WAJUMBE WA ODM KENYA WAZUA VURUGU
Vurugu zimezuka katika uchaguzi wa kuwachagua maafisa
wapya wa chama kikuu cha upinzani cha ODM nchini Kenya, chake aliyekuwa
waziri mkuu wa taifa hilo Raila Odinga.
Polisi waliwasili katika ukumbi wa uwanja wa
michezo wa kimataifa wa Kasarani viungani mwa jiji la Nairobi kurejesha
utulivu baada ya baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliodaiwa kuwa
walinda usalama kurusha vita pamoja na masanduku ya kupigia kura
wakijaribu kuvuruga uchaguzi huo.
Ugomvi ulizuka baada ya kuzuka madai
kuwa kulikuwa na orodha ya wajumbe bandia iliyokuwa ikisambazwa pamoja
na makaratasi bandia ya kupigia kura. Mbunge maalum Isaac Mwaura ambaye
anaishi na ulemavu wa ngozi-Albino-alionekana akisukwasukwa na wajumbe
baada ya kuzua zahama kuhusu madai hayo ya udanganyifu katika zoezi hilo
la upigaji kura.
Chama cha ODM ndicho chama kikubwa zaidi cha
kisiasa nchini Kenya kikiwa na idadi kubwa ya wabunge katika bunge la
kitaifa pamoja na Senate. Chama hicho kimemudu mgao mkubwa zaidi wa pesa
za kufadhili shughuli za vyama vya kisiasa kutoka kwa serikali ya
Kenya.
Kutokana na raslimali za chama hicho uchaguzi wa
leo umeonekana kuzua msisimko mkali pamoja na patashika baina ya
wanasiasa mashuhuru ambao wanagombania vyeo mbali mbali.
Bwana Odinga ambaye alishindwa na rais Uhuru
Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliokumbwa na madai ya udanganyifu mwezi
Machi mwaka uliopita anatetea kiti chake kama kiongozi wa chama, dalili
kwamba huenda akagombea tena kiti cha urais mwaka 2017.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji
kura Bwana Odinga alizungumzia maswala mbali mbali yanayohusiana na
usalama nchini Kenya pamoja na kuiponda serikali ya mpinzani wake Rais
Uhuru Kenyatta kwa kushindwa kuleta suluhu ya matatizo ya kiuchumi
yanayowakabili wakenya.
No comments:
Post a Comment