MSAJILI WA VYAMA NA SAKATA LA KUTEKWA PAROKO
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imeingilia kati sakata la
kutekwa na kujeruhiwa kwa Paroko wa Kanisa la Orthodox, Parokia ya
Mtakatifu Basili Mkuu, Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Padri Costantino
Mbilinyi (36), ikisema kulifumbia macho ni kuruhusu matukio ya uvunjifu
wa amani na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Msajili Mkuu, Jaji Francis Mutungi, alisema kuwa ofisi yake inafuatilia tuhuma za kutekwa kwa paroko huyo maarufu kama Father Kizito, ambaye anawahusisha wanachama wa CCM, akidai pia walimwekea pilipili na sindano ya kushonea viatu mfukoni.
Aidha, ofisi hiyo imesema wanamsaka mgombea ubunge wa Chama cha Chausta, Richard Minja, ambaye alichukua fomu kuwania nafasi hiyo, lakini ameshindwa kutokea hadharani na kuwapa ushirikiano ikiwamo kuhojiwa na kuendelea na mikutano ya kampeni ambayo itasitishwa Machi 15.
"Tumewahoji wagombea wa vyama vyote viwili vya CCM na Chadema kuhusu mwenendo mzima wa kampeni zinazoendelea katika jimbo la Kalenga ili kupata maoni yao na taarifa nyingine kuhusu matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa sheria...Hili la Paroko kutekwa na kujeruhiwa tunalifuatilia kujua ukweli na tutachukua hatua stahiki ili kutoa uwanja sawa wa haki kwa kila upande," alisema Nyahoza.
Father Kizito, anadaiwa kukamatwa na kutekwa na watu hao kabla ya kujeruhiwa juzi, majira ya saa 11 jioni kwa madai ya kukisaidia Chadema.
Ofisi hiyo imesema itakutana na wadau wake ili kueleza nia yake ya kuvilazimisha vyama vyote vyenye vikosi vya ulinzi vya vyama kuvivunja mara moja kabla ya kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani kwa kuwa chanzo cha machafuko au uvunjifu wa amani katika chaguzi hizo ni vikosi hivyo.
"Tunavitaka vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na visivyo na usajili wa kudumu, havitakiwi kuendelea kuwa na vikosi vya ulinzi kwa madai ya kujilinda wenyewe kutokana na Jeshi la Polisi kudaiwa kushindwa kutoa ulinzi wanaoutaka na badala yake vinaamua kujilinda vyenyewe.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na tuhuma hizo kuwasilishwa kwa Msajili wa vyama vya siasa, alidai kwamba tukio hilo ni la kupangwa na limetengenezwa na Chadema.
"Wanataka kupotosha maana wakati kiongozi huyo wa dini anakamatwa CCM hawakuwepo eneo hilo na waliomkamata si viongozi na wala si makada wetu na kwa maana hiyo tukio lenyewe ni la kupangwa na Chadema.
Wanatengeneza kwa sababu huyo bwana (Father Kizito) alikuwa na gari la M4C...Na itapendeza sana kama utawauliza pia na wananchi wenyewe ni nini kilichotokea. Hayo ni mambo ya kiuzushi," alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhan Mungi, alisema kuwa Polisi imeanza uchunguzi wa tukio hilo na iwapo tutabaini kuna chama kimehusika katika tukio hilo kwa lengo la kujinufaisha kisiasa kwa wapiga kura tutachukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika," alisema.
Katika tukio hilo, Paroko huyo anadai alipoteza kofia yake ya kitawa (Kikuli) kutokana na kipigo ambacho anadai pia amehalilishwa kama kiongozi wa dini anayehudumu katika makanisa ya Nyamihuhu na Nzihi. Dhehebu hilo lina makanisa 19 katika jimbo la Kalenga
No comments:
Post a Comment