mkuu wa halmasshauri ya usalama wa ndege nchini Australia

Waziri mkuu wa Australia amesema kuwa mitambo ya satelite ya nchi hiyo imenasa picha za vitu vinavyoonekana kama vifusi ambavyo huenda ni vya ndege ya Malaysia iliyopotea siku 13 zilizopita.

Waziri mkuu huyo, Tony Abbott, ameambia bunge mjini Canberra kwamba picha za Satelite zimeonyesha vitu viwili vinavyofanana na vifusi vya ndege hiyo. Taarifa hii imejitokeza karibu wiki mbili baada ya ndege hiyo kutoweka na abiria zaidi ya miambili kutoka mjini Kuala Lumpur Malaysia kuelekea Beijing.

Msemaji wa halmashauri ya usalama wa safari za ndege, John Young, baadaye alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo kimoja kina ukubwa wa mita 24, vimeonekana umbali wa kilomita 2500 kusini Magharibi mwa pwani ya Australia.Aliongeza kwamba,vifusi itakuwa vigumu kuviona vifusi hivyo na pia huenda sio vya ndege hiyo.

Wakati taarifa hii ilipotolewa, kulikuwa na ndege ya Australia katika neo hilo , ndege zaidi zinatarajiwa kuwasili katika eneo lenyewe na pia manowari ya jeshi inaelekea huko.

Wednesday 19 March 2014

 WASIWASI MWINGINE WATANDA UKRAINE

 

Hali ya wasiwasi imetanda eneo la Crimea kufuatia kuuawa kwa afisa mmoja wa kijeshi kwa kupigwa risasi. Jeshi la Ukraine lilisema kuwa afisa huyo aliuawa wakati watu wenye silaha waliokuwa katika sare za kijeshi za Urusiwalipofyatulia risasi kituo kimoja cha kijeshi cha Ukriane cha Kiev.

Afisa huyo ameuawa masaa machache baada ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov kumwonya mwenzake wa Marekani, John Kerry kuwa vitisho vya Marekani vya kuwekea taifa lake vikwazo vya aina yo yote baada yaCrimea kutangazwa na Urusi kuwa sehemu moja ya taifa hilo si haki.Urusi imesema inatafakari hatua zitakazochukuliwa na mataifa ya Magharibi kabla ya kuamua la kufanya.

Ikulu ya White House imesema kuwa Rais Obama na Chansela wa Ujerumani Angela Markel wamekubaliana katika mashauriano kwa njia ya simu kuwa wachunguzi wa kimataifa wanapaswa kutumwa Kusini na Mashariki mwa Ukriane kufuatia uamuzi wa Urusi kuchukua sehemu ya Crimea kutoka kwa Ukraine.

Maafisa hao wa Ikulu walisema viongozi haowawili walishutumu hatua ya Rais wa Urusi Putin ya kutangaza eneo hilo kuwa chini ya Urusi baada ya kura ya maoni.

Hata hivyo walisema kuwa njia za kidiplomasia zingali wazi kuhusiana na hali hiyo.
Mnamo Jumatano Makau wa Rais wa Marekani alisema huo ulikuwa unyakuzi wa ardhi.

Juma lililopita Marekani na Jumuiya ya Ulaya walisema watapiga tanji mali ya viongozi fulani wa Urusi na Ukraine na piakuweka masharti magumu ya wakaazi wa Urusi kutembelea mataifa hayo ya Magharibi.

NDUGU WA WALIOPOTEA NA NDEGE WATISHIA KULA

 NDUGU WA JAMAA WALIOPOTEA NA NDEGE YA MALAYSIA WATISHIA KUSUSIA CHAKULA

 

Jamaa za abiria wa China waliokuwa kwenye ndege ya Malaysia iliyopotea,wametishia kususia chakula ikiwa maafisa wa utawala wa Malaysia watakosa kutoa taarifa kamili kuhusu ndege hiyo siku 11 zilizopita.
 
Jamaa hao wameelezea kukerwa mno baada ya mkutano na maafisa wa shirika la ndege hiyo mjini Beijing.Maafisa wa Malaysia nao wanasema kuwa wanafanya kila wawezalo katika kuisaka ndege hiyo.

Ndege hiyo MH370 ilitoweka tarehe nane mwezi Machi ikiwa imewabeba watu 239.
Nchi 25 zinahusika na juhudi za kuisaka ndege hiyo huku China ikianza kuitafuta katika ardhi yake.Watu 153 raia wa China walikuwa kwenye ndege hiyo iliyokuwa inatoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing.

Vyombo vya habari nchini China vimekuwa vikikosoa juhudi za Malaysia katika kuitafuta ndege hiyo.Baadhi ya jamaa za wachina wanasema kuwa wanaamnini serikali ya Malaysia imebana taarifa kuhusu ndege hiyo na wanataka maelezo zaidi kuihusu.

Baada ya kukutana na maafisa wa shirika la ndege siku ya Jumanne, familia za waliokuwa kwenye ndege hiyo walitishia kususia chakula
"Tunachokitaka ni ukweli,'' alisema mwanamke mmoja.

Wakati huohuo, nchi jirani ya Malaysia, Thailand imesema kuwa jeshi lake limetambua kile linachosema ni Data za mtambo wa Rader ambazo huenda zilitoka kwenye ndege hiyo.
Inasema kuwa ndege hiyo ilikuwa inaelekea Magharibi baada ya kupoteza mwelekeo. Hii inathibitisha madai ya hapo ya awali ya jeshi la Malaysia.

MCHINA JELA MIAKA 20 KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO


Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu raia wa China, Yu Bo (45), kulipa faini ya Shilingi  bilioni tisa au kwenda jela miaka 20 baada ya kukiri kukutwa na nyara za serikali.


Yu, alikamatwa akiwa na kilo 303 za nyara hizo ikiwamo ngozi za vinyonga wawili vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 975 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Devota Kisoka, baada ya upande wa Jamhuri kumsomea mshtakiwa mashitaka na kukiri.


Alisema baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake, mahakama imemtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Shilingi bilioni tisa na akishindwa aende jela miaka 20. Hata hivyo hadi kufikia majira ya saa 9:00 alasiri hapo jana Yu alikuwa hajafanikiwa kulipa faini hiyo.


Kabla ya hukumu hiyo kusomwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na alimkumbusha mshtakiwa mashitaka yake.


Nchimbi alidai kuwa Desemba 30, mwaka 2013, katika Bandari ya Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na nyara hizo bila kuwa na leseni ya Mkurugenzi wa Wanyamapori.


Alidai kuwa mshtakiwa alikutwa akiwa na vipande 81 vya pembe za ndovu ambazo zimetokana na kuwaua tembo 40 zenye thamani ya Sh. 975,076,350 na ngozi mbili za vinyonga wawili zenye thamani ya Sh. 3,044,140 vyote vikiwa na jumla ya thamani ya Sh. 978,120,490 mali ya Serikali ya Tanzania.


Mshtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo alikiri na mahakama ikamhukumu adhabu hiyo.
 

Tuesday 18 March 2014

MAFURIKO YALETA MAAFA NIGERIA






Zaidi ya watu 50 wamefariki nchini Burundi baada ya kusombwa na maji pamoja na maporomoko ya udongo.Kwa mujibu wa waziri wa usalama, mvua kubwa ilinyesha usiku kucha katika mji mkuu Bujumbura na kusababisha uharibifu mkubwa.Majumba yamebomoka kufuatia mvua hiyo kubwa.

Waziri Gabriel Nizigama amesema kuwa tayari wamepata miili ya watu 50, waliofariki baada ya nyumba zao kuporomoka na kusombwa na maji.
Mitaa na vitongoji vya mji mkuu Bujumbura viliopo kaskazini vimeathirika zaidi.

Serikali ya Burundi mbali na kutangaza kwamba itagharamia mazishi na huduma kwa majeruhi, imetangaza pia siku moja ya maombolezi ya kitaifa siku ya Jumanne.

Baadhi ya walioshuhudia shughuli za uokozi
Miongoni mwa tarafa ambazo zimeathirika sana ni Kamenge sehemu inayopakana na mkoa wa Bujumbura.

Inaarifiwa watu wengi hususan watoto wamepoteza maisha.
Majeruhi wamelazwa katika hospitali kuu za serikali mjini Bujumbura na hasa Hospital Roi Khaled.

Na kutokana na uhaba wa nafasi katika vyumba vya kuhifadhi maiti, baadhi ya maiti zimezikwa leo,kwa idhini ya familiya zao na shughuli za uokozi zinaendelea lakini zinakabiliwa na ukosefu wa vifaa, inasadikiwa kuwa maiti nyingi bado zimenaswa katika vifusi vya majumba.

ALSHABAAB WASHAMBULIA HOTELI YA KIJESHI

 

Wanamgambo wa kiislam nchini Somalia wameshambulia hoteli moja muhimu katika eneo la Kati mwa Somalia ambalo wanamgambo hao walipoteza udhibiti wake wiki iliyopita.

Walioshuhudia shambulio hilo wameiambia BBC kuwa gari lililipuka nje ya hoteli hiyo katika mji wa Bulo-burde wanakoishi askari wa muungano wa Afrika na makamanda katika jeshi la Somalia .
Mlipuko huo ulifuatiwa na makabiliano ya risasi yaliyodumu kwa muda wa saa tano.

Walioshuhudia wanasema takriban watu kumi na wanne wameuawa katika shambulio hilo , ambalo wapiganaji wa al-Shabab wamesema walilitekeleza.

Mji wa Bulo-burde ulitwaliwa tena katika moja ya harakati za kijeshi zinazoendeshwa na vikosi vya Amison na vile vya serikali dhidi ya wanamgambo hao.

WAPINZANI WAFUNGWA MAISHA BURUNDI

 

Wanachama kadhaa kati ya sitini wa chama cha upinzani nchini Burundi MSD waliofikishwa mahakamani leo , wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hii ni baada ya serikali kuwatuhumu kwa kosa la kusababisha vurugu na kupanga njama ya mapinduzi dhidi yake.
Wengine bado wanasubiri hukumu huku kesi zao zikiendelea.
Walikamatwa baada ya kuhusishwa na purukushani iliyotokea tarehe nane mwezi Machi baina ya wafuasi wa chama hicho na polisi.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa leo katika mahakama ya jiji la Bujumbura.

Mawakili wao wamekosoa uamuzi huo wakisema kuwa umekiuka sheria kwa kile wamesema kwamba kuna maombi mengi waliomba kabla ya kesi hii kusikilizwa ingawa hayakuzingatiwa na mahakama.Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza imesema wapinzani walihusika na vurugu pamoja na kupanga njama ya mapinduzi.

Mnamo siku ya Jumatatu, Umoja wa mataifa na Muungano wa Ulaya zilielezea wasiwasi kuhusu mvutano wa kisiasa unaozidi kutokota kati ya serikali na vyama vya upinzani nchini Burundi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alilaani hali ya kisiasa nchini humo,akisema kuwa serikali inakandamiza uhuru wa kisiasa, uhuru wa kuongea na watu kukutana.

Bwana Ban alisema kuwa sio jambo zuri kwa polisi kuingilia maandamano ya upinzani.Agizo hili lilitokana na ghasia za kisiasa kati ya wanaharakati wa upinzani na polisi mapema mwezi huu.

Wiki jana mahakama nchini humo ilimchukulia hatua kiongozi wa chama cha upinzani (Movement for Solidarity and Development party) ambaye pia ni mwandishi habari wa zamani, Alexis Sinduhije na wanaharakati wengine 71 kwa madai ya njama ya mapinduzi.

Serikali pia ilisitisha shughuli zote za chama cha upinzani cha MSD kwa kipindi cha miezi minne baada ya kukishutumu kwa kuzua vurugu.
Chama hicho kimekanusha kusababisha vurugu zozote.

BUNGE MAALUM LA KATIBA LAVURUGIKA

 


Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, jana alianza vibaya kazi ya kuongoza hilo baada ya baadhi ya wajumbe kugoma kusikiliza taarifa ya Rasimu ya Katiba Mpya iliyokuwa iwasilishwe na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.


Hali hiyo ilitokea dakika chache tu baada ya Sitta kumtaka Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah kutangaza utaratibu unaofuata, akitangaza kuwasilishwa kwa Rasimu hiyo.

Hata hivyo, Bunge hilo liliahirishwa saa moja baadaye baada ya Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad, kutangaza kuahirishwa kwa Bunge hilo hadi hapo wajumbe watakapotangaziwa baadaye.

“Wajumbe Bunge limeahirishwa hadi hapo mtakapopewa taarifa baadaye, tunaomba muondoke ndani ya ukumbi huu,” alisema.

“Tutawatangazieni wakati tutakapokuja kuendelea na kikao cha Bunge. Waheshimiwa leo ninawaomba tutawanyike,” aliongeza.

Awali kabla ya kuahirishwa kwa Bunge hilo, Sitta alisimama na kumuomba Jaji Warioba kwenda mbele ya Bunge kuwasilisha taarifa yake.


Hata hivyo, baada ya tamko hilo la Mwenyekiti.  Profesa Ibrahim Lipumba, alisimama kuomba mwongozo akifuatiwa na Moses Machali, ambao hata hivyo, hawakusikilizwa na Mwenyekiti aliwataka kuketi kwa kuwa alisema hakuna mwongozo kwenye suala hilo.


Wengine waliosimama ni Freeman Mbowe, James Mbatia na Mchungaji  Christopher Mtikila.Hatua hiyo ilisababisha wajumbe wengine wa Umoja wa Wanaotetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimama na kugonga meza huku wakipasa sauti ya “Fuata kanuni mwenyekiti, tutaendelea hivi hadi utakapoacha kuvunja kununi.”
 
Inayodaiwa kuvunjwa ni kanuni ya 7 (1) h, ambayo inaelezea uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi ilitakiwa ianze, lakini ilitenguliwa ili kuruhusu Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo.
Wakati hayo yakiendelea Jaji Warioba alikuwa amesimama sehemu aliyotakiwa kuwasilisha taarifa yake kwa dakika tano bila kuanza kuisoma huku akiwa amepigwa butwaa kutokana na makelele yaliyotawala ndani ya ukumbi huo.

Licha ya makelele ya wajumbe hao, Sitta aliendelea kumsisitiza Jaji Warioba aendelee kuwasilisha taarifa yake, lakini ilishindikana kutokana kelele za zomea zomea kuongezeka na kumsababisha Jaji Warioba kuondoka mbele na kwenda kuketi sehemu maalumu waliyopangiwa  wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kufuatia hali hiyo, Sitta alisimama na kusema: “Katika mazingira haya hatuwezi kuendelea, naomba kutangaza kuahirisha Bunge kwa sasa hadi hapo tutakapotangaza baadaye.”

Baada ya kutamka hayo, Sitta alitoka nje ya ukumbi na baadaye kupita sehemu ya waandishi wa habari kuelekea kwenye chumba cha kikao.

Wakati akipita kwenye chumba cha waandishi wa habari akiwa ameongozana na Naibu Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, waandishi hao walimpa pole Sitta, naye alijibu: “ndiyo demokrasia yenyewe.”

Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wajumbe ndani ya ukumbi huo walionekana kurushiana maneno ya kushutumiana na kuonyeshana ishara za kudharauliana.
Avemaria Semakafu, akirushiana maneno na mjumbe mwingine Abdallah Juma (CUF) ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, walisuluhishwa na wajumbe wengine huku Juma akitolewa nje.
Awali kabla ya kuanza kwa kikao cha jioni, wabunge ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitishia kwamba wangesusia kuingia kwenye kikao hicho kwa ajili ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni.

Walisema kuwasilishwa kwa taarifa hiyo kabla ya Rais kulizindua Bunge hilo ni uvunjaji wa sheria na ukiukwaji wa kanuni za Bunge hilo.