Tuesday, 18 March 2014

BUNGE MAALUM LA KATIBA LAVURUGIKA

 


Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, jana alianza vibaya kazi ya kuongoza hilo baada ya baadhi ya wajumbe kugoma kusikiliza taarifa ya Rasimu ya Katiba Mpya iliyokuwa iwasilishwe na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.


Hali hiyo ilitokea dakika chache tu baada ya Sitta kumtaka Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah kutangaza utaratibu unaofuata, akitangaza kuwasilishwa kwa Rasimu hiyo.

Hata hivyo, Bunge hilo liliahirishwa saa moja baadaye baada ya Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad, kutangaza kuahirishwa kwa Bunge hilo hadi hapo wajumbe watakapotangaziwa baadaye.

“Wajumbe Bunge limeahirishwa hadi hapo mtakapopewa taarifa baadaye, tunaomba muondoke ndani ya ukumbi huu,” alisema.

“Tutawatangazieni wakati tutakapokuja kuendelea na kikao cha Bunge. Waheshimiwa leo ninawaomba tutawanyike,” aliongeza.

Awali kabla ya kuahirishwa kwa Bunge hilo, Sitta alisimama na kumuomba Jaji Warioba kwenda mbele ya Bunge kuwasilisha taarifa yake.


Hata hivyo, baada ya tamko hilo la Mwenyekiti.  Profesa Ibrahim Lipumba, alisimama kuomba mwongozo akifuatiwa na Moses Machali, ambao hata hivyo, hawakusikilizwa na Mwenyekiti aliwataka kuketi kwa kuwa alisema hakuna mwongozo kwenye suala hilo.


Wengine waliosimama ni Freeman Mbowe, James Mbatia na Mchungaji  Christopher Mtikila.Hatua hiyo ilisababisha wajumbe wengine wa Umoja wa Wanaotetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimama na kugonga meza huku wakipasa sauti ya “Fuata kanuni mwenyekiti, tutaendelea hivi hadi utakapoacha kuvunja kununi.”
 
Inayodaiwa kuvunjwa ni kanuni ya 7 (1) h, ambayo inaelezea uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi ilitakiwa ianze, lakini ilitenguliwa ili kuruhusu Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo.
Wakati hayo yakiendelea Jaji Warioba alikuwa amesimama sehemu aliyotakiwa kuwasilisha taarifa yake kwa dakika tano bila kuanza kuisoma huku akiwa amepigwa butwaa kutokana na makelele yaliyotawala ndani ya ukumbi huo.

Licha ya makelele ya wajumbe hao, Sitta aliendelea kumsisitiza Jaji Warioba aendelee kuwasilisha taarifa yake, lakini ilishindikana kutokana kelele za zomea zomea kuongezeka na kumsababisha Jaji Warioba kuondoka mbele na kwenda kuketi sehemu maalumu waliyopangiwa  wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kufuatia hali hiyo, Sitta alisimama na kusema: “Katika mazingira haya hatuwezi kuendelea, naomba kutangaza kuahirisha Bunge kwa sasa hadi hapo tutakapotangaza baadaye.”

Baada ya kutamka hayo, Sitta alitoka nje ya ukumbi na baadaye kupita sehemu ya waandishi wa habari kuelekea kwenye chumba cha kikao.

Wakati akipita kwenye chumba cha waandishi wa habari akiwa ameongozana na Naibu Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, waandishi hao walimpa pole Sitta, naye alijibu: “ndiyo demokrasia yenyewe.”

Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wajumbe ndani ya ukumbi huo walionekana kurushiana maneno ya kushutumiana na kuonyeshana ishara za kudharauliana.
Avemaria Semakafu, akirushiana maneno na mjumbe mwingine Abdallah Juma (CUF) ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, walisuluhishwa na wajumbe wengine huku Juma akitolewa nje.
Awali kabla ya kuanza kwa kikao cha jioni, wabunge ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitishia kwamba wangesusia kuingia kwenye kikao hicho kwa ajili ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni.

Walisema kuwasilishwa kwa taarifa hiyo kabla ya Rais kulizindua Bunge hilo ni uvunjaji wa sheria na ukiukwaji wa kanuni za Bunge hilo.

No comments:

Post a Comment