FAIDA ZA MBEGU ZA MABOGA MWILINI
Mbegu za maboga zimesheheni protini na madini kadhaa kama vile chuma, kopa, maginizia, manganizi na zinki, mbegu za maboga zinakuwa mbegu bora na muhimu kutafuna kila wakati kama wewe ni mpenzi wa kutafuna-tafuna. Unaweza kutumia mbegu za maboga kama unavyotumia karanga katika kuongeza ubora wa chakula. Imethibitika pasipo na shaka kuwa mbegu za maboga zina faida lukuki kiafya na zina uwezo wa kukuepusha na magonjwa hatari:
UGONJWA WA MOYO:
Mbegu za maboga zina kiasi kingi cha madini aina ya maginizia (magnesium) ambayo huboresha utendaji kazi wa viungo vya mwili. Huimarisha usukumaji wa damu kwenye moyo, huimarisha ukuaji wa mifupa na meno, huifanya mishipa ya damu kupitisha damu kwa urahisi na hufanya upatikanaji wa haja kubwa kuwa laini.
KINGA YA MWILI:
Mbegu za maboga pia zina kiasi kingi cha madini ya Zinki (Zinc). Madini haya yana faida nyingi mwilini, ikiwemo kuimarisha kinga ya mwili, kuboresha ukuaji na uundaji wa chembechembe hai za mwili, kuboresha usingizi, kuboresha ladha mdomoni na harufu, huboresha afya ya macho na ngozi, hurekebisha sukari na huboresha nguvu za kiume pia.
Upungufu wa madini ya ‘Zinc’ mwilini una uhusiano mkubwa sana na matatizo ya kuzaa watoto njiti, kuota chunusi nyingi mwilini, watoto kuwa na uwezo mdogo darasani kimasomo na matatizo mengine mengi ya kimwili na kiakili.
MAFUTA YA OMEGA 3:
Omega 3 ni moja kati ya mafuta muhimu sana mwilini. Jamii ya karanga pamoja na mbegu za maboga ni miongoni mwa mbegu zenye kiasi kingi cha mafuta aina hii. Hivyo ulaji wa mbegu za maboga utakuwezesha kupata kirutubisho hiki muhimu katika mwili wako na kukupa faida za mafuta haya ambazo ni nyingi.
KIBOFU CHA MKOJO:
Tangu enzi za mababu zetu, mbegu za maboga zimetumika kuimarisha afya ya wanaume kutokana na kuwa na kiasi kingi sana cha madini aina ya Zinc ambayo ni muhimu sana kwa afya ya kibofu cha mkojo. Mbegu za maboga pamoja na mafuta yake, yote kwa pamoja hutoa kinga kwenye kibofu kupatwa na matatizo ya kiafya, yakiwemo yale ya saratani ya kibofu.
KINGA DHIDI YA SARATANI:
Imethibitika kwamba watu ambao hula mlo wenye kiasi kingi cha mbegu za maboga wamegundulika kuwa na hatari ndogo sana ya kupatwa na saratani za tumbo, matiti, mapafu na kibofu.
No comments:
Post a Comment