WAPINZANI WAFUNGWA MAISHA BURUNDI
Wanachama kadhaa kati ya sitini wa chama cha upinzani
nchini Burundi MSD waliofikishwa mahakamani leo , wamehukumiwa kifungo
cha maisha jela.
Hii ni baada ya serikali kuwatuhumu kwa kosa la kusababisha vurugu na kupanga njama ya mapinduzi dhidi yake.
Wengine bado wanasubiri hukumu huku kesi zao zikiendelea.
Walikamatwa baada ya kuhusishwa na purukushani iliyotokea tarehe nane mwezi Machi baina ya wafuasi wa chama hicho na polisi.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa leo katika mahakama ya jiji la Bujumbura.
Mnamo siku ya Jumatatu, Umoja wa mataifa na
Muungano wa Ulaya zilielezea wasiwasi kuhusu mvutano wa kisiasa unaozidi
kutokota kati ya serikali na vyama vya upinzani nchini Burundi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,
alilaani hali ya kisiasa nchini humo,akisema kuwa serikali inakandamiza
uhuru wa kisiasa, uhuru wa kuongea na watu kukutana.
Bwana Ban alisema kuwa sio jambo zuri kwa polisi kuingilia maandamano ya upinzani.Agizo hili lilitokana na ghasia za kisiasa kati ya wanaharakati wa upinzani na polisi mapema mwezi huu.
Wiki jana mahakama nchini humo ilimchukulia
hatua kiongozi wa chama cha upinzani (Movement for Solidarity and
Development party) ambaye pia ni mwandishi habari wa zamani, Alexis
Sinduhije na wanaharakati wengine 71 kwa madai ya njama ya mapinduzi.
Serikali pia ilisitisha shughuli zote za chama
cha upinzani cha MSD kwa kipindi cha miezi minne baada ya kukishutumu
kwa kuzua vurugu.
Chama hicho kimekanusha kusababisha vurugu zozote.
No comments:
Post a Comment