AGIZO LA MAGUFULI LAPUNGUZA MSONGAMANO DAR
Msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro, umepungua kutokana na
baadhi ya barabara zilizokuwa zimefungwa kufunguliwa na kampuni ya
Strabag inayojenga barabara hiyo.
Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, kuiagiza kampuni hiyo ifungue barabara zilizokamika wakati wakiendelea na ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (Darts ili kupunguza foleni.
Barabara ya Ubungo hadi Kimara jana ilikuwa imepungua foleni kulinganisha na siku za nyuma, baada ya barabara nyingine kufunguliwa.
Kabla ya Dk. Magufuli kutoa agizo hilo, wakazi wa Mbezi hadi kimara walikuwa wakilazimika kukaa barabarani kwa saa tatu hadi nne ili kuvuka mataa ya ubungo kutokana na ufinyu wa barabara.
Tatu Almasi, mkazi wa Kiluvya, alisema kabla ya kufunguliwa kwa barabara hizo hali ilikuwa mbaya na hivyo kumlazimika kila siku kukodi pikipiki ili kuwahi kazini.
“Foleni haijaisha ila kwa sasa imepungua kwa kiasi siyo kama walivyokuwa wamefunga hizi barabara za pembeni, tulikuwa tunatumia gharama kubwa na muda mwingi kwenda kazini,” alisema Tatu.
Februari 27, mwaka huu, Dk. Maghufuli aliagiza kufunguliwa kwa barabara hizo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumiaji.
Ujenzi wa mabasi yaendayo kasi umekamilika kwa asilimia 55 na utagharimu Sh. bilioni 288.8 na unatarajia kukamilika mwakani.
No comments:
Post a Comment