TFDA YAPIGA MARUFUKU VIPODOZI VYENYE SUMU
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imepiga marufuku viambato
sumu visitumike katika kutengeneza vipodozi na kuzuia vipodozi 242
vyenye sumu nchini, vikiwamo Carolight na Princess.
Lengo la TFDA kuchukua hatua hiyo ni kutekeleza sheria ya uthibiti wa vipodozi ili visitumike na kuleta madhara kwa watumiaji.
Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alitaja viambato sumu vilivyopigwa marufuku kuwa ni Bithionol, Hexachlorophene, Zebaki (Mecury Compounds), Vinyi Chloride, Zirconium, Halgenated Salicylanilides na Chloroquine.
“TFDA inaendelea ukaguzi wa vipodozi vilivyoko sokoni na kupata sampuli mbalimbali na kuzipeleka maabara ili kujua usalama na ubora wake,” alisema.
Simwanza alisema TFDA ilifanya ukaguzi mwaka 2012 /2013 na kufanikiwa kukamata tani 34 za vipodozi visivyofaa vyenye thamani ya Sh. milioni 188.5 na kisha kuviteketeza.
Alisema hadi sasa mamlaka hiyo imethibitisha na kusajili vipodozi 3,968, na kuonya kuwa mtumiaji anapotumia vipodozi ambavyo havijathibitishwa na TFDA yupo kwenye hatari ya kupata madhara makubwa.
Aidha, alisema matumizi vipodozi vyenye viambato sumu hudhoofisha uchumi wa watumiaji na kwa nchi na gharama za matibabu kuwa kubwa katika kutibu madhara.
No comments:
Post a Comment