Friday, 14 February 2014

OKWI SASA RUKSA YANGA



 

Imethibitishwa kwamba yule kiungo nyota Mganda, Emmanuel Anorld Okwi ni mchezaji halali wa Yanga sasa.
Shirikisho la Soka Tanzania TFF limeelezea kuhusiana na habari hii njema kwa mashabiki wa Yanga baada ya kupata ufafanuzi kutoka kwa shirikisho la kimataifa Fifa.

TFF ndiyo waliosimamisha usajili wa Okwi, saa chache kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini jana wamethibitisha anaweza kuanza kuitumikia Yanga ambayo ilimwaga zaidi ya dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 160) kumpata.

Okwi, aliyetua Yanga wakati wa dirisha dogo ambapo sababu kuu kwa mujibu wa TFF ni kuwa, kulikuwa na kesi tatu zinazohusu usajili wake kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (Fifa), alizuiwa ili TFF ipate ufafanuzi kutoka Fifa.

Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, amesema kuwa, tayari wamepokea ufafanuzi kutoka Fifa ambapo Okwi ameruhusiwa kuitumikia Yanga baada ya kuthibitisha usajili wake kutoka SC Villa ya Uganda kwenda Yanga ulikuwa halali.

“Fifa tayari wametutumia mrejesho kuhusu Okwi kama tulivyowaomba, kwa sasa Okwi yupo huru kuichezea timu yake, hatua hiyo ni baada ya Fifa kuridhika na uhamisho wake kuwa halali kutoka Villa kwenda Yanga.
“Kila kitu kipo Ok na tayari viongozi wa Yanga tumewataarifu juu ya hilo na hatuna shaka naye tena,” alifafanua Mwesigwa.
Alipoulizwa Katibu wa Yanga, Beno Njovu, alikiri kupokea barua kutoka TFF huku akiongeza kuwa barua hiyo imebainisha kuwa TFF ipo kwenye mchakato wa kumtafutia leseni yake kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ili acheze pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga inashiriki.

“Kweli tumepokea barua kutoka TFF jana wakituambia kuwa Okwi ameruhusiwa na Fifa kuichezea Yanga kwenye michuano ya ndani na nje, pia barua hiyo imeeleza kuwa TFF inafanya jitihada za kumtafutia leseni ya Caf kwa ajili ya kucheza mchezo ujao dhidi ya Al Ahly iwapo Yanga itafuzu kufika raundi ya kwanza. Pia TFF wametupongeza kwa kuwa wavumilivu siku zote hizi,” alisema Njovu.

Yanga itacheza mchezo wake wa marejeano dhidi ya Komorozine ya Comoro, kesho Jumamosi ikiwa tayari na faida ya ushindi wa mabao 7-0 kwenye mchezo wao wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam.

Okwi alipohojiwa jana alisema: “Nimepata taarifa kuhusiana na hilo, ilikuwa ni vigumu kidogo kuamini, lakini baadaye nikathibitishiwa.
“Kwa kweli nimeshukuru sana, nimenyoosha mikono na kumshukuru Mungu ambaye ametenda na haki imepatikana. Sasa najiweka sawa kwa ajili ya kurejea na kuungana na wenzangu.”

Utata wa usajili wa Okwi unatokana na Simba kumuuza ‘bure’ kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia, ambapo hakudumu muda mrefu, akarejea kuichezea SC Villa ya Uganda kwa mkopo maalum kisha kutua Yanga, lakini Simba ambayo ilimuuza kwa dola 300,000 (Sh milioni 480) haijapata hata shilingi 10 mpaka leo.

No comments:

Post a Comment