SITTA AMPINGA WARIOBA
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ametofautiana na
kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba, ambaye amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema Bunge hilo
halina mamlaka ya kurekebisha Rasimu ya Katiba mpya.
Badala yake, Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ameungana na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, akisema Bunge hilo lina uwezo huo.
sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM) alisema ni jambo lisiloingia akilini na ambalo kamwe halikubaliki kwamba, Bunge hilo liitishwe na Rais kisha likutane kwa ajili ya kuihariri rasimu hiyo.
Alisema kazi ya kuihariri rasimu hiyo ni ya waandishi na kwamba, ilitakiwa ifanywe mapema, kabla Rais hajaliitisha Bunge hilo.
Sitta alisema maoni yaliyomo kwenye rasimu hiyo yalitolewa na watu 350,000 kati ya wananchi milioni 45 waliopo nchini, hivyo hayawezi kamwe kuwa ya mwisho kwa maana yoyote ile ya kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Sitta, Bunge lina uwezo wa kuvipitia vifungu vyote vya rasimu hiyo na kuvifanyia kazi kabla ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya ama kuikubali au kuikataa.
“Bunge huwa lina uwezo wa kuangalia vipengele vyote na kuvifanyia kazi,” alisema Sitta.
Alisema katika hilo, upo ushauri uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yule wa Zanzibar kuhusu uwezo wa Bunge hilo kufanyia kazi rasimu hiyo, ambao ndiyo watakaoufuata.
“Haiingii akilini wawakilishi 629 kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wakutane katika Bunge ili kazi yao iwe ni kuifanyia uhariri Rasimu ya Katiba. Akili haikubali kabisa. Ni mambo ya ajabu.”
Kauli hiyo ya Sitta imetolewa takriban mwezi mmoja baada ya Jaji Werema kusema wajumbe wa Bunge hilo wana mamlaka ya kurekebisha Rasimu ya Katiba, lakini hawawezi kuondoa misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya kijamii.
Jaji Werema alisema hayo bungeni, Februari 19, mwaka huu, wakati akitoa majibu ya hoja mbalimbali za wajumbe wa Bunge hilo baada ya kuwafafanulia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2012.
“Fanyeni mnavyotaka, lakini si kuondoa misingi ya kitaifa. Hamna mamlaka ya kuondoa misingi mikuu ya kitaifa,” alisema Jaji Werema.
Alisema misingi hiyo inaihusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge hilo, hivyo si sahihi kueleza kuwa ilikuwa maalumu kwa tume pekee.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kifungu cha tisa (2) katika kutekeleza masharti ya kifungu kidogo cha kwanza, tume itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii na kuhifadhi na kudumisha mambo tisa.
Inayataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwapo Jamhuri ya Muungano; uwapo wa serikali, Bunge na Mahakama; mfumo wa kiutawala wa kijamhuri na uwapo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Vingine ni umoja wa kitaifa, amani na utulivu na uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalumu kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura.
Inataja pia ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu; utu, usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria na uwapo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.
“Watu waliohojiwa kule ni wachache na nyinyi humo ndiyo wawakilishi wa wananchi, hivyo si vizuri kwa jicho la kisheria kutofanya marekebisho,” alisema Jaji Werema.
Aliongeza: “Nyinyi ni wawakilishi wa wananchi, mnayo kazi ya kuikarabati na kuijadili, na baadaye kuipeleka kwa wananchi kwa kura ya maoni. Kusema Bunge hili halina mamlaka ya kubadilisha lolote si sahihi. Hili ni swali linaloulizwa na wananchi huko.”
Alisema kama isingekuwa hivyo, basi rasimu hiyo ingeishia kwa Bunge Maalumu tu na wajumbe wake kufanya uamuzi. Lakini ndiyo maana inajadiliwa na kisha kupelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.
Kauli ya Jaji Werema inatofautiana na ile, ambayo imekuwa ikitolewa na Jaji Warioba kwamba, Bunge hilo halina mamlaka ya kurekebisha rasimu hiyo.
Jaji Warioba alisema litakuwa jambo lisilo la kawaida kwa Bunge hilo kubadili hoja ya msingi iliyopo kwenye rasimu hiyo, akisisitiza kuwa jukumu lake ni kuifanyia maboresho.
Alisema hayo wakati akihutubia mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wa tafakuri na maridhiano kuelekea Katiba Mpya, Februari 12, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Alisema madaraka ya Bunge Maalumu yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika Kusini, Namibia na Cambodia, bunge maalumu lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika rasimu ya katiba.
“Katika mazingira haya, bunge maalumu lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika rasimu ya katiba… lilikuwa na madaraka ya kuachana na rasimu ya katiba na kuandika rasimu mbadala,” alisema Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.
Jaji Warioba anafafanua zaidi kuwa Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba, lakini si suala la kawaida Bunge Maalumu kubadili hoja ya msingi.
No comments:
Post a Comment