Monday, 7 April 2014

 DK BALALI AMVAA MAALIM SEIF

 

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema serikali ya mkataba haiwezi kuleta maendeleo nchini, bali ni kujidanganya na kujirudisha nyuma kimaendeleo.Aliyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho katika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti, visiwani hapa.


Alisema serikali tatu haziwezi kutatua kero za Muungano, hivyo CCM itahakikisha inaendeleza mfumo wa Muungano wa serikali mbili.
“Tunaendelea kupigania serikali mbili. Tunafanya hivyo kwa sababu tunaipenda Zanzibar na Tanzania yetu,” alisema Dk. Bilal.


Aliwataka Wazanzibar kutokuwa na hofu kwa kuwapo kwa serikali mbili kwamba watamezwa na Muungano na kuwatoa wasiwasi kuwa Muungano hautaibeza Zanzibar.
Alisema Tanganyika na Zanzibar zimeonyesha mfano mzuri wa kumkomboa Mwafrika kwa kuunganisha nchi mbili na kuwa Tanzania, kwani nchi nyingi zilikuwa zikitafuta umoja huo lakini zilishindwa.


 “Leo nini kutafuta mbinu za kuutaka kuuvunja Muungano ambao umepanua fursa kwa Wazanzibari bila ya Muungano Wazanzibari tungebanana, Muungano umetusaidia kufifisha uhasama uliokuwapo ndani ya Zanzibar na kujenga umoja na kusahau tofauti zilizopo,” alisema Dk. Bilal. 


Alisema Watanzania wengi wanataka serikali mbili, hivyo watahakikisha wanaendeleza mfumo wa serikali mbili, kwani katika watu 100 asilimia ya watu 86 hawana tatizo na Muungano uliopo.Alitahadharisha kuwa Muungano hauwezi kudumu bila ya serikali mbili katika nchi zenye tofauti ya ukubwa wa nchi moja ndogo na nyingine kubwa, ni lazima kuwapo na uwiano utakaodumisha Muungano.


 Alisema CCM haitishiki na vitisho vya upinzani vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwa lengo la kutaka kuuvunja Muungano.
Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi, Mwangi Kundya, alisema mfumo wa Muungano wa serikali mbili umetoa fursa ya kupanuka kwa soko la biashara, ajira na uwekezaji katika nyanja mbalimbali na kuimarisha huduma za kijamii ikiwamo elimu, afya na umeme.


 Alisema hotuba ya Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, aliyoitoa hivi karibuni katika mkutano wa hadhara ilionyesha kukata tamaa, baada ya kuona dereva makini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonyesha na kuweka bayana mitego yote ambayo wao walitamani Tanzania iingie. 


“Dereva huyo baada ya kuwaonyesha wajumbe wa Bunge la Katiba mitego hiyo sasa wana hakika hawawezi kufanikiwa nia yao ila wanaona bora litote tugawane mbao,” alisema Kundya.


Aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kutambua dhima waliyonayo ya kuulinda, kuutetea Muungano na kutotazama takwimu zilizotolewa kwa ufinyu wake, bali wazichambue na kuzitazama kwa upana wake ili kubaini Watanzania wanachokitaka.

No comments:

Post a Comment