BUNGE LAWAKANA LIPUMBA NA MBATIA
LIPUMBA MBATIA
Bunge Maalumu la Katiba limesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
unaoundwa na baadhi ya wajumbe wake, wakiongozwa na Profesa Ibrahim
Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR) hautambuliwi.
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas
Kashililah, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE Jumapili, mjini hapa
juzi.
Dk. Kashililah alisema Ukawa utapata nguvu ya kisheria na kupewa
ushirikiano na ofisi ya Bunge iwapo utatambuliwa kwa mujibu wa kanuni za
Bunge Maalumu, ambazo ziko katika mchakato wa kutungwa.
Hata hivyo, Dk. Kashililah alisema ofisi ya Bunge inafahamu kwamba,
makundi mbalimbali ya wajumbe wa Bunge hilo yamekuwa yakikutana na
kujadili masuala yanayolihusu kila moja.
Kuundwa kwa umoja huo, kulitangazwa rasmi juzi na Profesa Lipumba,
mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Profesa Abdallah Safari na Mbatia.
Profesa Lipumba, Profesa Safari na Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais (NCCR-Mageuzi), wote ni wajumbe wa Bunge hilo.
Profesa Lipumba alisema umoja huo unaundwa na baadhi ya wajumbe
Bunge Maalumu la Katiba kutoka makundi tofauti yanayotambuliwa kwa
mujibu wa sheria.
Alisema lengo la Ukawa, pamoja na mambo mengine, ni kutetea rasimu
ya katiba iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa
na Jaji Joseph Warioba.
Pia alilitaja lengo jingine kuwa ni kuiboresha rasimu hiyo kwa
kuzingatia maoni ya wananchi na si `kuchakachuliwa’ kwa misimamo ya
vyama, taasisi au makundi ya kijamii.
Profesa Lipumba alisema miongoni mwa sababu za kuundwa kwa Ukawa ni
matamko ya baadhi ya viongozi kuwa, Bunge Maalumu la Katiba linaweza
kuja na maoni tofauti na yale ya wananchi yaliyoratibiwa na Tume ya
Warioba.
Matamshi hayo yalitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema, wiki iliyopita na kukaririwa na baadhi ya vyombo vya
habari.
No comments:
Post a Comment