WAANDISHI AL JAZEERA WAHUKUMIWA MIAKA 7 JELA
Mahakama nchini Misri imewahukumu jela miaka saba
wandishi watatu wa habari wa shirika la habari la Al Jazeera waliokuwa
wamezuiliwa kwa miezi sita nchini humo.
Walipatikana na hatia ya kueneza habari za kupotosha na kushirikiana na kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Muslim Brotherhood.
Mmoja wa wandishi hao ni Peter Greste, raia wa Australia na ambaye pia alikuwa mwandihi wa habari wa BBC wakati moja.
Hukumu ilipotolewa, Greste kwa hasira aligonga
mkono wake katika eneo ambako walikuwa wamezuiliwa huku mwenzake
akibururwa kutoka mahakamani na walinzi wa gerezani.
Familia za watuhumiwa nao wakaangua kilio. Kesi
hii imelaaniwa sana kote duniani hasa na mashirika ya kutetea haki za
binadamu pamoja na mashirika ya habari ya kimataifa.
Lakini nchini Misri, vyombo vya habari vilipeperusha habari hiyo kwa utofauti mkubwa.
Al Jazeera - ni shirika linaloonekana kuunga
mkono vuguvugu haramu la Muslim Brotherhood na kwa mtanzamo huo , ni
adui wa serikali.
Peter Greste ,ndiye alikuwa anaripoti matukio nchini Misri Disemba mwaka jana wakati wa harakati za mapinduzi.
Kisha yeye na wenzake wawili wakatuhumiwa kwa
kusaidia vuguvugu la kigaidi na kutangaza taarifa za kupotosha dhidi ya
serikali na maslahi ya taifa hilo.
Madai ambayo serikali ya Australia imekuwa ikikanusha vikali.
Serikali ya Australia ilitoa taarifa yake
ikisema kuwa imeshtushwa sana na uamuzi wa mahakama katika kesi ya Peter
Greste. Imeelezea kushangazwa sana na hukumu iliyotolewa. Serikali
imesema haielewi kabisa matukio haya.
Shirika la Al Jazeera lenyewe limepinga hukumu
iliyotolewa dhidi ya wandishi hao, Peter Greste, Mohamed Fahmy na Baher
Mohamed likisema kuwa inakiuka sheria.