WANAJESHI DRC MAHAKAMANI KWA UBAKAJI
Wanajeshi 39 wa serikali nchini DRC, waliotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, wamefunguliwa mashitaka Mashariki mwa nchi.
Mengi ya makosa walioshtakiwa nayo, yanahusiana
na ubakaji na vitendo vingine vya uhalifu wa kingono dhidi ya wanawake
na wasichana 130 mwezi Novemba mwaka 2012.
Waandishi wa habari wanasema kuwa
kesi hii dhidi ya jeshi, inakuja baada ya miezi mingi ya shinikizo
kutoka kwa jamii ya kimataifa hasa baada ya wanajeshi kadhaa kuachishwa
kazi bila ya kufunguliwa mashitaka.
Umoja wa Mataifa hata hivyo ulitishia kusitisha ufadhili wake kwa vikosi vya jeshi la DRC vilivyoshukiwa kufanya uhalifu.
Makundi ya wapiganaji waliojihami, hutumia ubakaji kama silaha ya vita.
Mwandishi wa BBC mjini Goma, Maud Jullien,
anasema kuwa makosa walioshitakiwa nayo wanajeshi hao ni pamoja na
ubakaji, uporaji na wengi walioshitakiwa ni wanajeshi wa kiwango cha
chini katika mahakama ya kijeshi Mashariki mwa mji huo.
Kesi hiyo itaangazia matukio ya mwaka jana
wakati waasi wa M23 walipoteka mji wa Goma huku maelfu ya wanajeshi wa
serikali wakilazimika kutorokea mjini Minova.
Kwa mujibu wa ripoti ya UN, angalau wanawake 102
na wasichana 33 walibakwa na kutendewa dhuluma zingine za kingono, na
wanajeshi Kusini mwa Goma.
Wakili anayewakilisga waathiriwa, Sylvestre Bisimwa,anasema idadi ya waathiriwa iliyonukuliwa na UN ni ndogo sana.
Alisema kua hadi sasa watu 1,014 - wanaume kwa wanawake, - wametajwa kama waathiriwa wa uhalifu wa kivita mjini Minova.
Kesi hii iliahirishwa kwa wiki mbili kufuatia
ombi la mawakili kadha wanaowawakilisha waathiriwa kuwa waruhusiwe
kwenda Minova kutafuta mashahidi zaidi.
Aidha bwana Bisimwa alielezea kushtushwa na idadi ndogo ya maafisa wakuu wa jeshi waliofikishwa mahakamani.
Wengi wa waathiriwa waliongeza kuwa wabakaji hawakuwa miongoni mwa watu 39 walioshtakiwa.
No comments:
Post a Comment