SHUGHULI YA KUITAFUTA MH370 IMESITISHWA
Mamlaka ya usalama wa safari za baharini nchini
Australia imesema kuwa operesheni ya kuitafuta ndege ya shirika la
Malaysia iliyotoweka imesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa na
mawimbi makali baharini.
Taarifa zinasema kuwa upepo mkali pamoja na mvua
kubwa inayonyesha katika eneo hilo ina maana kuwa ndege hazitoweza
kupaa kwa usalama. Mawimbi makali yameilazimisha meli ya jeshi la
wanamaji wa Australia kuondoka katika eneo ambalo mabaki yanayodhaniwa
kuwa ya ndege hiyo yalionekana hapo jana Jumatatu.
Dr
Erik van Sebille, ambaye ni mtaalam wa maswala ya Baharini katika chuo
kikuu cha New South Wales mjini Sydney, amefanya utafiti katika eneo
hilo la kusini mwa Bahari Hindi kutambua ni wapi na vipi vifusi
vinasafirishwa na mawimbi ya bahari. Anasema itakuwa vigumu sana kupata
mabaki ya ndege hiyo.
" Ni eneo lisiloweza kukalika duniani, acha
niseme. Upepo unaovuma ni mkali sana, mawimbi ni makubwa, ni mojawepo wa
mawimbi makubwa zaidi baharini. Unapofika katika eneo hili la kusini,
unaanza kuhisi athari za eneo la Antactica kwenye bahari.
Hapa
tunazungumzia dhoruba kali kali sana hususan wakati huu tunapoingia
majira ya kupukutika," anasema Dr. Erik van Sebille.Kadhalika amesema kuwa vifusi vilivyoenekana hapo jana tayari vimekwishaondolewa katika eneo hilo na mawimbi makali.
"Haitakuwa rahisi kabisa kupata kijisanduku cha
kunasa habari. Mawimbi ya eneo hili ni makali na kwa hiyo vifusi ambavyo
wametambua kwa sasa huenda vimehamishwa katika kipindi cha majuma
mawili au matatu tangu ndege hiyo ianguka-na huenda vimesafiri kilomita
alfu moja tayari. Na hii inaifanya vigumu kurejelea utafutaji kwa sababu
bahari inabadilika sana hapa-ina vurugu ukipenda."
Hapo awali naibu waziri wa mashauri ya nchi za
Kigeni wa China Xie Hangsheng, aliitaka serikali ya Malaysia kutoka
ushahidi unaoelezea kuwa ndege hiyo ilianguka katika eneo la Kusini mwa
bahari Hindi. Ndege hiyo ilitoweka kwenye mtambo wa Radar zaidi ya
majuma mawili yaliyopita.
No comments:
Post a Comment