LUKUVI AKATALIWA WAZO LA KUTOVIPA UHURU VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum kuhusu
Rasimu ya Kanuni za bunge hilo, Profesa Costa Ricky Mahalu, imewaumbua
wajumbe wake akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Bunge na
Sera), William Lukuvi.
Lukuvi na wajumbe wengine, wanatajwa kuwa vinara wa kutaka
waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia na kuripoti habari za kamati za
bunge hilo wakati zitakapokuwa zikikutana.
Akijibu hoja mbalimbali za wajumbe hao wakati akihitimisha semina
kuhusu rasimu ya Kanuni za Bunge juzi usiku, Profesa Mahalu alisema,
kamati yake imeona hakuna sababu kwa waandishi wa habari kuzuiwa
kuhudhuria vikao hivyo na kuripoti habari zitakazokuwa zikijadiliwa.
Alisema kamati imeona kuwa mchakato huo unawahusu wananchi na sio
vema kuwanyima uhuru na haki ya kupata habari kuhusu kinachoendelea,
kupitia waandishi wa habari.
Mapema wiki liyopita akichangia semina hiyo, Lukuvi alisema
waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia kwenye kamati hizo na kuripoti.
“Tuache wajumbe wamenyane humo ndani hata waandishi wa habari
wasiwepo, ila wataalam wanaweza kuitwa kama kutakuwa na hitaji,”
alisema.
Mjumbe mwingine Kidawa Hamid Swalehe, aliungana na Lukuvi pale
aliposema wageni pamoja na waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia
kwenye kamati.
“Waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia kwenye kamati, no,” alisema.
Lakini mjumbe Esther Bulaya, (Mbunge Viti Maalum CCM) ambaye
kitaaluma ni mwandishi wa habari, alipinga hoja ya ‘akina Lukuvi’ na
kwamba hatakubaliana na kifungu cho chote cha sheria kitakachokuwa
kinawekwa ili kuzuia uhuru wa habari.
“Napinga kipengele cho chote kinachonyima uhuru wa habari, ni vema
waandishi wa habari wakaruhusiwa kuingia na kufanya kazi zao kwenye
kamati,” alisema.
Pamoja na Bulaya, mjumbe mwingine Maria Sarungi, aliunga mkono waandishi wa habari kuingia kwenye kamati na kuripoti.
Naye Dk. Masele Maziku, alisema anashangaa kuna wajumbe wakifanya
mkakati wa kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye kamati wakati huo
huo wakitaka uwazi katika kupiga kura.
No comments:
Post a Comment