OBAMA ATAKA WACHUNGUZI WATUMWE UKRAINE
Rais Obama ametangaza mapendekezo ambayo huenda
yakatoa suluhu kwa mzozo wa Ukraine, ikiwemo kuwatuma wachunguzi wa
kimataifa na kuanzishwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na
serikali mpya mjini Kiev.
Bwana Obama amejadili swala hilo kwa njia ya simu na chanzela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Wachunguzi hao watalenga kulinda haki za watu wa kabila la Urusi
waliopo katika jimbo la Crimea; na kwa upande wake Urusi itahitajika
kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo hilo. Pendekezo hilo huenda
likajadiliwa pembezoni mwa mkutano utakaofanyika nchini Ufaransa
(Jumatano) ambao utawaleta pamoja wajumbe kutoka Marekani, Urusi na
kwingineko kwa ajili ya kuijadili Lebanon.
Hapo awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni
wa Marekani John Kerry, amelaani kile amekitaja kuwa kitendo cha
uchukozi kutoka Urusi dhidi ya Ukraine. Wakati wa ziara yake mjini Kiev
ambapo aliweka shada la maua kuwakumbuka waandamanaji waliouwawa mwezi
uliopita, bwana Kerry ameshutumu Moscow kwa kutumia uongo na vitisho
kuficha ukweli.
Mwandishi wa BBC Sarah Reinsford aliyepo mjini
Kiev amesema kuwa wakati akiweka shada la maua katika maeneo walikouwawa
mamia ya waandamanaji mjini humo, John Kerry alikaribishwa na umati wa
watu waliokuwa wakiomba msaada wa marekani.
Na hilo ndilo lililomleta hapa; kutoa msaada wa
hali na mali na pia wa kisiasa kwa serikali ya mpito ya Ukraine, na pia
ahadi ya msaada wa kifedha na wa kiufundi kusaidia katika kuimarisha
uchumi, amesema mwandishi wetu.
Lakini zaidi ya yote bwana Kerry ameleta ujumbe kwa Moscow.
" Nadhani ni bayana kwamba Urusi imekuwa
ikifanya bidii kubuni dhana ya kuiwezesha kutekeleza uvamizi zaidi.
Urusi imezungumzia raia wachache wanaozungumza kirusi ambao
wamezingirwa.
Ukweli ni kwamba hawajazingirwa! Ukweli ni kwamba serikali
mpya ya Ukraine imewajibika ipasavyo kwa kuhimiza utulivu na kujiepusha
na uchokozi," amesema Bwana Kerry.
Hakuna ushahidi, amesisitiza, kwa madai ya
urusi kwamba wanajeshi wake wanalinda raia wanaozungumza lugha ya kirusi
nchini Ukraine akiishutumu moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha
ukweli.
Katika karne ya ishirini na moja, bwana Kerry
ameonya, haiwezekani kuvamia taifa jingine na kisha kuamrisha matakwa
yako yatekelezwe kwa kutumia mtutu wa bunduki.
Na kisha akamhimiza rais
Putin kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo la Crimea na kushughulikia
malalamishi yake kupitia njia za kisheria na amani.
La sivyo, ameonya, kwamba Urusi itakabiliwa na vikwazo zaidi vya kiuchumi na kisiasa.
No comments:
Post a Comment