Monday, 3 March 2014

MILIPUKO YATOKEA NIGERIA 


Mji wa Maiduguri uliopo kazkazini mwa Nigeria umekumbwa na milipuko miwili, huku ripoti zikiarifu kwamba takriban watu 10 huenda wamepoteza maisha yao.

Mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Ufaransa kwamba mlipuko wa kwanza ulitokea katika eneo lililojaa watu huku wa pili ukilipuka wakati majirani walipokuwa wakiwasaidia waathiriwa.
Maafisa wa polisi wamesema kuwa watu wengi wamekwama chini ya vifusi.
Mji wa Maiduguri hutumiwa kama kambi ya wanajeshi wanaopigana na wanamgambo wa kiislamu wa Boko Haram.

Awali ripoti zimearifu kuwa kulikuwa na shambulizi la angani katika kijiji kimoja cha jimbo la Borno siku ya ijumaa.

Shahidi mmoja ameiambia BBC kwamba takriban raia 20 wamefariki.
Jeshi la Nigeria linadaiwa kuvilipua vijiji inavyoamini ni makao ya wanachama wa Boko Haram.

Sunday, 2 March 2014

LUKUVI AKATALIWA WAZO LA KUTOVIPA UHURU VYOMBO VYA HABARI

 
 
Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum kuhusu Rasimu ya Kanuni za bunge hilo, Profesa Costa Ricky Mahalu, imewaumbua wajumbe wake akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Bunge na Sera), William Lukuvi.
 
Lukuvi na wajumbe wengine, wanatajwa kuwa vinara wa kutaka waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia na kuripoti habari za kamati za bunge hilo wakati zitakapokuwa zikikutana.
 
Akijibu hoja mbalimbali za wajumbe hao wakati akihitimisha semina kuhusu rasimu ya Kanuni za Bunge juzi usiku, Profesa Mahalu alisema, kamati yake imeona hakuna sababu kwa waandishi wa habari kuzuiwa kuhudhuria vikao hivyo na kuripoti habari zitakazokuwa zikijadiliwa.
 
Alisema kamati imeona kuwa mchakato huo unawahusu wananchi na sio vema kuwanyima uhuru na haki ya kupata habari kuhusu kinachoendelea, kupitia waandishi wa habari.
 
Mapema wiki liyopita akichangia semina hiyo, Lukuvi alisema waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia kwenye kamati hizo na kuripoti.
 
“Tuache wajumbe wamenyane humo ndani hata waandishi wa habari wasiwepo, ila wataalam wanaweza kuitwa kama kutakuwa na hitaji,” alisema.
 
Mjumbe mwingine Kidawa Hamid Swalehe, aliungana na Lukuvi pale aliposema wageni pamoja na waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia kwenye kamati.
 
“Waandishi wa habari wasiruhusiwe kuingia kwenye kamati, no,” alisema.
 Lakini mjumbe Esther Bulaya, (Mbunge Viti Maalum CCM) ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, alipinga hoja ya ‘akina Lukuvi’ na kwamba hatakubaliana na kifungu cho chote cha sheria kitakachokuwa kinawekwa ili kuzuia uhuru wa habari.
 
“Napinga kipengele cho chote kinachonyima uhuru wa habari, ni vema waandishi wa habari wakaruhusiwa kuingia na kufanya kazi zao kwenye kamati,” alisema.
 
Pamoja na Bulaya, mjumbe mwingine Maria Sarungi, aliunga mkono waandishi wa habari kuingia kwenye kamati na kuripoti.
 
Naye Dk. Masele Maziku, alisema anashangaa kuna wajumbe wakifanya mkakati wa kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye kamati wakati huo huo wakitaka uwazi katika kupiga kura.

BUNGENI DODOMA

 BUNGE LAWAKANA LIPUMBA NA MBATIA

 

                       LIPUMBA                                                                  MBATIA

Bunge Maalumu la Katiba limesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaoundwa na baadhi ya wajumbe wake, wakiongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR) hautambuliwi.

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashililah, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE Jumapili, mjini hapa juzi.

Dk. Kashililah alisema Ukawa utapata nguvu ya kisheria na kupewa ushirikiano na ofisi ya Bunge iwapo utatambuliwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalumu, ambazo ziko katika mchakato wa kutungwa.

Hata hivyo, Dk. Kashililah alisema ofisi ya Bunge inafahamu kwamba, makundi mbalimbali ya wajumbe wa Bunge hilo yamekuwa yakikutana na kujadili masuala yanayolihusu kila moja.

Kuundwa kwa umoja huo, kulitangazwa rasmi juzi na  Profesa Lipumba, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari na Mbatia.

Profesa Lipumba, Profesa Safari na Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais (NCCR-Mageuzi), wote ni wajumbe wa Bunge hilo. 
Profesa Lipumba alisema umoja huo unaundwa na baadhi ya wajumbe Bunge Maalumu la Katiba kutoka makundi tofauti yanayotambuliwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema lengo la Ukawa, pamoja na mambo mengine, ni kutetea rasimu ya katiba iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Pia alilitaja lengo jingine kuwa ni kuiboresha rasimu hiyo kwa kuzingatia maoni ya wananchi na si `kuchakachuliwa’ kwa misimamo ya vyama, taasisi au makundi ya kijamii.

Profesa Lipumba alisema miongoni mwa sababu za kuundwa kwa Ukawa ni matamko ya baadhi ya viongozi kuwa, Bunge Maalumu la Katiba linaweza kuja na maoni tofauti na yale ya wananchi yaliyoratibiwa na Tume ya Warioba.

Matamshi hayo yalitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, wiki iliyopita na kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari.

WATOA CHANJO WASHAMBULIWA PAKISTAN


Watu wapatao 11 wameuawa katika shambulio la bomu dhidi ya watoa chanjo ya polio kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara lilifyatuka wakati msafara uliokuwa ukilindwa na polisi ukipita katika kijiji kimoja katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa karibu na mpaka na Afghanistan.
Shambulio hilo ni jipya kabisa miongoni mwa mashambulio yanayowalenga watoa huduma ya chanjo ya polio nchini Pakistan.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, lakini kundi la Taliban limekuwa likipinga mipango ya utoaji wa chanjo ya polio, mipango ambayo wanaichukulia kama mbinu ya ujasusi wa kimataifa.
Taarifa za awali zilisema msafara huo ulishambuliwa na makombora mawili tofauti siku ya Jumamosi.

Milipuko hiyo imeripotiwa kufuatiwa na mapigano makali ya bunduki kati ya majeshi ya usalama na wanamgambo.

Maafisa wamethibitisha kuwa watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo walikimbizwa katika hospitali ya karibu. Baadhi ya waliojeruhiwa wanasemekana kuwa katika hali mbaya.

Pakistan imeshuhudia vitendo vya ghasia kufanyiwa wafanyakazi wa afya, ambao wanamgambo wanawatuhumu pia kuwa sehemu ya njama za nchi za magharibi kupunguza idadi ya Waislam.

Zaidi ya watu 40 wanaohusishwa na mpango wa chanjo wameuawa nchini Pakistan tangu Desemba 2012.

Mwezi uliopita, watu wenye silaha wasiofahamika waliwaua kwa kuwapiga risasi wafanyakazi watatu wa kutoa chanjo ya polio, katika mji wa Karachi ulioko kusini mwa Pakistan, siku moja baada ya serikali kuanza zoezi la chanjo kwa nchi nzima.

Pakistan ni moja kati ya nchi tatu zinazokabiliwa na milipuko ya ugonjwa wa polio, duniani zikiwemo Nigeria na Afghanistan.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Pakistan ilikuwa na wagonjwa 91 wa polio mwaka jana, wakiwa wameongezeka kutoka idadi ya wagonjwa 58 mwaka 2012.

Saturday, 1 March 2014

 WAJUMBE WA ODM KENYA WAZUA VURUGU


Vurugu zimezuka katika uchaguzi wa kuwachagua maafisa wapya wa chama kikuu cha upinzani cha ODM nchini Kenya, chake aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo Raila Odinga.

Polisi waliwasili katika ukumbi wa uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani viungani mwa jiji la Nairobi kurejesha utulivu baada ya baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliodaiwa kuwa walinda usalama kurusha vita pamoja na masanduku ya kupigia kura wakijaribu kuvuruga uchaguzi huo.
Ugomvi ulizuka baada ya kuzuka madai kuwa kulikuwa na orodha ya wajumbe bandia iliyokuwa ikisambazwa pamoja na makaratasi bandia ya kupigia kura. Mbunge maalum Isaac Mwaura ambaye anaishi na ulemavu wa ngozi-Albino-alionekana akisukwasukwa na wajumbe baada ya kuzua zahama kuhusu madai hayo ya udanganyifu katika zoezi hilo la upigaji kura.

Chama cha ODM ndicho chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini Kenya kikiwa na idadi kubwa ya wabunge katika bunge la kitaifa pamoja na Senate. Chama hicho kimemudu mgao mkubwa zaidi wa pesa za kufadhili shughuli za vyama vya kisiasa kutoka kwa serikali ya Kenya.

Kutokana na raslimali za chama hicho uchaguzi wa leo umeonekana kuzua msisimko mkali pamoja na patashika baina ya wanasiasa mashuhuru ambao wanagombania vyeo mbali mbali.

Bwana Odinga ambaye alishindwa na rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliokumbwa na madai ya udanganyifu mwezi Machi mwaka uliopita anatetea kiti chake kama kiongozi wa chama, dalili kwamba huenda akagombea tena kiti cha urais mwaka 2017.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji kura Bwana Odinga alizungumzia maswala mbali mbali yanayohusiana na usalama nchini Kenya pamoja na kuiponda serikali ya mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta kwa kushindwa kuleta suluhu ya matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wakenya.

FAIDA ZA PARACHICHI MWILINI


 


Kama yalivyo matunda yote kwa ujumla kuwa yana faida sana katika mwili wa binadamu, vivyo hivyo na Parachichi. Tunda hili lina maajabu makubwa katika kupambana na maradhi hatari ya moyo na sataratani ya matiti kutokana na virutubisho ilivyonavyo.

Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi juu ya tunda hili, awali ya yote tunda hili lina kirutubisho aina ya Aloic Acid ambayo ni aina fulani ya mafuta mazuri yanayosaidia kushusha kolestrol mwilini. 


Katika utafiti mmoja waliofanyiwa watu kadhaa waliokuwa na matatizo ya kolestro mwilini, baada ya kutumia maparachichi kwa muda wa siku saba, walionesha mabadiliko mazuri katika afya zao kwa kupungua kiwango cha kolestro mbaya mwilini.

Aidha, parachichi lina kiwango kikubwa sana cha madini aina ya potasium ambayo ni muhimu sana katika kuimarisha mzunguruko wa damu mwilini. 

Inaelezwa kwamba ulaji wa kiwango kikubwa cha madini ya potasiamu, hutoa kinga madhubuti dhidi ya magonjwa yatokanayo na mzunguruko mbaya wa damu mwilini, kama vile ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu na kiharusi.
 

Mbali ya madini hayo, parachichi lina virutubisho vingine kama vile Folate (Folic acid) ambacho ni muhimu sana kwa afya na ustawi wa moyo, kwa maana hiyo watu ambao wanakula sana vyakula kama parachichi lenye kirutubisho hicho, watukuwa salama dhidi ya magonjwa ya moyo au kiharusi kwa asilini 55.
Kirutubisho kingine kinachopatikana kwa wingi kwenye parachichi ni Fatty Acids, ikiwemo Oleic Acid.


Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, imedhihirika kwamba virutubisho hivyo ni kinga tosha dhidi ya saratani ya matiti. Kwa maana nyingine, wanawake wanaokula kwa wingi maparachichi, wanaipa miili yao kinga dhidi ya saratani hiyo ambayo hivi sasa imekuwa tishio miongoni mwa wanawake nchini.

Parachichi linaweza kuliwa kama mtu atakavyopenda, wapo watu wanaopenda kula bila kuchanganya na kitu kingine, lakini pia parachichi linaweza kuliwa kwa kupaka kwenye mkate badala ya Blue Band. Halikadhalika parachichi linaweza kuliwa kwa kuchanganya na nyanya, vitunguu, ndimu na chumvi kidogo kama kachumbari ya kipekee.

VIRUTUBISHO VYA PARACHICHI
Kwa ujumla, parachichi ni chanzo kizuri cha Vitamini K, Vitamini B6 na Vitamini C.


Aidha, tunda hili lina kiwango kizuri cha virutubisho aina ya Folate, kopa na ufumwele (Fiber). Fiber ni muhimu katika kuwezesha mtu kupata choo laini na bila matatizo. Bila kusahau kwamba tunda hili ni chanzo kizuri pia cha madini ya Potasiamu: ina kiwango kikubwa kuliko hata ndizi.


Ingawa parachichi ni tunda, lakini lina kiwango kikubwa cha mafuta (fats) ambayo yanakadiriwa kuwa kati ya asilimia 71 – 88, kiwango ambacho ni cha juu kwa asilimia 20 ukilinganisha na matunda mengine. Kwa wastani, parachichi moja lina gramu 30 za mafuta, lakini kati ya hizo, gramu 20 ni za mafuta mazuri kiafya (Monounsaturated fats na Aloic Acid) ambayo husaidia kujenga afya bora mwilini.


Utafiti zaidi kuhusu tunda hili unamalizia kwa kusema kwamba parachichi lina takribani aina 20 za Vitamin, madini na virutubisho muhimu (Phytonutriens) ambavyo hutuo kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mengi hatari. Baadhi ya Vitamini zilizomo na asilimia zake kwenye mabano ni pamoja na Vitamin E (4%), Vitamin C (4%), Folate (6%), Fiber (4%), Iron (2%) na Potasium (4%).
 

Kwa ujumla tunda la Parachichi lina faida nyingi kiafya na tunatakiwa tuyale kwa wingi, hasa ukizingatia huu ndiyo msimu wake. ni jambo la kushangaza sana kuona kwamba watu wengine msimu wa maparachichi unaingia hadi unakwisha, mtu hajala hata moja. KUMBUKA KINGA NI BORA KULIKO TIBA!

 UKRAINE KUOKOLEWA KIUCHUMI

 

Rais wa Urusi Vladmir Putin amewaagiza maafisa wake kuanza kufanya mashauriano na mataifa ya Magharibi ili kubuni mikakati ya kukwamua Ukraine kutoka katika matatizo ya kiuchumi.

Lakini kwa kile ambacho waandishi wa habari wanasema ni habari za kuhitilafiana kutoka Moscow, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo imetoa taarifa inayokosoa vikali Serikali mpya ya Ukraine.
Alhamisi wiki hii Rais Putin aliamuru zoezi la kijeshi kufanyiwa karibu na mpaka na Ukraine.

Naye Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry amesema kuwa mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, amemhakikishia kwamba Urusi itaheshimu Uhuru na mipaka ya Ukraine.

Hata hivyo John Kerry amesisitiza kuwa Marekani inafuatilia kwa makini vitendo vinavyofanywa na Urusi kuhusiana na Ukraine.
Wakati huohuo habari zinasema kuwa watu wenye silaha wameteka uwanja wa ndege wa jimbo la Cremea wa Simfer-ropot.

Habari hizo zimetangazwa na shirika la habari la Urusi la Interfax na lingine la Ukraine la UNIAN, zinasema kuwa watu 50 wenye silaha walifika kwenye uwanja huo katika malori huku zikipeperusha bendera za Urusi.
Crimea ni jimbo la pekee kubwa katika Ukraine ambalo lina watu wengi wenye asili ya Urusi.

Mapema Alhamisi, kundi la wanajeshi waliokuwa wamevalia sare rasmi , bila nembo rasmi walivamia Bunge la eneo hilo la Crimea na kuwatimua Mawaziri