KENYA YAPELEKA WANAJESHI SUDANI KUSINI
Kamati Kuu ya Usalama Nchini Kenya imependekeza kwa
bunge liidhinishe nyongeza ya idadi ya wanajeshi wake wa kudumisha
amani walioko nchini Sudan Kusini, chini ya kivuli cha Umoja wa Mataifa,
kwa majeshi 310.
Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Rais Uhuru
Kenyatta imesema imechukua hatua hiyo kufuatia ombi la baraza la usalama
la Umoja wa Mataifa lililofanywa Desemba 24, mwaka jana.
Katika
taarifa iliyotolewa na msemaji wa ikulu ya Nairobi usiku wa kuamkia
leo, kamati hiyo ambayo imekutana kwa mara ya kwanza tangu Rais Uhuru
Kenyatta kuanza utawala wake mwaka mmoja uliopita ilisema kuwa Kenya
itawatoa wanajeshi wengine ili kufanya idadi ya wanajeshi wake walioko
Sudan Kusini kufikia 1,000.
Taarifa hiyo ilieleza wazi kuwa wanajeshi wa Kenya wanaingia huko chini ya Umoja wa Kimataifa na wala sio kama taifa huru.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mapigano ya
wenyewe kwa wenyewe kuanza kati ya jeshi la Sudan Kusini linalomuunga
mkono Rais Salva Kiir na wanajeshi waasi wanaomuunga mkono makamu wa
rais wa zamani Daktari Riek Machar, Uganda iliwatuma wanajeshi nchini
humo kuunga mkono Rais Salva Kiir.
Katika taarifa hiyo kamati ya usalama nchini Kenya ilisema kuwa hali ya usalama nchini Sudan Kusini imeathiri Kenya.
Wakimbizi wengi wametorokea Kenya, taifa
ambalo kwa hivi sasa linakabiliwa na matatizo yake mengi ya kiuslama
kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wa Somalia .
Miongoni mwa matatizo ya kiusalama yaliyotajwa
katika taarifa hiyo ni mapigano kati ya makabila mbalimbali nchini Kenya
na pia hatari ya mashambulizi ya kigaidi katika uwanja wake wa
kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Mkutano huo wa usalama ulioongozwa na Rais Uhuru
Kenyatta ulisema usalama katika uwanja huo utaimarishwa kwa kuimarisha
mitambo ya kuwapekua wasafiri wa kimataifa.
Nairobi ni kitovu kikubwa cha usafiri kwa
watalii na wafanyabiashara katika eneo zima la ukanda wa mashariki na
upembe wa Afrika.
Rais Uhuru Kenyatta hii leo atasafiri hadi mji
Mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kama hatua mojawapo ya viongozi wa eneo la
Afrika Mashariki la kutafuta suluhu la mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
yanayoendelea nchini humo.
No comments:
Post a Comment