Friday, 7 March 2014

 BUNGE LA KATIBA: WABUNGE NUSURA WAZICHAPE


 

Aibu kubwa imetokea katika kikao cha jana asubuhi cha Bunge Maalumu la Katiba baada ya baadhi ya wajumbe kutaka kurushiana makonde, hali iliyosababisha Bunge kuchafuka na kumlazimisha Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kukiahirisha.
Hali hiyo ilizuka wakati wajumbe wa Bunge hilo wakijadili vifungu vya Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, kwa lengo la kuvifanyia marekebisho.


Mtafaruku huo ulizuka baada ya mjumbe wa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari, kuilalamikia sekretarieti ya Bunge kwa madai ya kukiuka utaratibu.


Bakari alisema orodha ya wajumbe waliotajwa na Kificho kutoa mapendekezo ya marekebisho ya vifungu vya rasimu hiyo, hawakuwapo kwenye ile waliyonayo wajumbe wa kamati hiyo.


“Sekretariati inakwenda kinyume cha utaratibu. Haiwezekani sekretariati wakuletee wewe (mwenyekiti wa muda) majina na siyo kwa kamati…Mimi kama mjumbe wa kamati hii sikubaliani hata kidogo na utaratibu huo. Sekretarieti ichukuliwe hatua,” alisema Abubakari.


Alisema kwa mfano, mjumbe ambaye alitajwa awali na Kificho kutoa mapendekezo ya marekebisho kwenye kifungu cha 58 cha rasimu hiyo, Christopher Ole Sendeka, na aliyetajwa baadaye, Ummy Mwalimu, majina yao hayamo kwenye orodha, ambayo kamati inayo.

Kifungu hicho kinazungumzia muundo na majukumu ya Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu.


Wakati  Abubakar akitoa maelezo hayo, sauti za baadhi ya wajumbe zilikuwa zikisikika zikisema “waondolewe, waondolewe.”  Wakimaanisha wale, ambao majina yao hayamo kwenye orodha iliyonayo kamati.


Kufuatia malalamikoa ya Abubakari, Kificho alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Profesa Costa Mahalu, kusimama na kutoa maelezo.


Profesa Mahalu alithibitisha kwamba, kamati yake haina majina, ambayo yanatajwa na Kificho.

 Alisema sekretarieti ina majina ya wajumbe bila hoja, wakati juzi walikuwa na mapendekezo ya hoja kwa vifungu vya kanuni pamoja na majina.


 “Sasa inawezakana orodha yetu ina wajumbe wachache na orodha aliyonayo mwenyekiti (Kificho) ina majina mengi… Sasa hii inaonekana inaleta utata. Hivyo, naomba tuendelee,” alisema Profesa Mahalu.


Hata hivyo, wajumbe hawakuridhika na maelezo hayo wakitaka majina yanayotajwa na Kificho yaondolewe.


SENDEKA AIBUKA
Kificho alimsimamisha Sendeka, ambaye alisema: “Mimi siyo dhaifu wa kanuni za Bunge. Nimetajwa kuwa jina langu halipo. Katika hili mwenyekiti sikupeleka jina langu kwa Abubakar. Nilipeleka jina langu kwa sekretarieti. Kama Abubakar ana chama chake aseme,” alisema Sendeka.

Aliongeza: “Mimi, Ummy Mwalimu na Peter Serukamba tulipeleka majina yetu sekretarieti. Kama mapigo yetu yanawaudhi wengine hilo ni la kwao.”


Kauli ya kudai kuwa Abubakar, ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni (CUF), ana chama chake anachokitetea ndani ya Bunge, iliwaudhi baadhi ya wajumbe, ambao walikuwa wakizomea na wengine kucheka.

Hali hiyo ilimfanya Kificho kusimama na kuwaonya wajumbe dhidi ya kutumia maneno yenye kuamsha hasira bungeni.


 “Tujitahidi tusionyeshe misimamo ya vyama humu bungeni. Lengo linalokusudiwa linaweza kutetereka. Si vyema kuanza kuonyeshana vidole huyu ni wa CCM, huyo ni CUF, huyu ni wa Chadema, hiyo itaibua hisia tofauti,” aliasa Kificho.


 Aliongeza: “Hivyo, Ole Sendeka ulimi umekwenda mbali kidogo ukamgusa Abubakar na hiyo ndiyo maana kumetokea ghasia humu. Nakuombeni wabunge tuwe wamoja kwa sababu kazi yetu mbele ni kubwa na sasa tupo bado kwenye kanuni.


“Nakuomba Abubakar ashushe kidogo na Ole Sendeka pamoja na wajumbe wengine msirudie kufanya hivyo.”

Hata hivyo, sauti za baadhi ya wajumbe zilisikika wakitaka Sendeka amwombe radhi Abubakar, lakini Kificho hakutaka kufanya hivyo.


Baada ya hapo, alisimama tena Abubakar naye akafafanua alichokuwa amesema awali kuwa utaratibu anaotumia Kificho kuwataja majina wachangiaji una kasoro, kwani majina hayo hayamo kwenye orodha, ambayo kamati inayo.
Alisema iwapo muda wa kuwasilisha majina kwa ajili ya marekebisho ya vifungu ukipita, basi asiruhusiwe mjumbe mwingine kuingizwa kinyemela.


VIJEMBE DHIDI YA SENDEKA
Hata hivyo, akijibu vijembe vya Ole Sendeka, Abubakar alisema: “Sifikirii kama Sendeka ana uwezo wa kujua kanuni kama mimi. Mimi ninazijua kanuni za mabunge, kuanzia mwaka 1980. Sitaki niombwe radhi, lakini Sendeka ajue tu kwamba, kuna watu wanajua zaidi kuliko yeye.  Hawezi kutoka mtu kutoka Simanjiro kuja hapa bungeni miaka 10 na kudai anajua zaidi kuliko wengine.”


Vijembe hivyo vilizua vurugu kubwa, baada ya wajumbe, wengi wao kutoka CUF na CCM kusimama, huku kila mmoja akiongea bila kufuata utaratibu.


Baadhi ya wajumbe, akiwamo Abdallah Sharia (Dimani CCM), walishikana maungo na Khatib Haji (Konde-CUF), kiasi cha kulazimika askari wa usalama kuwatenganisha.


Pamoja na juhudi za Kificho kuwatuliza wajumbe, hali iliendelea kuchafuka, na hivyo kumlazimisha aliahirishe Bunge hadi saa 10:00 jioni jana.


Aliahirisha Bunge majira ya saa 6:17 wakati katika hali ya kawaida huahirishwa kwa mapumziko saa 8:00 mchana.


KITI CHALALAMIKIWA
Mjumbe wa Bunge hilo, Yusufu Manyanga, alisema kiti cha mwenyekiti hakiendi vizuri na kushauri utaratibu uboreshwe.

Alisema wameingiza virusi kwenye taasisi kutokana na kiti kutoa upendeleo wa kuchangia kwa wajumbe wanasiasa.


“Wanasiasa wanatuburuza, haiwezekani watu wale wale wanapewa nafasi ya kuzungumza,” alisema Manyanga.


POSHO KUBWA MNO

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keisy, alisema tatizo ni fedha, kama zingepunguzwa Bunge lisingeahirishwa mara kwa mara na kupendekeza  walau wajumbe wangelipwa Sh. 100,000 kila mmoja badala ya Sh. 300,000.


MAKUNDI YA URAIS TATIZO
Mjumbe mwingine, Yussufu Salim Hussein, alisema mwenyekiti anayumba na kwamba, kinachoyumbisha ni mtandao wa urais mwaka 2015.


Aliwataja Sendeka (Simanjiro-CCM), Ummy (Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM) kuwa ni miongoni mwa wajumbe waliomo kwenye mtandao huo, ingawa hakufafanua.


Alisema vurugu zinazotokea na kusababisha vikao kuahirishwa mara kwa mara zinatokana na kutokuwa kwa kanuni za mwenyekiti za namna ya kuendesha semina ya wajumbe kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu iliyoanza Jumatano wiki iliyopita bungeni.


MWENYEKITI TATIZO
Mbunge wa Kwimba (CCM), Mansoor Hiran, alilalamikia kitendo cha mwenyekiti kuwapa nafasi ya kuchangia watu wale wale tu na pia hachungi muda, ambaye wakikubaliana waanze kikao saa 4, yeye anakwenda saa 5, akipanga waanze saa 10, yeye anakuja saa 11.


Hata hivyo, baada ya wajumbe kurejea jana jioni hali ilionekana kubadilika, kiasi cha wengine kutumia hekima na busara kuwakumbusha wajumbe wajibu wao.Miongoni mwao ni James Mbatia aliyewambia wajumbe ….


Kadhalika Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya alitumia kauli za busara kuwataka wajumbe kutambua kuwa Watanzania wana matumiani makubwa sana nao. 


Alisema kuwa zimekuwa zikipigwa simu nyingi hali kama hiyo inapotokea na kuwakumbusha kuwa bunge la katiba linapaswa kuendeswa kwa maridhiano zaidi wala siyo suala la kupiga kura ya wazi au siri.

No comments:

Post a Comment