MGOMO WA DALADALA MOSHI
Vurugu kubwa zimezuka katika kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi na
kusababisha gari lililowabeba askari kanzu wa Jeshi la Polisi mkoa wa
Kilimanjaro kupopolewa kwa mawe na kisha kuvunjwa vioo na watu
wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi yanayotoa huduma hiyo katika miji
ya Arusha na Moshi.
Vurugu hizo zilitokana na wamiliki wa mabasi pamoja na madereva kugoma kutoa huduma kuanzia asubuhi saa 11 hadi saa 10:30 jioni wakilalamika kuwa wanalazimishwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani kutoa rushwa ili kuficha makosa baada ya kuwadai stakabadhi ya uthibitisho wa malipo wanayotoa kwa askari hao.
Gari la Polisi lilipopolewa kwa mawe na kuvunjwa vioo likiwa na askari kadhaa ni lenye namba za usajili T 743 ADC Toyota Land Cruiser, lilikumbana na dhoruba hiyo baada ya askari kujaribu kumkamata mmoja wa madereva wa mabasi hayo ambaye hakufahamika jina mara moja anayefanya safari kati ya Moshi Mjini na Holili mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kufuatia mgomo huo, abiria wanaosafiri katika miji ya Arusha, Moshi na wilaya sita za mkoa wa Kilimanjaro walikwama kwa kutwa nzima jana.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mabasi Kanda ya Kaskazini (Akiboa), Hussein Mrindoko, wamesema kua wameamua kugoma kutokana na baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani kugeuza stakabadhi za malipo yanayotokana na faini kuwa mtaji wa kibiashara kwa kuwa wanatoza gari moja faini ya Sh. 30,000 hadi mara tatu kwa siku.
“Tunakuomba Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (Leonidas Gama) uchukue hatua za kimaadili dhidi ya maofisa watatu wa Jeshi la Polisi ambao wamekuwa wakifanya maamuzi ya kibabe na kusababisha uzaliwe mgogoro huu. Huyo ofisa anayekojoa nyuma ya magari halafu amelewa ni fedheha kwa jeshi na serikali kwa ujumla,” alisema Mrindoko katika kikao alichoitisha mkuu huyo wa mkoa.
Wakiwa katika mkutano huo wa usuluhishi, baadhi ya madereva hao na wamiliki wa mabasi walimweleza Gama kwamba Mkuu wa kikosi hicho, Mkuu wa kituo kidogo cha Polisi cha Stendi Kuu ya Mkoa na Mkaguzi wa Polisi kituo cha Himo wamekuwa na desturi ya kufanya kazi kwa ubabe ikiwamo kuwapiga makonde na kuwabambikizia makosa baada ya kuhoji uhalali wake, hivyo kusababisha uhasama mkubwa.
Akijitetea, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO), Joseph Mwakabonga, alikiri kumpiga makonde mmoja wa wamiliki wa mabasi wa wilaya ya Hai, Abdulrazack Mtoro, akidai sheria inamruhusu kufanya hivyo pale kunapokuwa na vurugu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Stendi Kuu (OSC), Hendry Nguvumali, alisema madereva na wamiliki wa mabasi hayo wanashuhudia uongo kwa kumdanganya mkuu wa mkoa kwamba yeye ni mlevi wa kupindukia na amekuwa akikojoa nyuma ya mabasi ya abiria, jambo ambalo haliwezi kumzuia kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, akizungumzia malalamiko yanayotokana na kupotoka kwa maadili ya askari, alisema ofisi yake itachukua hatua za kimaadili haraka iwezekanavyo, ingawa wananachi pamoja na madereva wa mabasi hayo wanatakiwa pia kutii sheria za usalama barabarani bila kushuruti.
“Nitachukua hatua mara moja kuhusu maadili, hili la ulevi wa kupindukia kwa kweli limelidhalilisha Jeshi la Polisi, lakini pia suala la kupiga watu makonde siyo utaratibu kwa sababu ofisa anatakiwa kufuata sheria na kwa kuwa amekiri mwenyewe (RTO) nitalitazama kwa kufanya uchunguzi,” alisema Boaz.
Gama alisema iwapo mgomo huo wa mabasi utaachwa uendelee kwa siku ya pili, unaweza ukasababisha kuporomoka kwa uchumi wa mkoa huo. Gama aliamuru Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kupeleka ofisini kwake ratiba inayoonyesha namna anavyokutana na wadau wa usafirishaji pamoja na kushughulikia kero zinazotokana na askari wa usalama barabarani.
“Nyie Polisi, Sumatra na wasafirishaji mnafanya kazi zenu kwa kuviziana na kutengenezeana uhasama ili kuonyeshana ubabe. Muda mfupi baada ya kukaa na kamati yangu ya ulinzi na usalama, nitatoa taarifa kwa umma kuhusiana na hatua za kinidhamu nilizochukuliwa kama serikali kwa niaba ya Waziri Mkuu,” alisema Gama na kuongeza:
“Sumatra nataka mnieleze kwa nini agizo langu hamjatekeleza hadi sasa na mmezalisha mgogoro huu?” Mgomo huo ulisababisha wananchi kutumia usafiri wa bodaboda, bajaj na magari madogo ya kukodi. Hawa Hussein, mkazi wa Rombo alisema mgomo huo uliathiri shughuli zake nyingi za kiuchumi.
Francis Meena, mkazi wa Sanya Juu alisema mgomo huo ulisababisha adha kubwa ikiwamo kutembea kwa miguu umbali mrefu huku wengine wakilazimika kuingia gharama za kukodi bodaboda kwa gharama ya Sh. 5,000. Mkaguzi mmoja aliliambia gazeti hili kuwa magari hayo yanastahili kukamatwa na trafiki kwa kuwa mengi ni mabovu na yanakiuka sheria za barabarani.
Alizitaja kuwa ni kupakia abiria katika maeneo yasiyo rasmi, hayafanyiwi usafi na kutokidhi viwango vya magari ya abiria. Alisema wamiliki wake wanalalamikia, magari yao kukamatwa, lakini wana makosa mengi ya kiusalama.
“Ninakuambia katika magari 300 ni magari 20 yatakidhi vigezo vya kubeba abiria kama yakikaguliwa sawasawa,” alisema mkazi mmoja wa mjini Moshi aliyejitambulisha kama msafiri wa kila siku ndani ya mkoa wa Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment