MAREKANI YAIONYA URUSI KUHUSU UKRAINE
Hatua hii inawadia siku moja tu baada ya Urusi kuamuru kufanyika kwa
mazoezi ya kijeshi yanayoshirikisha askari wapiganaji laki moja na nusu
kwenye mpaka wake na Ukraine .
Kujitokeza kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine kumeimarisha uhasama ulioko kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John
Kerry amesema kuwa Urusi inapaswa kukubali ushauri ya kwamba mataifa ya
kigeni yasiingile mambo ya ndani ya Ukraine.
Alisema kuwa kujiingiza kijeshi katika hali ilivyo nchini Ukraine kwa hivi sasa ni kosa kubwa.
Mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya muungano wa
NATO wametoa taarifa ambapo wamesema kuwa wanachama wake wataendelea
kuunga mkono uhuru na hadhi ya taifa la Ukraine.
Serikali ya Marekani imesema kuwa imetenga mbinu
mbalimbali inazotazamia kutumia kuimarisha Ukraine kiuchumi, huku
kukiendelea kuwa na hofu kuwa huenda taifa hilo likashindwa kuendelea
kulipa madeni yake.
Kwa wakati huu msaada wa kijeshi pekee kwa
Ukraine hautoshi kwani taifa linalotaka kusaidia lazima kwanza
liimarishe hali ya kukubaliwa kwake katika taifa hili ambalo
limegawanyika kwa imani yake kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.
Wabunge kadhaa wa Marekani wameonya kuwa Jumuiya
ya Ulaya na Marekani wasipotoa msaada wa pesa taslimu Urusi huenda
ikafanya hivyo.
No comments:
Post a Comment