FAIDA ZA UYOGA MWILINI
Uyoga una vitamini na aina nyingi za madini. Virutubisho
vilivyothibitishwa kuwemo kwenye uyoga ni pamoja na Vitamin B2, B3, B5,
B6, B Complex pamoja na madini ya Potasiamu na ‘phosphorus’. Virutubisho
hivyo ni muhimu kwenye mwili wa binadamu katika kutoa na kuimarisha
kinga ya kupambana na ‘wavamizi’ maradhi.
Aidha, inaelezwa kuwa
uyoga ni chanzo kingine kizuri sana cha madini ya chuma (iron) na kopa
ambayo yanahusika kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wa usambaza wa hewa ya
oksijeni mwilini. Kupatikana kwa madini ya chuma na kopa kwenye uyago
ni jambo la kipekee ambalo linafanya mmea huo kuwa tofauti na muhimu.
Zikifafanuliwa nguvu za uyoga (Mashrooms) kwa mapana, inaelezwa kuwa
Vitamin B2 inayopatikana kwenye uyoga, ni tiba tosha kwa watu
wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kichwa unaojulikana kama ‘kipanda uso’.
Kiasi kidogo cha uyoga utakachokula kitapunguza kasi ya kuumwa kichwa
hicho.
Vilevile Vitamin B inasifika kwa uwezo wake wa kuzuia uchovu
wa mwili (fatique) na akili hasa wakati wa kazi nyingi. Vitamin B3
husaidia kupunguza kiwango cha mafuta mabaya ya Kolestrol mwilini,
wakati Vitamin B6 yenyewe huondoa hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au
moyo kusimama ghafla (Heart Attack).
Kama faida zote za kiafya
zilizo orodheshwa hapo juu zinazopatikana kwenye uyoga hazikutosha, basi
kuna faida nyingine ambayo inatokana na madini aina ya Zinc
yanayopatikana kwa wingi kwenye mboga hii. Zinc ina faida nyingi sana
mwilini na miongoni mwa faida hizo ni uimarishaji wa kinga ya mwili
(Immune System).
Zinc si muhimu tu kwa uimarishaji wa kinga mwilini,
bali pia kwa uponyaji wa haraka wa vidonda mwilini. Vilevile mboga hii
inasaidia sana ukuaji mzuri wa seli za mwili, huimarisha kiwango cha
sukari mwilini na kukufanya kusikia ladha na harufu ya vyakula na vitu
vingine ipasavyo.
Kwa ujumla uyoga ni mboga muhimu na inapaswa
kuliwa na kila mtu anayejali afya yake kutokana na faida zinazopatikana
humo. Kuanzia leo, jaribu kuweka uyoga katika orodha ya mboga unazonunua
kila wiki kwa ajili ya familia yako.
Bila shaka kwa wakazi wa miji
midogo na vijijini, mboga hii hupatikana kwa wingi wakati wa mvua na kwa
miji mikubwa kama Dar es Salaam, uyoga unaweza kupatikana kwenye masoko
maalum kama, Kariakoo, Kisutu na ‘super market’ mbalimbali.
No comments:
Post a Comment