Tuesday, 25 February 2014

BUNGE LA KATIBA:WABUNGE WACHUKUA TSH MILIONI 129 KWENYE KIKAO

 

Wakati Bunge Maalum la Katiba likikutana kwa takribani nusu saa tu jana huku wajumbe wakiendelea kulipwa mamilioni ya fedha za kodi za wananchi, baadhi ya wajumbe wa wamelalamika na kupinga hali ya kuendelea kuahirisha vikao kwa kuwa hatua hiyo inasababisha matumizi makubwa ya fedha za umma na muda.

Bunge hilo limekuwa likiahirishwa tangu kuanza Jumanne iliyopita kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wajumbe kuzisoma kanuni pamoja na Kamati ya Kanuni kukamilisha kazi ya kuzichambua na kuwasilisha mbele ya wajumbe hao kwa ajili ya kuzijadili na kuzipitisha, kabla ya kuanza kujadili Rasimu ya Katiba.

Wajumbe hao walitoa madai hayo jana baada ya kikao hicho kufanyika kwa nusu saa na kuhairishwa wakidai kuwa huko ni kupoteza muda na rasilimali za Watanzania  bila sababu ya msingi.

Jana wajumbe takribani 629 waliokwisharipoti waliingia katika kikao kilichodumu kwa nusu saa kuanzia saa 3:00 asuhuhi hadi saa 3:30 na kuahirishwa. Kutokana na kila mjumbe kulipwa posho ya kikao ya Sh. 220,000 kwa siku, jana kwa dakika 30 zilitumika takribani Sh. 128,920,000 zilitumika kuwalipa wajumbe hao.

Baada ya Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Ameir Pandu Kificho, kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Ezekia Oluoch kutoka Vyama vya Wafanyakazi, alishauri siku mbili ambazo kamati itakuwa inaendelea na
kazi ya kuchambua kanuni, wajumbe waendelee na kazi ya kuijadili Rasimu ya Kanuni na maoni yapelekwe kwenye Kamati.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi bunge, Oluoch alisema
anashangazwa na uamuzi huo kwa kuwa unapoteza rasilimali na muda kwa kuwa tangu bunge hilo lianze Februari 18 mwaka huu hakuna jambo la msingi lililofanyika.

“Tungeambiwa hivi wala tusingewahi asubuhi, sasa tunaambiwa hadi Jumatano, siku zote hizi mbili tunafanya nini hapa Dodoma, ni matumizi
mabaya ya muda na rasilimali za Watanzania ambao ndiyo wanatulipa tunavyokuwa hapa,” alisisitiza.

Profesa Sospeter Muhongo alisema anashangaa kazi hiyo kushindwa kukamilika kwa siku hizo wakati walikuwa na mwongozo wa Rasimu ya Kanuni.

“Tusipokuwa waangalifu kuzingatia muda hii kazi haitaisha, kwa hiyo tukubaliane kwamba muda uliopangwa ukimalizika hakuna muda wa nyongeza kwa maelezo kwamba hawajamaliza, wananchi wanavyotuona tunaweza kujifurahisa tunafanya vitu vya maana sana, lakini watu wanatushangaa, kama kamati haiwezi unaitoa tunaendelea mbele,” alisema Profesa Muhongo ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Waziri wa Nishati na Madini.

Mjumbe mwingine, James Mbatia, alisema kanuni hizo ni ngumu na zimetengenezwa kama kanuni za kudumu za Bunge, jambo ambalo litawafanya wajumbe wengine washindwe kuzitumia.

“Fikiria mvuvi wa Muleba au Mwanza au mkulima ambaye hana uzoefu na mambo ya kibunge, hizi kanuni zinavyotengenezwa ni ngumu inaonyesha zinanakiliwa na kubandikwa wakifuata zile Kanuni za Kudumu za Bunge,” alisema na kuongeza:“Huu ni mkutano wa siku 70 na si bunge la kudumu. Zingepaswa ziwe kwenye karatasi mbili au tatu kwa kuwa tupo hapa kwa tendo la Katiba ambalo ni maridhiano.”

Alisema wabunge waliozizoea kanuni na ukumbi huo bado zinawasumbua, kwa mtu ambaye amekuja mara ya kwanza anawekewa masharti ya uvaaji ikiwamo kuvaa suti na kwamba tatizo kubwa lipo kwenye muundo wa Bunge lenyewe kwa kuwa wengi wa wajumbe wanatokana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Alisema Katiba si kwa ajili ya kizazi hiki bali vizazi vya miaka 100 ijayo, na kwamba mambo yanakuwa magumu kwa kuwa yanazungumzwa masuala ya nchi mbili kwa wakati moja.

Alisema mkutano huo ni wa siku 70 na ni sawa na mkutano wa kawaida, hivyo huwezi kutengeneza kanuni kama kanuni za kudumu kama mtu anayeandaa kanuni zitakazotumika kwa miaka 20 ijayo.

“Ni kanuni ngumu sana na zinachanganya, wanasahau kuwa Katiba ni suala la maridhiano, Bunge la Nepal lilitumia siku 90 kutengeneza Kanuni. Ukishakosea kwenye kanuni ndiyo basi, hizi zilitengenezwa na sekretarieti ambazo siyo wajumbe wa Bunge, zinapaswa kutokana nawajumbe wenyewe iwe ya kurasa mbili au tatu,” alisema.

Alisema kwa mwendo huo haoni dalili za Bunge hilo kuanza wiki hii wala ijayo na kwamba Watanzania wasikubali kuondoshwa kwenye hoja ya msingi na kupelekwa kwenye suala la posho.

Aidha, alikosoa kanuni hizo na kudai kuwa zimetengenezwa kwa hofu ya watawala na kwamba kuweka kanuni ya kumtoa nje mjumbe kwa siku kumi kwa Bunge la siku 70 ni ajenda isiyo na lengo jema.

Ally Kessy, ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), alisema kuahirishwa kwa vikao vya bunge tangu wiki iliyopita kwa madai kwamba wajumbe wanahitaji muda wa kutosha kusoma Rasimu hiyo ni kupoteza bure fedha za wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema haoni sababu ya bunge hilo kuahirisha vikao kwa hoja ya kutoa muda wa kutosha kwa wabunge kusoma vya Rasimu ya Kanuni.

“Haina sababu, busara inakosekana, Mwenyekiti wa Muda alikwishaunda kamati ya wajumbe 20 ya kumshauri, kwa nini sasa hali hii inaendelea kuwa hivi?” alihoji.

Alisema kwa upande wake ameisoma Rasimu hiyo kwa siku mbili tu na kuielewa, hivyo haoni kwa nini wajumbe wahitaji siku nyingi kuisoma na kuielewa.

Naye Mjumbe kutoka kundi la Vyama vya Wavuvi Zanzibar, Issa Ameir Suleiman, alisema: “Sisi tunaona hawatundei haki, lengo letu lilikuwa kuja na kufanya kazi moja kwa moja, lakini sasa tunaingia wiki ya pili bado hatujaanza kujadili Rasimu ya Katiba.”

Halima Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema maadalizi mabovu ya bunge hilo ndicho kilichosababisha mambo mengi kwenda kinyume cha matarajio yao.

Alisema kutokana na kazi kubwa na umuhimu wa kupitia kanuni na kuzichambua kwa kina kukosa maandalizi ndiyo sababu ya bunge hilo kushindwa kufanya kazi yake kwa wakati.

“Maandalizi ya kuchambua Rasimu ya Kanuni ni kazi kubwa na ilitakiwa kanuni zipitiwe mapema na kuchambuliwa kwa kina, lakini kutokana na kutokuwapo kwa maandalizi ya kutosha ndiko kunakozalisha ucheleweshwaji na utendaji kazi wa ovyo.

“Mimi siitetei kamati ambayo ilitakiwa kupitia kanuni, lakini kimsingi kanuni ni muhimu sana kuingia katika mjadala wa Katiba na kama kanuni itakuwa mbovu, ni wazi kuwa katiba nayo itakuwa mbovu na kanuni ikiwa nzuri ni wazi kuwa Katiba itakuwa nzuri kwa maana kanuni ndizo zinatoa mwongozo wa mjadala wa Katiba,” alisema.

  “Nina shaka kama kweli makundi ambayo yamekuja katika bunge yamekuja kwa ajili ya kuboresha Rasimu ya pili ya Katiba au wamekuja kwa ajili ya kupinga maoni ya Watanzania zaidi ya milioni 45 ambao walitoa maoni yao,” alisema na kuongeza:

 “Kanuni zimekuja na vipengele mbalimbali ambavyo vinatoa nguvu nyingi kwa Bunge kuliko Sheria kwa maana ya kutaka kuondoa maneno au mapendekezo ya Rasimu ya pili na kuweka mapendekezo mapya, jambo ambalo litakuwa ni kutowatendea haki Watanzania.

No comments:

Post a Comment