Thursday, 13 March 2014

 AK 47 ZAKAMATWA NCHINI TANZANIA

 

MKUU WA MAJESHI NCHINI ERNEST MANGU

Watu  wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukamatwa wakiwa na bunduki mbili za kijeshi aina ya AK 47 baada ya kuingia katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mkoani na nchi jirani Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam wakitokea mkoani Tabora.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni kituoni hapo na kuwavuta watu waliokuwa kituoni na maeneo ya jirani baada ya polisi kufyatua risasi hewani katika harakati za kuwatia mbaroni watuhumiwa hao.

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda walisema waliwaona polisi wakiwasili kituoni  wakiwa wamevalia kiraia na kuingia katika eneo la kuegesha teksi.

Mmoja wa mashuhuda hao, alisema baada ya kufika eneo hilo polisi waliwaomba madereva wa teksi wasogeze magari mbali na kuwaeleza kwamba watakaposikia milio ya risasi wasishtuke kwa kuwa polisi wako kazini.


Naye dereva teksi ambaye alikataa kutaja jina lake alisema: “Wale (watuhumiwa) walikuwa tayari mtegoni kwani mmoja wao alipokuwa anashuka alikuwa ameshika begi lenye rangi nyeusi, askari walipomuona  wakafyua risasi mbili hewani, jamaa alitupa begi na kukimbia,” alisema.


Hata hivyo, Shuhuda huyo alieleza kuwa mtuhumiwa huyo hakufika mbali kwani alikamatwa na askari kwa msaada wa wananchi huku mwenzake akikamatwa na polisi baada ya kutajwa na mtuhumiwa wa kwanza.


“Tulipowauliza walisema walikuja kwa ajili ya kufanya biashara kwani wao walinunua bunduki hizo kwa Sh. milioni moja na mteja wao alitakiwa kuzinunua kwa Sh. milioni mbili taslimu kila moja,” alisema dereva huyo akimkariri mtuhumiwa wa kwanza.


Habari zaidi zilieleza kuwa baada ya polisi kuwatia mbaroni watuhumiwa hao, waliwapeleka katika kituo cha polisi cha Urafiki.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Konondoni, Camillius Wambura, alipoulizwa kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, hakutaka kutoa maelezo zaidi, lakini alithibitisha kutokea na watuhumiwa hao kutiwa mbaroni.


Wambura alisema kwamba Jeshi la Polisi linawashikilia na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.


“Ni kweli wamekamatwa watuhumiwa wawili, ila polisi tutatoa tarifa Ijumaa (kesho) kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, atakapo zungumza na waandishi wa habari,” alisema Kamanda Wambura.


Kumekuwa na mlolongo wa matukio makubwa ya kutumia silaha nchini, hali ambayo imesababisha kuzorota kwa usalama hasa katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Kagera ambako silaha nzito za kivita hutumika kuteka magari.


Vyanzo vya silaha hizi inaelezwa ni kutoka nchi jirani ambako kutokana na kukosekana kwa amani na kudumu kwa mapigano ya mara kwa mara baina ya waasi na vikosi vya serikali, kumesababisha kuzagaa kwa silaha katika mipaka ya Tanzania na nchi hizo kiasi cha kufanya upatikanaji wake kuwa rahisi kwa watu wenye nia ya kufanya uhalifu wa silaha.
Ends

No comments:

Post a Comment