Wednesday, 12 March 2014

BUNGE LA KATIBA KANUNI ZAPITISHWA


 

 PROF COSTA MAHALU

Baada ya mvutano wa takribani wiki tatu, hatimaye Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, wameridhia Rasimu za Bunge hilo na sasa zinaanza kutumika rasmi kujadili Rasimu ya Katiba, lakini vifungu vya jinsi ya upigaji kura kwa ajili ya kupata uamuzi vitaamuliwa baadaye na wajumbe.


Akiwasilisha azimio la kutunga na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum bungeni jana, Mwenyetiki wa Kamati ya Muda ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni za Bunge Maalum, Profesa Costa Mahalu, alisema suala la aina ya upigaji wa kura kwa ajili ya kupata uamuzi bado linaendelea kushughulikiwa.


Alisema suala hilo litawekwa katika kanuni husika baada ya kuamuliwa, kama ambavyo bunge hilo litakavyoona inafaa.


Kanuni hizo zimetungwa chini ya kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ambacho kinaelekeza Bunge Maalum litatunga kanuni kwa ajili ya kuendesha shughuli za Bunge Maalum.


Mvutano ulikuwa kwenye kanuni za 37 na 38 zinazozungumzia upigaji kura. Wakati  awali kanuni ya 37 inazungumzia utaratibu wa kufanya uamuzi kuwa ni kura, ile ya 38 inazungumzia namna ya kupiga kura ikisema wakati wa kupiga kura, kila mjumbe atapiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’.


Fasili ya pili ya kanuni hiyo inasema utaratibu wa kupiga kura utakubaliwa na Bunge Maalum baada ya kupitishwa kwa kanuni hizo.


Baada ya kuwasilishwa kwa azimio hilo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Pandu Ameir Kificho, aliwapa nafasi wajumbe kadhaa kutoa kauli zao za kuunga mkono.
 

No comments:

Post a Comment