Monday 28 April 2014

 MZOZO WA KIDIPLOMASIA
 KATI YA KENYA NA SOMALIA


Mzozo wa kidiplomasia unanukia kati ya Kenya na Somalia baada ya polisi kumkamata kimakosa mmoja wa maafisa wakuu wa ubalozi wa Somalia nchini Kenya Siyad Mohamud Shire .

Tayari balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Ali Nur ameitwa na serikali yake kueleza matukio yanayoambatana na kukamatwa kwa raiya wa asili ya kisomali ambao serikali inasema baadhi yao hawana vibali vya kuishi nchini.

Maafisa wa polisi nchini Kenya wamekuwa wakiendelea na msako wao dhidi ya wahamiaji haramu na wale wanaoshukiwa kushiriki matendo ya kigaidi na uhalifu.
Hata hivyo serikali ya Somalia imesikitishwa nao kwa kumkamata afisa wa ubalozi wa Somalia anayeshughulikia masuala ya kisiasa Siyad Mohamud Shire.

Kwa sababu hiyo Somalia imetuma taarifa katika vyombo vya habari ikisema kuwa waziri mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed amefanya mazungumzo na balozi wa Somalia nchini Kenya aliyefika Mogadishu hapo Jumapili kumweleza hatma ya raiya wa Somalia wanaoishi Kenya katika msako unaoendelea.

Japokuwa serikali ya Kenya kupitia kwa wizara ya usalama wa kitaifa imekuwa ikishikilia kuwa hailengi jamii yoyote katika kuwakamata raiya wa kigeni na kuwarejesha katika nchi zao ama kambi za wakimbizi.Taarifa hiyo imeanusha hilo na kusema maafisa wa polisi wamekuwa wakiwazuilia wasomali wengi na kuwatesa.

Tukio la kumnasa, Bwana Siyad Mohamud Shire limechukuliwa na serikali ya Somali kuwa ukiukaji mkubwa wa mkataba wa kidiplomasia.Inasemekana kuwa bwana Shire alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa muda licha ya kuwa na kitambulisho cha kazi.

Mkutano kati ya waziri mkuu wa wa Somali na balozi wa Kenya ulifanyika baada ya baraza la mawaziri kuandaa kikao kisichokuwa cha kawaida kujadili hali ilivyo Kenya.

Juhudi za kumpata waziri wa mambo ya nje wa Kenya balozi Amina Mohamed kueleza msimamo wa serikali hazikufaulu ila maafisa wa polisi walikataa kuzungumzia suala hilo wakisema kuwa litashughulikiwa na ngazi ya juu.

Polisi nchini Kenya walianza msako kote nchini wiki tatu zilizopita baada ya matukio mengi yanayoambatanishwa na ugaidi ama uhalifu kutokea huku zaidi ya watu kumi wakifariki baada ya milipuko kadhaa kutokea katika mtaa wa Eastleigh na maeneo jirani jijini Nairobi.

Kisichojulikana kwa sasa ni namna nchi zote mbili zitakavyoendelea kushirikiana kidiplomasia katika mazingira yaliyopo.

 

683 WAHUKUMIWA KIFO MISRI



Jaji wa mahakama nchini Misri, amewahukumu kifo watu 683 akiwemo kiongozi wa kundi la Muslim Brotherhood Mohammed Badie.
Mawakili wa watuhumiwa wanasema kuwa wateja wao walikabiliwa na makosa mengi yakiwemo, kushambulia kituo cha polisi mjini Minya mwaka 2013 ambapo polisi mmoja aliuawa.
Jaji huyo pia alibatilisha hukumu ya kifo iliyotolewa kwa watu 492 kati ya watu 529. Hukumu hiyo ilipitishwa mwezi Machi na sasa watahudumia kifungo cha maisha jela.
Kesi na kasi ya kuzisikilizwa kwa kasi hizo, imesababisha hasira na kukosolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Matifa UN.

Kadhalika shirika la Huma Rights Watch limelalamika kuwa kesi hizo zilisikilizwa tu kwa saa chache huku mahakama ikiwazuia mawakili kuwawakilisha washitakiwa.
Duru zinasema kuwa jamaa wa watuhumiwa waliokuwa wanasubiri nje ya mahakama walizirai baada ya kupokea taarifa za hukumu hiyo.

Mwezi jana shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, lililaani kesi hizo likisema kuwa zinakiuka sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.
Msemaji wa shirika hilo, Navi Pillay, alisema kuwa kesi hiyo ilikumbwa na makosa mengi ya utarataibu.

Maafisa wa utawala nchini Misri wamekuwa wakiwasaka na kuwakamata wapiganaji wa kiisilamu na wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood ambao walimuingiza mamlakani aliyekuwa Rais Mohammed Morsi ambaye baadaye aliondolewa na Julai.
Mamia wameuawa huku maelfu ya raia wakikamatwa.

Monday 7 April 2014

 DK BALALI AMVAA MAALIM SEIF

 

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema serikali ya mkataba haiwezi kuleta maendeleo nchini, bali ni kujidanganya na kujirudisha nyuma kimaendeleo.Aliyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho katika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti, visiwani hapa.


Alisema serikali tatu haziwezi kutatua kero za Muungano, hivyo CCM itahakikisha inaendeleza mfumo wa Muungano wa serikali mbili.
“Tunaendelea kupigania serikali mbili. Tunafanya hivyo kwa sababu tunaipenda Zanzibar na Tanzania yetu,” alisema Dk. Bilal.


Aliwataka Wazanzibar kutokuwa na hofu kwa kuwapo kwa serikali mbili kwamba watamezwa na Muungano na kuwatoa wasiwasi kuwa Muungano hautaibeza Zanzibar.
Alisema Tanganyika na Zanzibar zimeonyesha mfano mzuri wa kumkomboa Mwafrika kwa kuunganisha nchi mbili na kuwa Tanzania, kwani nchi nyingi zilikuwa zikitafuta umoja huo lakini zilishindwa.


 “Leo nini kutafuta mbinu za kuutaka kuuvunja Muungano ambao umepanua fursa kwa Wazanzibari bila ya Muungano Wazanzibari tungebanana, Muungano umetusaidia kufifisha uhasama uliokuwapo ndani ya Zanzibar na kujenga umoja na kusahau tofauti zilizopo,” alisema Dk. Bilal. 


Alisema Watanzania wengi wanataka serikali mbili, hivyo watahakikisha wanaendeleza mfumo wa serikali mbili, kwani katika watu 100 asilimia ya watu 86 hawana tatizo na Muungano uliopo.Alitahadharisha kuwa Muungano hauwezi kudumu bila ya serikali mbili katika nchi zenye tofauti ya ukubwa wa nchi moja ndogo na nyingine kubwa, ni lazima kuwapo na uwiano utakaodumisha Muungano.


 Alisema CCM haitishiki na vitisho vya upinzani vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwa lengo la kutaka kuuvunja Muungano.
Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi, Mwangi Kundya, alisema mfumo wa Muungano wa serikali mbili umetoa fursa ya kupanuka kwa soko la biashara, ajira na uwekezaji katika nyanja mbalimbali na kuimarisha huduma za kijamii ikiwamo elimu, afya na umeme.


 Alisema hotuba ya Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, aliyoitoa hivi karibuni katika mkutano wa hadhara ilionyesha kukata tamaa, baada ya kuona dereva makini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonyesha na kuweka bayana mitego yote ambayo wao walitamani Tanzania iingie. 


“Dereva huyo baada ya kuwaonyesha wajumbe wa Bunge la Katiba mitego hiyo sasa wana hakika hawawezi kufanikiwa nia yao ila wanaona bora litote tugawane mbao,” alisema Kundya.


Aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kutambua dhima waliyonayo ya kuulinda, kuutetea Muungano na kutotazama takwimu zilizotolewa kwa ufinyu wake, bali wazichambue na kuzitazama kwa upana wake ili kubaini Watanzania wanachokitaka.

RWANDA YAADHIMISHA MAUAJI YA KIMBALI



Rwanda inaadhimisha miaka 20 tangu kutokea mauaji ya kimbari mwaka 1994.
Watu laki nane waliuawa wengi wakiwa wa kabila la Tutsi na Wahutu wenye msimamo wa kadri. Wote waliuawa na watutsi wenye msimamo mkali.

Hii leo Rais Paul Kagame anatarajiwa kuwasha mwenge ambao utasalia hivyo kwa siku 100 ,kipindi ambacho mauaji ya kimbare yalifanyika.Mgogoro wa kidiplomasia umesababisha Waziri wa sheria wa Ufaransa, kujiondoa katika shughuli za kumbukumbu ingawa Ufaransa inasema kuwa balozi wake ataiwakilisha nchi hiyo.

Wengi wa waathiriwa wa mauaji ya Rwanda, walishambuliwa kwa mapanga kwa siku 100. Mauaji hayo yalianza Aprili mwaka 1994, punde baada ya kufariki kwa hayati Rais Juvenal Habyarimana.

Alifariki wakati ndege yake iliposhambuliwa katika anga ya Kigali na kudunguliwa.
Baadhi ya viongozi wa kidini walihusishwa na ghasia zilizofuata kifo cha Habyarmana.
Mauaji ya kimbari yaliisha mwezi Julai 1994 wakati chama cha RPF, kilichokuwa cha waasi wa Tutsi wakati huo, kilipoingia nchini humo kutoka Uganda na kuchukua uongozi wa nchi hiyo.

Kumbukumbu zinaanza kwa kuwekwa mauwa katika eneo la kumbukumbu ya mauaji hayo na kufuatiwa na kuwashwa kwa mwenge katika uwanja wa michezo wa Amahoro mjini Kigali.Mwenge huo umekuwa ukitembezwa katika nchi hiyo kwa miezi mitatu iliyopita

Viongozi wa kimataifa akiwemo waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair,aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na katibu mkuu wa UN Ban Ki-moon wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.Mnamo Jumapili mamia ya watu walihudhuria maombi kuwakumbuka maelfu waliouawa .

WAUKRAINE WANAOUNGA MKONO URUSI WAVAMIA MIJI


Rais wa Mpito wa Ukraine, Oleksandr Turchynov, ameitisha mkutano wa dharura wa maafisa wake wa usalama baada ya waandamanaji wanaounga mkono Urusi kuvamia na kuingia katika Ofisi za Serikali katika miji mitatu Mashariki mwa Ukraine.
Miji ya Donetsk,Kharkiv na luhansk, ndiyo imeshuhudia maandamano makubwa zaidi .
Waandamanaji walikabiliana na maafisa wa polisi na kuziweka bendera za Urusi katika makao makuu ya miji hiyo .

Wanadai wanataka kufanyike kura ya maoni ili na wao wafuate mkondo wa rasi jirani ya Crimea kujitenga na Ukraine .Serikali ya Kiev imeishtumu Urusi kwa kuchochea ghasia hizo iliipate fursa ya kuivamia Ukraine kijeshi kwa niya ya kuigawanya.

Kaimu waziri wa usalama wa taifa wa Ukraine Arsen Avakov amesema polisi tayari wamewaondoa waandamanaji ambao walikuwa wamepora silaha kutoka kwenye handaki kuu ya jimbo la Kharkiv.

Matukio hayo yamevutia hisia kali kutoka kwa mataifa jirani ,Rais wa jamhuri ya Czech Milos Zeman amesema kuwa vikosi vya NATO vinafaa kujiandaa kuivamia Urusi kwa kuingilia kijeshi mashariki mwa Ukraine.

Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amenukuliwa akiiambia gazeti la The Daily Telegraph kuwa Urusi inajaribu kuibua makanda yenye ushawishi barani Uropa.

WAASI NCHINI LIBYA WAKUBALI MAFUTA YAUZWE


Makubaliano yameafikiwa kuondoa kizuizi cha kusafirisha mafuta mashariki mwa Libya. Mauzo ya mafuta katika nchi za ng'ambo nchini humo yaliathirika pakubwa katika kipindi cha miezi minane iliyopita baada ya kufungwa kwa bandari zilizo katika eneo la mashariki linalotawaliwa na makundi ya wanamgambo.

Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyiwa katika jiji la Beghazi, Waziri wa Maswala ya Haki wa Libya, Salah Al-Maghani, alithibitisha kuondolewa kwa muda kwa vizuizi vya kuuza mafuta.
Vituo vya mafuta vya Hureiga na Zuetina vilivyo na uwezo wa kuzalisha mafuta mapipa 200,000 kwa siku hivi sasa vimesimamiwa na Serikali.Vituo viwili vilivyo vikubwa zaidi nchini humo vya Mashariki mwa nchi vya Ras Lanuf na Sidra vitafunguliwa kwa muda wa majuma machache yajayo, kulingana na Waziri.

Mapatano yaliafikiwa kati ya makundi ya wapiganaji yaliyosababisha kufungwa kwa vituo hivyo na kundi ambalo Serikali ililitaja kama "wapatanishi". Msemaji wa Waziri Mkuu ameambia BBC kuwa Serikali imekubali kuwalipa mishahara walinzi wa vituo hivyo vya mafuta.Juhudi za mwezi uliopita za kufikia mapatano ya kuanza kuuza mafuta tena katika vituo hivyo hazikufaulu.

Wale wanaozuia mafuta kuuzwa katika vituo hivyo wamekuwa wakilalamika kuwa sekta ya mafuta nchini Libya inakabiliwa na ufisadi mkubwa, lawama ambayo imekanushwa na maafisa wa Serikali.

Wapiganaji hao pia wamekuwa wakisema kuwa wakaazi wa Mashariki wanahitaji mapato makubwa zaidi kutoka kwa mauzo ya mafuta. Waziri wa Haki sasa anasema kuwa Serikali itachunguza lawama za ufisadi.

Libya imepata hasara ya zaidi ya Dola Bilioni tisa tangu kufungwa kwa vituo hivyo vya mafuta. Eneo la Mashariki ndilo linalozalisha kiwango kikubwa cha mafuta.