MISHAHARA LAZIMA IPUNGUZWE ASEMA KENYATTA
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ameamuru maafisa wakuu
watendaji wa mashirika ya serikali kukubali mishahara yao kukatwa kwa
asilimia 20, la sivyo waachishwe kazi.
Akiongea kwenye kongamano la kitaifa kuhusu
gharama kubwa ya matumizi ya serikali, Rais Kenyatta alisema kuwa hatua
yake na naibu wake pamoja na baraza la mawaziri kupunguza mishahara yao
kwa asilimia 20 haikuwa kwa sababu ya kufurahisha watu.
Kadhalika Kenyatta ameongeza kusema
kuwa uchumi wa nchi hauwezi kuwa mzuri ikiwa kila mtu anataka nyongeza
ya mishahara badala ya kuzingatia kupunguza gharama ya maisha na
uzalishaji wa bidhaa.
''Wakuu wa mashirika ya serikali watatakiwa
kukubali mishahara yao kupunguzwa kwa asilimia 20. Kuna wakenya ambao
wanaweza kushikilia nyadhifa hizo kwa pesa ndogo ikilinganishwa na zile
wanazopata wakuu hao,'' aliongeza kusema Kenyatta.
Kenyatta amesema matumizi ya pesa za serikali ni
ya juu mno na kwamba hayawezi kudhibitiwa ikiwa baadhi ya wafanyakazi
wa sekta ya umma wataendelea kupata mishahara mikubwa.
Rais alisema lazima safari za kwenda nje ambazo
zinafanywa na baadhi ya wafanyakazi wa serikali, kupunguzwa. Wakati
huohuo, Rais aliwataka wabunge kukubali mishahara yao kukatwa kwani ni
baadhi ya wabunge anaopokea mishahara mikubwa duniani.
Swala la mishahara ya wabunge ni swala tete sana nchini Kenya.
Rais Kenyatta, alisema kuwa serikali inatumia
kati ya dola dilioni 4.6 kwa mishahara ya wafanyakazi wa umma na kutumia
dola bilioni 2.3 kwa maendeleo.
No comments:
Post a Comment