WABUNGE WATAMANI LISSU KUWA WAZIRI
Wajumbe wawili wa Bunge Maalum la Katiba, ambao ni wabunge wa CCM, Abdul
Marombwa (Kibiti) na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro) kwa nyakati
tofauti wamempongeza Tundu Lissu, kwa kujibu maswali na kutoa ufafanuzi
mzuri wa masuala ya kanuni kama vile waziri.
Lissu Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema) na sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo, aliwakosha wajumbe wengine kwa kujibu maswali ya wajumbe kuhusu sheria na kanuni kwa uelewa mkubwa.
Ole Sendeka alitoa pongezi zake bungeni juzi jioni wakati wabunge wakiendelea na semina yao kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.
“Kwanza nakupa pongezi sana kwa umahiri wako wa kujibu na kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali ya kisheria na kanuni, ningependekeza mheshimiwa rais angekuteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria,” alisema.
Marombwa alimpongeza Lissu wakati akizungumza nje ya ukumbi wa bunge siku mbili kabla ya Sendeka kufanya hivyo.
“Amekuwa akijibu maswali ya wajumbe bila kuonyesha upendeleo au misimamo ya chama chake.
“Anajibu na kutoa ufafanuzi mzuri kama vile waziri, mara zote haonyeshi kuegemea upande wa chama chake kama inavyokuwa wakati wa mijadala ya Bunge la kawaida,” alisema.
Moja ya hoja ambazo Lissu alizitolea ufafanuzi ni hoja ya kuwa na ‘mgeni rasmi’ ambayo katika tafsiri ya Rasimu ya Kanuni hiyo imesema ni Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais wa Zanzibar atakayealikwa na Mwenyekiti kulihutubia Bunge Maalum.
Akizungumzia matarajio yake katika Bunge Maalum la Katiba, alisema wanaweza kuipata Rasimu inatakayopendekezwa kama wajumbe wataondoa tofauti na itikadi za kivyama.
No comments:
Post a Comment