Thursday, 6 March 2014

CRIMEA WAPIGA KURA KUJIUNGA NA URUSI



Wabunge wa Mji ulio kusini mwa Ukraine,Crimea wamepiga kura ili kuwa sehemu ya Urusi.

Bunge limesema uamuzi huo utaachwa mikononi kwa watu wa Crimea kwa ajili ya kupiga kura ya maoni tarehe 16 mwezi Machi.
Serikali ya Kiev imesema inaamini kuwa Crimea kujiunga na Urusi ni kinyume na Katiba.

Crimea, ambayo wakazi wake walio wengi wana asili ya Urusi, imekua katika malumbano baada ya kuanguka kwa Rais wa taifa la Ukraine.

Taarifa ya Bunge la Crimea imekuja wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kujadili hatua ya kupeleka vikosi vya Urusi katika ardhi ya Ukraine.

Wednesday, 5 March 2014

MAGEUZI CHINA NI LAZIMA



Waziri mkuu wa China, Li Keqiang, ameuambia mkutano wa kila mwaka, wa bunge la taifa hilo mjini Beijing, kwamba maendeleo ya kiuchumi yatabaki kuwa jukumu kubwa zaidi la serikali, lakini marekebisho ya kimsingi ni sharti yatekelezwe japo ni machungu.

Bwana Li amewaambia maelfu ya wajumbe katika bunge la taifa hilo, Great Hall of the People, kwamba shabaha ya kila mwaka ya ukuaji wa kiuchumi itasalia kuwa asilimia saba nukta tano.

Akizungumzia tatizo la uchafuzi, amesema kuwa moshi mkubwa unaondelea kutanda katika miji mikubwa ya China, ni onyo la kiasili dhidi ya maendeleo yasiokuwa na mpango.

Waziri huyo mkuu wa China kadhalika ametangaza marufuku dhidi ya majengo mapya ya serikali kama sehemu ya kile alichokitaja kuwa mapambano bila huruma dhidi ya ufisadi.

MAUAJI ZAIDI NIGERIA



Ghasia zaidi zimetokea Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ambapo watu 13 wameuawa.

Mkaazi wa kijiji cha Jakana karibu na mji wa Maiduguri jimbo la Borno amesema takriban watu 40 wameuawa katika shambulio lililofanywa na kundi la Boko Haram JUmatatu usiku.

Kaskazini mwa Nigeria imeshuhudia mashambulio ya kundi la Boko Haram licha ya operesheni ya jeshi inayoendelea.

Hapo Jumapili usiku watu 30 waliuawa katika shambulio mji wa Mafa na watu wengine 90 waliuawa katika siku ya Jumamosi katika shambulio la bomu mjini Maiduguri.

OBAMA ATAKA WACHUNGUZI WATUMWE UKRAINE

 http://blogs.reuters.com/great-debate/files/2013/07/obama-best.jpg


Rais Obama ametangaza mapendekezo ambayo huenda yakatoa suluhu kwa mzozo wa Ukraine, ikiwemo kuwatuma wachunguzi wa kimataifa na kuanzishwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na serikali mpya mjini Kiev.
Bwana Obama amejadili swala hilo kwa njia ya simu na chanzela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Wachunguzi hao watalenga kulinda haki za watu wa kabila la Urusi waliopo katika jimbo la Crimea; na kwa upande wake Urusi itahitajika kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo hilo. Pendekezo hilo huenda likajadiliwa pembezoni mwa mkutano utakaofanyika nchini Ufaransa (Jumatano) ambao utawaleta pamoja wajumbe kutoka Marekani, Urusi na kwingineko kwa ajili ya kuijadili Lebanon.
  
Hapo awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry, amelaani kile amekitaja kuwa kitendo cha uchukozi kutoka Urusi dhidi ya Ukraine. Wakati wa ziara yake mjini Kiev ambapo aliweka shada la maua kuwakumbuka waandamanaji waliouwawa mwezi uliopita, bwana Kerry ameshutumu Moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.


Mwandishi wa BBC Sarah Reinsford aliyepo mjini Kiev amesema kuwa wakati akiweka shada la maua katika maeneo walikouwawa mamia ya waandamanaji mjini humo, John Kerry alikaribishwa na umati wa watu waliokuwa wakiomba msaada wa marekani.
 
Na hilo ndilo lililomleta hapa; kutoa msaada wa hali na mali na pia wa kisiasa kwa serikali ya mpito ya Ukraine, na pia ahadi ya msaada wa kifedha na wa kiufundi kusaidia katika kuimarisha uchumi, amesema mwandishi wetu.

Rais Putin.

Lakini zaidi ya yote bwana Kerry ameleta ujumbe kwa Moscow.
" Nadhani ni bayana kwamba Urusi imekuwa ikifanya bidii kubuni dhana ya kuiwezesha kutekeleza uvamizi zaidi. Urusi imezungumzia raia wachache wanaozungumza kirusi ambao wamezingirwa.
 
Ukweli ni kwamba hawajazingirwa! Ukweli ni kwamba serikali mpya ya Ukraine imewajibika ipasavyo kwa kuhimiza utulivu na kujiepusha na uchokozi," amesema Bwana Kerry.
 
Hakuna ushahidi, amesisitiza, kwa madai ya urusi kwamba wanajeshi wake wanalinda raia wanaozungumza lugha ya kirusi nchini Ukraine akiishutumu moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.

Katika karne ya ishirini na moja, bwana Kerry ameonya, haiwezekani kuvamia taifa jingine na kisha kuamrisha matakwa yako yatekelezwe kwa kutumia mtutu wa bunduki.

Na kisha akamhimiza rais Putin kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo la Crimea na kushughulikia malalamishi yake kupitia njia za kisheria na amani.
La sivyo, ameonya, kwamba Urusi itakabiliwa na vikwazo zaidi vya kiuchumi na kisiasa.

HATIMAYE CCM WAMALIZA MGOGORO


Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemaliza mgongano wa muda mrefu wa vigogo wa kuwania uenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo, baada ya kutoa baraka zote kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kugombea nafasi hiyo.
 
Wakati Waziri Sitta akipewa baraka hizo na wajumbe hao kupitia Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, ameripotiwa kuamua kutogombea nafasi hiyo.
 
Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu, amepitishwa na kamati hiyo kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo kutokea Zanzibar.  

Sitta jana ameelezea kupitishwa na chama chake, lakini alisema kuwa hakuwa kwenye mkutano huo hadi mwisho. “Niliingia kwenye kikao na kutoka mapema, sijui kama uamuzi huo umefikiwa,” alisema.
 
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya kikao hicho vinaeleza kuwa, uamuzi wa kamati hiyo ulifikiwa baada ya kuwaita viongozi hao na kuwahoji kwa nyakati tofauti iwapo wana nia ya kugombea nafasi hizo au la.
 
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Waziri Sitta na Waziri Suluhu, walipitishwa kwa kauli moja kuwania nafasi hizo, baada ya kamati hiyo kujiridhisha kwamba, wamekidhi sifa.
 
Mbali na Sitta, Suluhu na Chenge, chanzo hicho kilieleza kuwa mwingine, ambaye aliitwa na kuhojiwa na kamati hiyo ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, aliyefahamika kwa majina la Mwajuma Mgeni, ambaye hata hivyo, naye kama Chenge aliamua kutogombea nafasi hiyo.
 
Kabla ya kamati hiyo kutoa baraka hizo, kiongozi pekee aliyejitokeza hadharani na kutangaza azma ya kuwania nafasi hiyo ni Sitta pekee.
 
Sitta alisema anataka kuwania nafasi hiyo ili apate fursa ya kutimiza kwa vitendo ndoto ya Rais Jakaya Kikwete ya kuhakikisha Tanzania inapata katiba bora.
 
Imeelezwa kuwa wajumbe kadhaa walipendekeza jina la Sitta lipitishwe pasipo kuwapo mgombea mwingine, kwa maelezo kuwa wana-CCM wengine waliokuwa wanatajwa, wanaonekana kutokuwa na uwezo wa kulimudu Bunge hilo.
 
“Tumetoka kwenye kikao cha wajumbe wa CCM na kwa namna ya pekee, imekubalika kwamba Sitta ndiye anayefaa kwa uenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,” kilieleza chanzo kimojawapo kwa sharti la kutokutajwa jina lake gazetini.

 
“Kama chama kimeonyesha imani yake kwa Sitta, na kwa mujibu wa Sheria, Makamu wake anatakiwa kutoka Zanzibar ambapo jina la Samia Suluhu limepitishwa ndani kwa wajumbe wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.

 
Sitta amekuwa akitajwa ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba, kwamba anafaa kuchukua nafasi hiyo kutokana na rekodi nzuri aliyoiacha alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Monday, 3 March 2014

G7 NA UKRAINE

G7 YAILAUMU URUSI KUHUSU UKRAINE




Kundi la mataifa saba yaliyostawi zaidi kiviwanda almaarufu kama G7 limelaani vikali hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Urusi nchini Ukraine-viongozi kundi hilo wakitaja hatua ya Urusi kama ukiukaji wa uhuru wa Ukraine.


Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa pia saini na Umoja wa Ulaya EU-Urusi imetakiwa kushughulia wasiwasi wake kuihusu Ukraini kupitia mashauri au upatanishi.


Kundi hilo la mataifa saba tajiri zaidi duniani maarufu kama G-Seven limesema kuwa linachukuwa uamuzi wa kuahirisha matayarisho ya kongamano ambalo lingefanyika nchini Urusi mwezi juni mwaka huu kutokana na vitendo vya Moscow. Taarifa hiyo inakuja wakati vikosi vya Urusi vikiimarisha uthibiti katika rasi ya crimea ambapo Urusi inasema kuwa inalinda raia wake baada ya serikali kupinduliwa mjini Kiev.


Mbunge mashuhuri wa Urusi - Vyacheslav Nikonov, ameimabia BBC kwamba Urusi imejiandaa kwenda vitani kulinda maslahi yake nchini Ukraine na hususan katika mji wa Sevastopol.


"Ukraine ilialikwa kujiunga na Nato na hii ina maana kuwa marekani, au vituo vyake vya kijeshi vitawekwa nchini Ukraine. Urusi itafanya lolote, itahatarisha kuingia vita kuzuia hilo kutokea. Ni kuhusu kituo cha kijeshi, ni kuhusu mustakabal wa Urusi, mustakabal wa Ukraine. Sidhani kama mataifa ya magharibi yanaelewa kwamba Ukraine ni mahali ambapo Urusi ilizaliwa," amesema Nikonov.



Wanajeshi wasiotambuliwa washika doria katika kambi moja ya kijeshi nchini Ukraine.
Awali serikali ya mpito ya Ukraine iliishutumu Urusi kwa kutangaza vita na kuwaamuru wanajeshi wake kuwa tayari kwa makabiliano.Shirika la kujihami kwa mataifa ya Magharibi NATO limetowa wito kwa Urusi kuwaondoa wanajeshi wake nchini Ukrainena kuzitaka pande zote kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya amani.


Taarifa hiyo imetolewa baada ya mkutano wa dharura wa mabalozi wa NATO mjini Brussels kujadili mgogoro huo. Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema kuwa huenda wachunguzi wa umoja wa mataifa wakatumwa kusaidia kusuluhisha hali ya mambo.


"Tunatoa wito kwa urusi kuheshimu ahadi zake za kimataifa, kuondoa vikosi vyake na kujiepusha na uvamizi katika maeneo mengine nchini Ukraine. 


Tunatowa wito kwa pande zote kufuata njia ya amani katika kusuluhisha mgogoro huo kupitia mazungumzo, kupitia wachunguzi wa kimataifa chini ya mwavuli wa umoja wa baraza la usalama la umoja wa mataifa au shirika la ushirikiano wa kiusalama ulaya OSCE,'' amesema bwana Rasmussen.

 HALI BADO SI SHWARI BUNGE LA KATIBA


Bunge Maalum la Katiba lipo njiapanda baada ya kuwapo mivutano isiyoisha miongoni mwa wajumbe huku kukiwa na taarifa kwamba ikiwa leo muafaka kuhusu upigaji kura hautapatikana, baadhi ya wajumbe watajiuzulu.

 
Ikiwa hali hiyo itatokea, uwezekano wa Mkutano wa Bunge hilo kuendelea ni mdogo hivyo linaweza kuvunjika.
 
Taarifa za uhakika kutoka Dodoma zinaeleza kuwa baadhi ya wajumbe wanataka kura ya leo inayolenga kuamua juu ya kanuni za bunge hilo katika kupitisha rasimu ya katiba iwe ya siri au ya wazi, nayo iwe ya wazi.
 
“Kwa kweli hadi sasa tuna zaidi ya majina 250 ya wajumbe ambao wanapinga vikali jaribio lolote la kutaka kura ya kumua kanuni leo iwe ya wazi badala ya siri. Hili likitokea nafikiri Bunge hili litakuwa limefikia ukomo,” kilisema chanzo chetu kutoka Dodoma na kuongeza kuwa:

 
“Yaani ni mambo ya kushangaza saba, Chama Cha Mapinduzi inaelekea kimetoa maelekezo kuhusu hali hii. Waameamu kutumia njia hii kuwatisha wabunge. Wanataka kutumia wingi wao vibaya kushawishi vitu ambavyo havina maana.”
 
Kutokana na mvutano huo, wajumbe hao wameazimia kuwa leo watajiuzulu ujumbe kwenye Bunge hilo kwa madai kwamba wenzao hasa wanaotoka CCM, wanataka kura ya wazi kuamua mgogoro uliokuwa umetokea wiki iliyopita kuhusu upigaji kura wa kupitisha rasimu ya kanuni zitakazosimamia uendeshaji wa Bunge hilo.