G7 YAILAUMU URUSI KUHUSU UKRAINE
Kundi la mataifa saba yaliyostawi zaidi kiviwanda
almaarufu kama G7 limelaani vikali hatua za kijeshi zilizochukuliwa na
Urusi nchini Ukraine-viongozi kundi hilo wakitaja hatua ya Urusi kama
ukiukaji wa uhuru wa Ukraine.
Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa pia saini na
Umoja wa Ulaya EU-Urusi imetakiwa kushughulia wasiwasi wake kuihusu
Ukraini kupitia mashauri au upatanishi.
Kundi
hilo la mataifa saba tajiri zaidi duniani maarufu kama G-Seven limesema
kuwa linachukuwa uamuzi wa kuahirisha matayarisho ya kongamano ambalo
lingefanyika nchini Urusi mwezi juni mwaka huu kutokana na vitendo vya
Moscow. Taarifa hiyo inakuja wakati vikosi vya Urusi vikiimarisha
uthibiti katika rasi ya crimea ambapo Urusi inasema kuwa inalinda raia
wake baada ya serikali kupinduliwa mjini Kiev.
Mbunge mashuhuri wa Urusi - Vyacheslav Nikonov,
ameimabia BBC kwamba Urusi imejiandaa kwenda vitani kulinda maslahi yake
nchini Ukraine na hususan katika mji wa Sevastopol.
"Ukraine ilialikwa kujiunga na Nato na hii ina
maana kuwa marekani, au vituo vyake vya kijeshi vitawekwa nchini
Ukraine. Urusi itafanya lolote, itahatarisha kuingia vita kuzuia hilo
kutokea. Ni kuhusu kituo cha kijeshi, ni kuhusu mustakabal wa Urusi,
mustakabal wa Ukraine. Sidhani kama mataifa ya magharibi yanaelewa
kwamba Ukraine ni mahali ambapo Urusi ilizaliwa," amesema Nikonov.
Awali serikali ya mpito ya Ukraine iliishutumu
Urusi kwa kutangaza vita na kuwaamuru wanajeshi wake kuwa tayari kwa
makabiliano.Shirika la kujihami kwa mataifa ya Magharibi NATO limetowa
wito kwa Urusi kuwaondoa wanajeshi wake nchini Ukrainena kuzitaka pande
zote kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya amani.
Taarifa hiyo imetolewa
baada ya mkutano wa dharura wa mabalozi wa NATO mjini Brussels kujadili
mgogoro huo. Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema kuwa
huenda wachunguzi wa umoja wa mataifa wakatumwa kusaidia kusuluhisha
hali ya mambo.
"Tunatoa wito kwa urusi kuheshimu ahadi zake za
kimataifa, kuondoa vikosi vyake na kujiepusha na uvamizi katika maeneo
mengine nchini Ukraine.
Tunatowa wito kwa pande zote kufuata njia ya
amani katika kusuluhisha mgogoro huo kupitia mazungumzo, kupitia
wachunguzi wa kimataifa chini ya mwavuli wa umoja wa baraza la usalama
la umoja wa mataifa au shirika la ushirikiano wa kiusalama ulaya OSCE,''
amesema bwana Rasmussen.
No comments:
Post a Comment