Thursday, 13 March 2014

SITTA  APATA 86.5%

 


Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, jana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge Maalum la Katiba.


Akitangaza matokeo hayo saa 12:07 jioni Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema Sitta alimshinda mpinzani wake, Hashim Rungwe Sipunda kwa kupata kura 487 (asilimia 86.5) dhidi ya kura 69 (asilimia 12.3) za mpinzani wake.


Dk. Kashililah alisema kuwa Bunge hilo lilikuwa na wapiga kura 629, lakini waliopiga kura ni wajumbe 563 na kwamba kura zilizoharibika ni saba (asilimia 1.2).


Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, ukumbi mzima wa Bunge ulilipuka kwa shangwe na vifijo, hali iliyomfanya Rungwe kuinuka katika kiti chake na kumfuata Sitta kumpongeza na kukumbatiana naye kwa furaha.


Baadhi ya wajumbe walianzisha wimbo wa “Tuna imani na Sitta, tuna imani na Sitta”.


Tukio lingine lililosisimua  wajumbe ni hatua ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kumfuata Sitta na kupeana mikono.

No comments:

Post a Comment