HATIMAYE CCM WAMALIZA MGOGORO
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wamemaliza mgongano wa muda mrefu wa vigogo wa kuwania uenyekiti wa
kudumu wa Bunge hilo, baada ya kutoa baraka zote kwa Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kugombea nafasi hiyo.
Wakati Waziri Sitta akipewa baraka hizo na wajumbe hao kupitia Kamati ya
Uongozi ya Wabunge wa CCM, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew
Chenge, ameripotiwa kuamua kutogombea nafasi hiyo.
Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan
Suluhu, amepitishwa na kamati hiyo kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti
wa Kudumu wa Bunge hilo kutokea Zanzibar.
Sitta jana ameelezea kupitishwa na chama chake, lakini
alisema kuwa hakuwa kwenye mkutano huo hadi mwisho. “Niliingia kwenye
kikao na kutoka mapema, sijui kama uamuzi huo umefikiwa,” alisema.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya kikao hicho vinaeleza
kuwa, uamuzi wa kamati hiyo ulifikiwa baada ya kuwaita viongozi hao na
kuwahoji kwa nyakati tofauti iwapo wana nia ya kugombea nafasi hizo au
la.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Waziri Sitta na Waziri Suluhu, walipitishwa
kwa kauli moja kuwania nafasi hizo, baada ya kamati hiyo kujiridhisha
kwamba, wamekidhi sifa.
Mbali na Sitta, Suluhu na Chenge, chanzo hicho kilieleza kuwa mwingine,
ambaye aliitwa na kuhojiwa na kamati hiyo ni Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar, aliyefahamika kwa majina la Mwajuma Mgeni,
ambaye hata hivyo, naye kama Chenge aliamua kutogombea nafasi hiyo.
Kabla ya kamati hiyo kutoa baraka hizo, kiongozi pekee aliyejitokeza
hadharani na kutangaza azma ya kuwania nafasi hiyo ni Sitta pekee.
Sitta alisema anataka kuwania nafasi hiyo ili apate fursa ya kutimiza
kwa vitendo ndoto ya Rais Jakaya Kikwete ya kuhakikisha Tanzania inapata
katiba bora.
Imeelezwa kuwa wajumbe kadhaa walipendekeza jina la Sitta lipitishwe
pasipo kuwapo mgombea mwingine, kwa maelezo kuwa wana-CCM wengine
waliokuwa wanatajwa, wanaonekana kutokuwa na uwezo wa kulimudu Bunge
hilo.
“Tumetoka kwenye kikao cha wajumbe wa CCM na kwa namna ya pekee,
imekubalika kwamba Sitta ndiye anayefaa kwa uenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba,” kilieleza chanzo kimojawapo kwa sharti la kutokutajwa jina
lake gazetini.
“Kama chama kimeonyesha imani yake kwa Sitta, na kwa mujibu wa Sheria,
Makamu wake anatakiwa kutoka Zanzibar ambapo jina la Samia Suluhu
limepitishwa ndani kwa wajumbe wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Sitta amekuwa akitajwa ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba, kwamba
anafaa kuchukua nafasi hiyo kutokana na rekodi nzuri aliyoiacha
alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment